Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Tafakari ya Neno la Mungu

Tafakari ya kina kuhusu Fumbo la Pasaka

Kiini cha imani katika ufufuko ni tukio la kihistoria lililoshuhudiwa na wafuasi ambao walikutana kweli na Kristo Yesu, Mfufuka.

31/03/2018 13:51

Usiku wa Mkesha wa Pasaka ni muhimu sana katika maisha ya Kanisa kwani tunakumbuka Siku ya kufufuka kwake Kristo. Yesu Kristo hakufa tu bali amefufuka. Yesu asingelifufuka kusingelikuwa na maaana yo yote ya kuja kwake duniani na Ukristo usingekuwepo. Adhimisho hili latangaza mwisho wa mauti na kutangaza mwanzo wa uzima wa milele. Kristo Yesu ameshinda mauti. Alama ya Mshumaa wa Pasaka ni mwanga, kielelezo cha mwanzo mpya. Kuhusu kifo cha Yesu maelezo juu ya mateso katika maandiko matakatifu hayatofautiani. Habari ya hukumu kifo na maziko ya Yesu iko wazi kabisa na Wainjili wameandika vizuri. Kuhusu ufufuko; Injili, Matendo ya Mitume na Nyaraka za Mtume Paulo maelezo juu ya ufufuko yanatofautiana lakini shida si kwamba Yesu hakufufuka au la. Tofauti kubwa ni nani alitokewa mara ya kwanza na Kristo na alimtokea wapi au alitokea wapi kwanza.

Wapi? Wainjili Mathayo na Yohane wanasema Yesu alimtokea kwanza Maria Madgalena na wenzake huko Yerusalem- Yoh. 20:15 mama unalia nini? Unamtafuta nani? Naye akidhania ya kuwa ni mtunza bustani, akamwambia Bwana, ikiwa umemchukua wewe, unaiambie ulipomweka, nami nitamwondoa ……. Baadaye Mariamu akaenda akawapasha habari wanafunzi wake ….  Nimemwona Bwana.

Alitokea wapi? Yohane na Luka – wanasema aliwatokea wanafunzi wake huko Yerusalemu. Marko na Mathayo wanasema huko Galilaya.. Tofauti hii ya mahali si shida kubwa – jambo la msingi ni kuwa Yesu amefufuka na kuwatokea wafuasi wake kitu ambacho kinazindua jumuiya ya wakristo. Ukweli kuhusu ufufuko unaendelea kutoa ushuhuda. Baada ya kifo chake mitume walitawanyika - tulidhani kwamba angetukomboa - wale wa Emaus wanasema hivi. Hakika walipoteza matumaini. Halafu – tena tunasikia wakimhubiri Kristo mfufuka, wanakufa juu yake - ni nini kilichowafanya wawe tayari kufa kwa ajili ya Kristo kama kweli Kristo hakufufuka?

Tunasikia mitume wanaishi maisha mapya ya ufufuko - wakieleza wazi kile kilichowapata. Hawakuwa tayari kudanganya. Mtu mmoja anasema; BILA UFUFUKO, UKRISTO NA KANISA VINGEBAKI NI FUMBO ZAIDI YA FUMBO LENYEWE LA UFUFUKO. Kwamba Kristo ni mzima - anatupatia maisha mapya ya mitume. Angalia jumuiya ya kwanza ya wakristo – Mdo. 2:42. Mtakatifu Agostino anasema; anamgusa Kristo, anayemwamini Kristo. Hakuna ufufuko, hakuna Ukristo. Mfano wa umeme ukizima usiku, hakuna mwanga wowote. Katika Rom. 10:9 tunasoma - kwa sababu ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. Sisi  tuko hapa kwa sababu ya imani hiyo. Tena Mtakatifu Agostino anasema imani ya kikristo ni imani ya ufufuko. Wengi hutambua/huamini kifo cha Kristo hata wapagani. Mahali alipozikwa panajulikana na wote/wengi. Wakristo huenda zaidi,  kwamba Kristo amefufuka na mtu hawezi kuitwa mkristo asipoamini katika ufufuko wa Kristo.

Huko kumfufua Kristo ni kwamba Mungu amethibitisha agano alilosema – Mdo, 17;13 - kwa maana ameweka siku atakayowahukumu walimwengu kwa haki, kwa mtu yule aliyemchagua, naye amepewa watu wote uthabiti wa mambo haya kwa kumfufua katika wafu. Mtume Paulo akiandika miaka 25  baada ya ufufuko wa Bwana anashuhudia hivi: 1 Kor. 15:1-8 tunasoma hivi, basi ndugu zangu, nawaarifu ile Injili niliyowahubiria, ambayo ndiyo mliyoipokea, na katika hiyo mnasimama, na  kwa hiyo mnaokolewa, ikiwa mnayashika sana maneno niliyowahubiri, isipokuwa mliamini bure. Kwa maana naliwatolewa ninyi hapo mwanzo yale niliyoyapokea mimi mwenyewe, ya kuwa Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yanenavyo maandiko, na kuwa alimtokea Kefa, tena na wale thenashara, baadaye aliwatokea ndugu zaidi ya mia tano pamoja, akamtokea Yakobo tena na mitume wote, na mwisho wa watu wote, alinitokea mimi, kama ni mtu aliyezaliwa si kwa wakati wake. Tunahitaji tena ushuhuda mwingine zaidi ya huo?

