2018-03-30 16:50:00

Tafakari ya Njia ya Msalaba Kuzunguka Magofu ya Colosseo, 2018


Tafakari ya Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo yaliyoko mjini Roma, Ijumaa kuu, Kanisa linapofanya kumbukumbu ya mateso na kifo cha Kristo Yesu Msalabani, kwa mwaka 2018: ni mwaliko kutoka kwa vijana kwa Mababa wa Kanisa kusikiliza kwa makini kilio chao cha imani na mang’amuzi ya miito, na kukijibu kwa kuwaongoza na kuwasindikiza katika maisha yao, kwani, wanataka kumfuasa Kristo Yesu kama Bwana na Mwalimu, lakini bado wanayo hofu na machungu makubwa mioyoni mwao. Wanataka kuonja huruma na upendo wa Mungu ambao kimsingi ni chemchemi ya amani, huruma, msamaha na utu wema unaofumbatwa katika Fumbo la Msalaba!

Baba Mtakatifu Francisko amewadhaminishwa vijana wa kizazi kipya kuandika tafakari ya Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo kwa Mwaka 2018. Vijana wanatafakari maana ya haki, kashfa ya Fumbo la Msalaba katika maisha ya mwanadamu; umuhimu wa kuwa na mambo rejea katika maisha ya vijana; changamoto ya majadiliano katika ukweli na uwazi pamoja na mapambano ya maisha yanayowakabili vijana katika ulimwengu wa utandawazi, maendeleo na sayansi. Tafakari ya vijana hawa imeratibiwa na kuhaririwa na Professa Andrea Monda kadiri ya taarifa iliyotolewa na Dr. Greg Burke, Msemaji mkuu wa Vatican.

Hizi zote ni jitihada za Mama Kanisa kutaka kuwasikiliza vijana wa kizazi kipya kama sehemu ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana itakayotimua vumbi mwezi Oktoba, 2018, lakini utangulizi wake kufanyika kuanzia tarehe 19 Machi 2018 na kuhitimishwa, Jumapili ya Matawi, Kanisa lilipokuwa linaadhimisha Siku ya Vijana Duniani na kwa Mwaka huu katika ngazi ya Kijimbo. Baba Mtakatifu Francisko anawataka vijana kutafakari Fumbo la Pasaka: yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu katika maisha yao ya kila siku.

Vijana katika tafakari hii, wanamwona Kristo Yesu kama mashuhuda hai waliokuwepo mjini Yerusalemu, takribani miaka 2000 iliyopita, wakifuata nyayo za Yesu hatua kwa hatua katika Njia ya Msalaba, kila mmoja wao kadiri ya hali, mazingira na umri wake; kielelezo cha watu waliomtuhumu na hatimaye, kumhukumu Kristo Yesu kuteswa na hatimaye, kufa kifo cha aibu Msalabani. Yesu anakubali kupokea Msalaba kwa hiyari na kuubeba kuelekea Mlimani Kalvari! Vijana wanajiuliza ni mara ngapi wamekuwa wagumu na wakaidi wanapopewa dhamana au wajibu wa kutekeleza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi?

Lakini, Yesu anaubeba Msalaba huu mzito hadi Mlimani Kalvari ambako anateswa, anadhihakiwa, ana nyanyaswa na kukataliwa na watu! Yesu akiwa kwenye Njia ya Msalaba anaanguka mara tatu, hali hii iwasaidie vijana kutambua kwamba, wana nafasi na uwezo wa kuamka tena na kuendelea na safari pale imani inapoingia mchanga au matumaini yao yanapotoweka kama ndoto ya mchana! Yesu anapokutana na Simoni wa Kirene anayemsaidia kubeba Msalaba, hapa vijana wanasema, hii ni fursa ya kukutana na huruma na upendo wa Mungu, kwa kujitambulisha na jirani zao, ingawa wanaonekana kuwa ni watu tofauti kabisa pengine kutokana na rangi, tamaduni au mahali wanapotoka!

