Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Tafakari ya Neno la Mungu

Fumbo la Pasaka liwaletee uhuru kamili, haki, amani, upendo na ustawi

Maadhimisho ya Fumbo la Pasaka yawawezeshe waamini kuuvua utu wake uliochakaa kutokana na dhambi na kumvaa Kristo Yesu, Mfufuka ili kuanza kutembea katika neema ya utakaso! - AP

31/03/2018 12:35

Nchi inapopata uhuru wake wa bendera, raia wake wanasherehekea uhuru kutoka utumwa wa utawala wa wakoloni. Kadhalika mfungwa atokapo gerezani anafurahia uhuru aliorudishiwa. Leo wakristo popote duniani tunasherekea sikukuu ya Uhuru tukikumbuka siku tulipokombolewa na Bwana wetu Yesu Kristo kutoka utumwa wa dhambi na ukoloni wa utawala wa shetani. Tukiwa kama taifa huru sasa tunasafiri na Mkombozi wetu tukiwa kifua mbele kuelekea nchi ya ahadi. Kwa hiyo tunatakiana “Heri kwa Pasaka na tunaimba Aleluya!” kwa siku hamsini hadi Pentekoste, Siku kuu ya kuzaliwa kwa Kanisa, siku ambayo Mitume walitoka kimasomaso kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kuhusu: Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo kwa wafu!

Neno Pasaka kwa Kilatini ni transitus – maana yake kuvuka, kutoka, kupita. Asili ya sikukuu ni Wayahudi, walipokombolewa kutoka utumwani Misri, walivuka bahari ya shamu na kuingia nchi ya ahadi. Wakristo wameichukua Pasaka ya Wayahudi na kuipatia maana mpya ya mateso ya ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristu. Katika safari ya maisha ya Yesu unakuta harakati nyingi za kuingia na kutoka ya transitus na kuvuka huko. Harakati za kuingia na kutoka zinaonekana zaidi wakati wa mateso, kufa na kufufuka kwake. Hebu tumfuatilie.  Masimulizi ya mateso ya Yesu yanaanza hivi: “Basi kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu, hali akijua ya kuwa saa yake imefika, atakayotoka katika ulimwengu kwenda kwa Baba, […]” (Yn. 13:1). Kwa hiyo mateso na ufufuko ni kutoka kwa Yesu hapa duniani na kuingia katika ulimwengu wa Mungu.

Pasaka ya kuvuka kijito cha Kedroni na kuingia Getsemani: “Wakati ule Yesu alitoka pamoja na wanafunzi wake kwenda ng’ambo ya kijito cha Kedroni.” Usiku wa Pasaka ya Wayahudi, haikuwezekana Myahudi kutoka nje ya mipaka ya hekalu la Yerusalemu. Yesu anavunja sheria. Anatoka nje ya hekalu anavuka mto kedroni na kuingia bustanini Getsemani kwenye gizani mithili ya paradisi iliyoharibiwa na Adamu. Yesu anaingia katika giza la Getsemani yaani katika mateso yaliyopelekea kifo chake. Kabla hajakaa sawa huko bustanini anafika Yuda na kikosi chake. Askari wanashindwa kuingia kwa vile wakati wa usiku bustanini ni pahala patukufu. Kwa hiyo Yesu kwa ujasiri anaenda kuwakabili. Hapa Yesu anapeleka Pasaka kwa askari, yaani wabadili fikra wanapomwona mhalifu akijileta mwenyewe kwao kama alivyofanya Yesu.

Pasaka ya kuingia na kutoka katika Ikulu ya Pilato: Harakati za kuingia na kutoka ziliendelea wakati wa mahojiano ya faragha na mkuu wa mkoa, Pilato aliyewakilisha dola ya kirumi. Pilato anamhoji Yesu ndani ya ofisi ya ikulu iitwayo Praitorio. Wayahudi hawakuthubutu kuingia sehemu hiyo (ya makafiri) wakichelea kujinajisi kabla ya sikukuu ya Pasaka. Yesu anaingia na kufanya majadiliano na mkuu wa dola masuala ya siasa na utawala. Pilato anaonekana mara nyingi akitoka na kuingia Praitorio na mara nyingine akiwa na Yesu anayemtangazisha kwa watu: “Tazama, mtu huyu!”. Kwa hiyo hata serikali inamtambua na kumthibitisha kuwa ndiye binadamu halisi mwenye utu. Kisha Pilato anamkabidhi Yesu kwa Wayahudi, wanaomtwisha msalaba na kutoka ndani ya mji kuelekea Golgota. Kumbe, hata ndani ya utawala wa nchi kunahitajika Pasaka ya kuona na kuheshimu utu na ubinadamu.

Pasaka katika mahojiano na makuhani na waandishi: Katika mahojiano na makuhani na wapambe wa habari, Yesu aliyajibu maswali yao ili kuwapa ujumbe wa kipasaka (kuwaweka huru). Mathalani alipozabwa kofi na kuonywa vikali na kijakazi: “Wamjibu hivi kuhani mkuu!” Yesu alimjibu kijakazi ili kumkomboa dhidi ya unyanyasaji na kumfundisha jinsi ya kutathmini matukio. Lakini maswali mengine hakuyajibu kwani hayakuwa na tija ya kipasaka. Aidha katika mahojiano na Makuhani wakuu, unaweza kuona kuwa walikuwa na woga mkubwa wa Pasaka, yaani waliogopa kuondokana na mtindo wao wa dini na kuingia katika mtindo mpya alioupendekeza Yesu.