 

UFUFUKO WA KRISTO – NI TOFAUTI NA UFUFUKO WETU.

Katika Agano la Kale tuna habari ya kina Enoko, Nabi Eliya aliyechukuliwa kwa upepo wa kisulisuli baadaye hatusikii tena habari zao. Katika Agano Jipya tuna habari ya Bikira Maria kupalizwa Mbinguni dhihirisho la utukufu wa mwili na mwanadamu. Yeye anapalizwa mbinguni. Ufufuko wa Kristo ni tofauti na ufufuko mwingine  - KKK 646 - ufufuko wa Kristo haukuwa kurudi katika maisha ya kidunia, kama ilivyokuwa ufufuko mwingine alioufanya kabla ya Pasaka, kama ule wa binti Yairo, wa kijana wa Naim, wa Lazaro. Kwa kweli haya yalikuwa ni matokeo ya miujiza lakini wale waliotendewa miujiza waliyarudia maisha ya kidunia ya kawaida. Katika mwili wake uliofufuka, anapita kutoka hali ya kifo kufikia maisha mengine yaliyo juu ya wakati na mahali. Mwili wa Yesu katika ufufuko umejazwa nguvu ya Roho Mtakatifu, unashiriki maisha ya uzima wa kimungu katika hali ya utukufu wake hivi kwamba Mt. Paul anaweza kusema kuwa Kristo ni mtu mbinguni -  1 Kor 15,35-50.

JE, SISI NASI TUTAFUFUKA?

Ufufuko ni nini? Mtunga Zaburi 16 (Mungu unihifadhi mimi, kwa maana nakukimbilia.....) anamchagua Mungu kama hazina yake bora. Anataka kukaa pamoja naye mpaka milele, lakini anaogopa kumpoteza saa ya kufa atakapokwenda kuzimu – Zab 49 ;15. Katika tamaa yake ya kuishi na Mungu anaanza kutumaini kwamba Mungu atajua njia ya kumtoa kuzimuni. Hiyo njia imekamilishwa na Yesu Kristo mwenyewe. Katika Hek. 11;12 tunasoma hivi; mwadilifu, maana yake asiye na dhambi, afungamanaye na Mungu, hafi kabisa – lakini wewe unaviachilia vyote kwa kuwa ni vyako, Ee Mfalme Mkuu mpenda roho za watu, maana roho yako isiyoharibika imo katika vyote.

Kwa njia ya Kristo sisi tunapata uzima mpya.

Rum. 8,29, maana wale aliowajia tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu. 2 Kor 5,17 – hata imekuwa mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya, ya kale yamepita tazama yamekuwa mapya. Yoh 14, 5-6 Tomaso akamwambia Bwana sisi hatujui uendako nasi twaijuaje njia? Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia na kweli na uzima, mtu haji kwa Baba ila kwa njia ya mimi. Yoh. 3,5 –Yesu akajibu amini, amini, nakuambia, mtu asipozaliwa kwa maji na roho hawezi kuuingia ufalme wa Mungu. Mk. 16,16 aaminiye na kubatizwa ataokoka asiyeamini atahukumiwa.

Namna gani tutafufuka? KKK 999- tunasoma na kuamini kuwa – Kristo amefufuka pamoja na mwili wake hasa - tazameni mikono yangu na miguu yangu ya kuwa ni mimi mwenyewe - Lk 24,39, lakini hakuurudia uzima wa kidunia. Wakati huo huo ndani yake wote watafufuka pamoja na miili yao wenyewe waliyo nayo sasa, lakini mwili huo utageuzwa katika mwili mtukufu, katika mwili wa kiroho - Fil. 3,21; 1 Kor. 15,44.  Labda mtu atasema wafufuliwaje wafu? Nao huja kwa mwili gani? Ewe mpumbavu, uipandayo haihuiki isipokufa, nayo uipandayo hupandi mwili ule utakaokua ila chembe tupu.... hupandwa katika uharibifu hufufuliwa katika kutoharibika, wafu watafufuliwa wasiwe na uharibifu ... maana sharti huu uharibikao uvae kutoharibika, nao huu wa kufa uvae kutokufa- 1 Kor 15,35-53.

Mtume paulo anatufundisha sisi sote kwamba watu wote wazima kwa wafu wamwaminio Kristo watafufuliwa na kushirikishwa utukufu wa mbinguni. Soma zaidi  1 Thes. 4:13-18 akiandika habari kuhusu kufufuka kwa wafu na kusubiri kwake siku ya Bwana mtume Paulo anaandika hivi maana ikiwa twaamini ya kwamba Yesu alikufa, akafufuka vivyo hivyo na hao waliolala katika Yesu, Mungu atawaleta pamoja naye;..... kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza kisha sisi tulio hai, tuliosalia tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu ili tumlaki Bwana hewani na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele. Rom 1,4 tunasoma hivi Mungu Baba atawafufua wakristo kwa nguvu ile ile na kwa karama ile ile ya roho kama alivyomfufua Yesu Kristo.