Vijana wanafanya tafakari ya kina kutoka katika undani wa maisha yao, kielelezo kwamba, wanao uwezo wa kuchunguza dhamiri zao, kujadiliana na hatimaye, kuzungumzana na Kristo Yesu katika maisha ya sala yanayofumbatwa katika unyenyekevu wa moyo unaoweza kuwasaidia vijana wa kizazi kipya kugundua siri kuu ya upendo wa Kristo Yesu unaofumbatwa katika Fumbo la Msalaba. Vijana wanataka kujenga na kudumisha utamaduni na sanaa ya kusikiliza kwa makini kama vile Kristo Yesu alivyowasikiliza wanawake wa Yerusalemu na kuwatuliza katika mahangaiko yao. Kwa bahati mbaya, vijana wa kizazi kipya ni watu ambao wanaishi katika unafiki na ulaghai, hawataki kuuangalia ukweli kwa macho makavu!

Vijana wajifunze kutoka kwa Yesu kuzungumza ukweli, kukoselewa pale wanapokosea bila ya kuhukumu! Vijana wanasema, majadiliano yanayofumbatwa katika ukweli na uwazi yanagusa undani wa mtu, yanawainua wanyonge kama ilivyokuwa kwa wanawake wakati wa Yesu. Hii ni changamoto kwa vijana kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Vijana wanayaona mateso, mahangaiko na hata kifo cha Kristo Yesu kati ya wakimbizi na wahamiaji; waathirika wa nyanyaso za kijinsia na utumwa mamboleo pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi: Hawa ndio wale ambao wanavuliwa bila aibu utu na heshima yao kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu. Vijana wawe na jicho la huruma na mapendo kwa wale wote wanaoteseka sehemu mbali mbali za dunia. Vijana wanashangazwa na ukuu na utakatifu wa ubinadamu wa Kristo unaodhalilishwa pale Msalabani. Utu na heshima ya binadamu wote vinapaswa kulindwa na kuendelezwa!

Vijana wa kizazi kipya wanaoogelea katika maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano, wanamwangalia Kristo Yesu na jinsi anavyoweza kuwasaidia kukabiliana na changamoto za maisha yao ya kila siku! Hawa ni vijana wanaolemewa na Msalaba wa maisha; ni watu ambao si rahisi sana kuaminiwa bali ni watu wanaoshutumiwa na kuhukumiwa kutokana na maneno na matendo yao yanayosigana sana na yale ya “vijana wa zamani”. Mbele ya: mateso na kifo cha aibu, Yesu hakukata tamaa, bali alijiaminisha mbele ya Baba yake wa mbinguni, kiasi hata cha kudiriki kukamilisha kazi ya ukombozi kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake.

Leo hii vijana wanajiaminisha zaidi kwa habari zinazovurumishwa kwenye mitandao ya kijamii! Maneno ya Kristo Yesu ni chemchemi ya furaha, upendo, msamaha na upatanisho wa kweli. Lakini vijana wanataka kulipiza kisasi pale wanaotendewa ubaya; ni watu ambao macho yako “kodo” kwenye luninga na simu za viganjani. Vijana wanaalikwa kumkimbilia Kristo katika utupu wao, ili aweze kuwafundisha mambo msingi ya maisha! Mateso na Kifo cha Yesu pale Msalabani kinawaachia vijana maswali ambayo majibu yake yanapatikana kwenye Fumbo la Msalaba! Mara nyingi ni watu wanaotaka kukimbia magonjwa, mateso na hata kifo kwa kutafuta njia za mkato katika maisha! Lakini, Yesu amediriki kukabiliana na Fumbo la Mateso na Kifo chake hadi dakika ya mwisho ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Yesu anajisadaka kweli kweli na hapa si rahisi sana kuwafafanulia vijana maana ya Fumbo la Kifo, kwani wao kifo wanadhani kiko mbali sana na maisha yao! Vijana wanahamasishwa kuangalia Msalaba ili kugundua: huruma, upendo na msamaha wa Mungu katika maisha yao! Vijana wanapaswa kumtafuta Kristo Yesu kutoka katika undani wa moyo na maisha yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.