Pasaka ya kutoka msalabani na kukabidhi roho yake: Msalabani, Yesu anatoka katika mateso na kukabidhi roho yake, ksha mwili wake unatolewa msalabani na kuingizwa kwenye “kaburi jipya, ambalo hajatiwa bado mtu yeyote ndani yake.” (Yn 19:41), yaani anatoka katika kifo cha upendo na kuingizwa pahala palipohifadhiwa na Mungu. Kumbe ukijitoa sadaka ya upendo unapata utulivu wa moyo.

Pasaka (kuingia na kutoka) baada ya Ufufuko: Baada ya ufufuko tunashuhudia watu wanaingia na kutoka makaburini. Mtu kwanza kuingia na kutoka makaburini ni Maria Magdalena akiwa katika pilikapilika za kumtafuta mpendwa wake wa moyo. Wengine wanaokimbizana kwenda kaburini ni Petro na Yohane. Kijana Yohane anamzidi mbio Petro na kufika wa kwanza. Kisha kuna pilikapilika za kuingia na kutoka kaburini. Yohana anachungulia kaburi bila kuingia ndani. Petro kwa kuchelewa anafika na kuingia, ndipo Yohane naye anaingia na kisha wote wawili wanaona na kusadiki. Kumbe kaburini kwenye giza sasa kutokana na upendo unaona mwanga wa uzima katika wafu.

Maria alibaki nje ya kaburi amejiinamia akilia. Anapoinuka na kuliangalia kaburi anamwona mtu amesimama mbele yake. Lakini anashindwa kumtambua akidhani ni mtunza bustani. Yesu anamwita kwa upendo: “Maria!” Naye akageuka na kumtambua Yesu: “Rabbuni, Mwalimu!”. Ufufuko wa Yesu na kukutana na Maria ni Pasaka. Imebadilisha makaburi (bustani au paradisi ya kifo), na kuwa bustani ya upendo. Kumbe hata sisi tunaweza kusherekea Pasaka daima na kumwona Mfufuka kibinadamu katika uzuri wa uumbaji, kwa njia ya neno linalogusa mioyo yetu. Pasaka ya kuingia kwenye umoja wa upendo: Katika bustani ya upendo, Maria anataka kumshikilia Yesu lakini anakataliwa: “Usinishikilie, kwa sababu bado sijapanda kwenda kwa Baba.” (Yn 20:17). Safari ya kuihitimisha Pasaka inaendelea. Maria inambidi atoke pale bustanini na kwenda kuwahabarisha wanafunzi kwamba Yesu atapaa kwenda kwa Baba ili kuikamilisha Pasaka. Pasaka inakamilika pale mbingu na dunia zinapoungana pamoja. 

Sote tusherekee Pasaka: Ndugu zangu, sikukuu Pasaka inatualika sote tunaomwamini Kristu na hata wasioamwamini Mungu kujikomboa yaani kutoka utumwani na kuwa huru. Pasaka ni mwaliko kwa kila mmoja wetu kujihoji kama yuko katika utumwa wa gani ili kufanya transitus, yaani kujikomboa na kuwa huru. Yesu aliingia katika mapambano na watu wenye fikra za chuki na uhasama lakini kwa upendo wake akaingiza haki. Pasaka inatualika kujinasua kutoka utumwa wa fikra hizo zilizojikita katika serikali, siasa, jamii, kazi, familia na katika dini. Pasaka inatualika kujinasua kutoka utumwa wa matumizi ovyo ya mitandao ya kijamii unatupelekea kususa thamani za mila na desturi zetu na hivi kudhoofisha malezi na elimu. Pasaka inahitajika kutunasua kutoka utumwa mamboleo wa kuwarubuni vijana wa kike na wa kiume kwa malengo ya kifuksa na ya kiuchumi. Pasaka inahitajika kutunasua katika utumwa wa kufanya kazi chafu zinazomilikiwa na nguvu za giza au rushwa. Aidha kujinasua na kujigandamizia mali, utumwa wa kutamani vyeo na kujizolea kiki za kisiasa hadi kuliangamiza taifa na ulimwengu.

Pasaka kuwanasua waandishi wa habari kutoka utumwa kutoa taarifa kavu bila kuzipembua kama yule kijakazi, aliyeirukia mambo na kumpiga Yesu kofi bila kufikiri. Vyombo vya habari vina kazi ya kutoa “Breaking news” ya matukio mabovu. Lakini Pasaka ni kuonesha thamani iliyoko katika hiyo habari yaani kupanda mbegu njema katika mazingira mabovu. Ndiyo maana ya Pasaka ya Yesu kwa upendo wa mateso yake aligeuza ukatili, kuwa wokovu, hadi mateso yake yakaitwa: “kosa lenye heri.” Hii ndiyo “Mantiki ya Habari Njema” anavyosema Papa Francisko. Je, wanahabari wanaweza kuibua thamani ipi chanya katika mazingira ya malumbano ya kisiasa, kwenye mazingira ya kifamilia, ya ajali mbalimbali, katika mauaji mbalimbali, nk Hiyo ndiyo namna ya kusherekea Pasaka yaani uhuru wa kweli. Ndugu zangu maisha ni safari yenye matumaini ya kufika kikomo cha kuungana na Huruma na Upendo ambao ni Kristo mwenyewe. Safari ni Pasaka yaani kujinasua kutoka utumwa wa ubinafsi na uchoyo na kuingia kwenye uhuru wa huruma, upendo na mshikamano. Nakutakia Pasaka njema katika safari yako ya maisha.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.

Vatican News!

31/03/2018 12:35