2018-03-31 11:36:00

Fumbo la Msalaba liwawezeshe waamini kuona aibu na kuwa na matumaini


Tafakari ya Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo mjini Roma, Ijumaa Kuu, 30 Machi 2018, imeandaliwa na jopo la vijana 15 wenye umri kati ya miaka 16-27 walioongozwa na Professa Andrea Monda. Hii ni tafakari ambayo ni mwendelezo wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana itakayofanyika hapa mjini Vatican mwezi Oktoba 2018 ikiongozwa na kauli mbiu “Vijana, imani na mang’amuzi ya miito.” Kwa namna ya pekee kabisa, vijana wameangalia mazingira ya mateso, wamekutana na kusali na Kristo Yesu katika tafakari ya Fumbo la Msalaba mintarafu maisha yao ya ujana!

Mara baada ya Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo, Baba Mtakatifu Francisko alitoa tafakari yake iliyojikita zaidi katika: Injili ya matumaini inayosimikwa katika Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Pili ni toba na wongofu wa ndani kutokana na aibu, usaliti na kutopea katika utumwa wa dhambi na utawala wa Ibilisi, shetani! Kwa kuutema upendo na kumwacha Kristo ateseke peke yake, ingawa Kristo mwenyewe ameendelea kukaa kati pamoja na watu wake.

Baba Mtakatifu anasema, hii ni aibu na usaliti wa kumkataa Yesu na badala yake kumkumbatia Baraba, uchu wa mali na madaraka na hatimaye, kumezwa na malimwengu badala ya kuambata maisha ya uzima wa milele. Hii ni aibu ya usaliti unaopata chimbuko lake kutoka katika moyo wa binadamu na kushuhudiwa kwa ukali wa ulimi kama upanga unaomshutumu na kumkejeli Kristo Yesu, ajiokoe mwenyewe, ili watu wapate kumwamini! Inasikitisha sana kuona watu na hata baadhi ya viongozi wa Kanisa wakipenda kujikweza, kiasi cha kudhalilisha ule upendo wa kwanza ulioneshwa na Kristo! Ni aibu inayoendelea kujionesha katika ulimwengu wa utandawazi unaotaka kuwarithisha vijana wa kizazi kipya ulimwengu uliomeguka na kusambaratika; dunia inayosheheni makovu ya vita, ghasia na kinzani; uchoyo na ubinafsi ambao unawanyanyasa na kuwatenga watoto wadogo, wagonjwa na wazee. Hii ni aibu kwani watu wamekata mishipa ya aibu na wala hawaoni sababu ya kuwa tena na aibu.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumwomba Mwenyezi Mungu awajalie kupata aibu takatifu itakayowawezesha kutubu na kuongoka kwa kuguswa na ukimya wa Kristo pale Msalabani, kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu. Ni toba ya kweli inayowahakikishia kwamba, Kristo Yesu ndiye pekee anayeweza kuwaponya na kuwaganga kutoka katika ukoma wa chuki na uhamasa, ubinafsi na uchoyo; kiburi, hasira, tamaa na uchu wa mali na madaraka, kwa kuwarejeshea tena utu wao kama watoto wapendwa wa Mungu, ili waweze kufurahia wanaporejea tena nyumbani kwa Baba, katika maisha mapya!

Hii ni toba inayowasaidia waamini kutambua udogo na utupu ili kukimbilia na kuambata mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, kama ilivyokuwa kwa Mfalme Daudi kutoka katika kilindi cha ubaya wa moyo na dhambi, akajipatia nguvu kutoka kwa Mungu. Ni toba iliyomwezesha Petro Mtume, kuangua kilio alipomkana Kristo Yesu mara tatu kwamba, hamfahamu hata kidogo. Baba Mtakatifu anawahimiza waamini, kukimbilia na kuambata toba ya kweli kwa kuguswa na kuu wa huruma ya Mungu inayowasha moto wa Injili ya matumaini inayofumbatwa katika upendo usiokuwa na mipaka! Haya ni matumaini yanayoweza kushida ubaya wa moyo na dhambi, kwa njia ya msamaha unaoshinda tabia ya chuki na uhasama, ili kuweza kuwakumbatia jirani kama kielelezo cha umoja, upendo na udugu na hivyo kufukuzia mbali giza la uhasama na woga usiokuwa na mashiko!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, hii ni Injili ya matumaini inayoendelea kutoa harufu ya upendo wa Mungu na faraja kwa nyoyo za vijana wengi wanaoendelea kujisadaka na kujiwekwa wakfu kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo na mshikamano katika ulimwengu ambao umegubikwa na blanketi na kutaka kupata faida kubwa na mapato yasiyotolewa jasho! Hii ni Injili ya upendo inayotekelezwa na watawa na wamisionari wanaojisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini, watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii na watu wasiojulikana; kati ya watu wanaonyonywa na kunyanyaswa utu na heshima yao; watu wenye njaa na wafungwa.

Hii ni Injili ya matumaini kwa Kanisa Takatifu ambalo linaundwa na waamini watakatifu na wadhambi, licha ya mashambulizi mazito kutoka kila pembe, lakini bado linaendelea kuwa ni mwanga unaoangaza, unaotia shime sanjari na kushuhudia upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka kwa binadamu wote; kielelezo cha upendo kwa jirani, safina ya wokovu, chemchemi ya ukweli na uhakika wa mambo. Hii ni Injili ya matumaini yanayobubujika kutoka katika Fumbo la Msalaba lililogeuza chuki na hofu ya walimu wa Sheria na wanafiki kuwa ni chemchemi ya Fumbo la Ufufuko linalogeuza uvuli wa mauti na giza la dhambi kuwa ni mwanga angavu wa Jumapili isiyokuwa na ukomo, kwa kuwafundisha kwamba, upendo wa Kristo ni kiini chao cha Injili ya matumaini! Hii ndiyo neema ya Injili ya matumaini matakatifu.

Baba Mtakatifu anamwomba Kristo Yesu awasaidie kuvua majivuno ya yule mhalifu aliyesulubiwa pamoja na Kristo, ili hatimaye, waweze kuondokana na ufinyu wa mawazo, rushwa na ufisadi kwa kutumia fursa inayopatikana ili kukejeli, kuhukumu na kushutumu na hatimaye, kuwatwika watu wengine, hata Mwenyezi Mungu akiwemo mzigo wa dhambi binafsi.  Waamini wamwombe, Kristo Yesu, kuwajalia kuweza kumwangalia kwa uso wa aibu kama ilivyokuwa kwa yule mhalifu mwingine; uso wa aibu, toba na matumaini ambao umebahatika kuona katika udhaifu wake wa kibinadamu pale Msalabani ushindi wa Mungu, akapiga magoti mbele ya huruma ya Mungu na kwa uaminifu mkuu akabahatika “kupora” paradiso!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.