Nani atafufuka? Katika KKK 998- tunasoma hivi .. Watu wote waliokufa - wale waliofanya mema kwa ufufuko wa uzima, na wale waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu - Yoh 5,29; Dan 12,2 –tena, wengi wa hao walalao katika mavumbi ya nchi wataamka, wengine wapate uzima wa milele, wengine aibu na kudharauliwa milele. Tunasoma pia katika 1Thes. 4,14 kuwa - maana ikiwa twaamini ya kwamba Yesu alikufa akafufuka, vivyo na hao waliolala katika Yesu Mungu atawaleta pamoja naye. Ufufuko wa mkristo wategemea ufufuko wa Kristo.

Katika KKK – 1005 – tunaambiwa kuwa ili kufufuka pamoja na Kristo ni lazima kufa pamoja na Kristo, ni lazima kutokuwamo katika mwili na kukaa pamoja na Bwana – 2Kor. 5,8 – lakini tunao moyo mkuu, nasi tunaona ni afadhali kutokuwamo katika mwili na kukaa pamoja na Bwana. Katika kwenda huko, yaani kifo, roho hutengana na mwili – Fil. 1,23. Nayo itaungana na mwili wake siku ya ufufuko wa wafu. 1Kor 15,20 - lakini sasa Kristo amefufuka toka wafu, limbuko lao waliolala. Kwa kifupi ufufuko wa wakristo wategemea ufufuko wa Kristo. Mtu hajifufui mwenyewe bali kwa njia ya Kristo. Mungu Baba anawafufua wakristo kwa nguvu ile ile na karama ile ile aliyomfufua Yesu Kristo. Tunaamini kwamba mkristo amepewa uzima mpya unaomfanya kuwa mtoto wa Mungu – Rum. 8,14- kwa kuwa wote wanaoongozwa na Mungu, hao ndio wana wa Mungu. Mungu Baba huunganisha Kristo mfufuka na mkristo kwa imani na ubatizo – Rum. 1,16;6,4, - basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima.

TUNAISHI NAMNA GANI HUU UFUFUKO?

Ingefaa tujiulize sote tulioko hapa, huu ushuhuda wa utukufu wa ufalme wa Mungu unaoonekana kati yetu ni kwa kiasi gani tunauthibitisha katika maisha ya kawaida. Ni kwa nini bado dunia inagubikwa na dalili zaidi za kifo kuliko za ufufuko? Angalia ufisadi, uongo, tamaa ya madaraka na fedha tamaa za mwili zilizokithiri, ukosefu wa uaminifu, uvunjivu wa amani na haki katika familia, jumuiya na jamii, ubinafsi, mauji ya maalbino, kutokuwa tayari kukubali na kusema ukweli, uvivu na mambo kama hayo. Je kuna kasoro mahali gani kuhusu ufahamu wetu juu ya ufufuko wa Bwana? Je sisi tulioko hapa na tunaoamini katika ufufuko hatuwezi kufanya zaidi ya hiki tunachofanya au tulichokifanya? Tunashudiaje huu ufufuko?

Katika Yoh. 11: 17-27 tunasoma kuwa, Yesu alipofika, alimkuta Lazaro amekaa kaburini kwa siku nne.  Mji wa Betania upo karibu na Yerusalemu, kadiri ya maili mbili hivi. Wayahudi wengi walikuwa wamefika kwa Martha na Maria kuwapa pole kwa sababu ya ndugu yao. Martha aliposikia kwamba Yesu anakuja, alikwenda kumlaki; lakini Maria akaendelea kukaa nyumbani. Martha akamwambia Yesu, Bwana, kama ungalikuwa hapa, kaka yangu hangalikufa. Lakini hata sasa najua ya kuwa Mungu atakupa cho chote utakachomwomba. Yesu akamwambia, kaka yako atafufufuka. Martha akamjibu, najua atafufuka siku ya mwisho. Yesu akamwambia, Mimi ni ufufuo na uzima; anisadikiye mimi hata kama atakufa, ataishi, na kila anayeishi na kunisadiki hatakufa milele. Je, wasadiki hayo? Naye akamjibu, ndiyo Bwana, nasadiki ya kuwa wewe u Kristo, Mwana wa Mungu, atakayekuja ulimwenguni humu. Hapa Yesu anadhihirisha wazi kuwa yeye ndiye ufufuko na uzima.

Hata hivyo: Ukuu wa ufufuko wa Kristo ni uhakika wa ufufuko wetu. Kwamba sisi hatutakufa kamwe. Kifo cha Kristo huonesha upendo wake na ukamilifu wa upendo huo ni ufufuko wake. Leo tuna haki ya kuimba na mzaburi - 118,24 siku hii ndiyo aliyoifanya Bwana tutashangilia na kuifurahia. Aleluya, Aleluya. Amina. Heri na Baraka tele katika sikuku ya ufufuko wa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo.

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.

31/03/2018 13:51