2018-03-30 16:18:00

Papa Francisko asema, kuna fursa tele za kutubu na kumwongokea Mungu


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi jioni, tarehe 29 Machi 2018 akiwa kwenye Gereza kuu la “Regina Coeli” mjini Roma, ameadhimisha Ibada ya Karamu ya Mwisho, Mama Kanisa alipokuwa anafanya kumbu kumbu ya kuanzishwa kwa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Daraja Takatifu na Amri ya upendo inayomwilishwa katika huduma ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Baba Mtakatifu amewaosha miguu wafungwa kumi na wawili kutoka katika nchi saba na wafungwa kutoka Afrika ni wale wanaotoka Morocco, Nigeria na Sierra Leone.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake akawakumbusha kwamba, wakati wa Yesu kazi ya kuwaosha watu miguu ilikuwa ikifanywa na watumwa, lakini hii ilikuwa ni kazi ambayo Yesu ameitekeleza mwenyewe kama ushuhuda wa huduma ya upendo miongoni wa watu wa Mungu na kwamba, uongozi katika Kanisa unafumbatwa katika huduma makini na wala si ufahari wa maisha kama walivyodhani akina Yakobo na Yohane, wana wa Mzee Zebedayo, waliomwomba Yesu nafasi za upendeleo katika utawala wake. Yesu kwa jicho la upendo na huruma na kuwakumbusha kwamba, wakuu wa mataifa huwatala watu wao kwa nguvu na wakubwa wao kuwatumikisha, bali kwenu ninyi mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi wenu, na mtu anayetaka kuwa wa kwanza wenu, atakuwa mtumwa wa wote. Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, kwa mwelekeo huu mpya wa uongozi ndani ya jamii, Kristo Yesu alileta mapinduzi makubwa katika mawazo na fikra za watu, kumbe, hata leo hii, kiongozi anapaswa kuwa ni mtu wa huduma.

Binadamu katika safari ya maisha yake, anao uwezo wa kutubu na kumwongokea Mungu na hivyo, kushiriki kuandika historia inayofumbatwa katika haki, upendo, msamaha katika huduma, badala ya mwelekeo wa sasa wa viongozi wengi kuonesha ubabe, dhuluma, mauaji, vita na kinzani. Viongozi wengi wamegubikwa na kiburi, jeuri na tabia ya kutaka kulipiza kisasi. Kristo Yesu anakazia huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, wafungwa kumi na wawili kutoka Gereza la “Regina Coeli” ni mfano wa Mitume kumi na wawili waliooshwa miguu na Yesu mwenyewe, Siku ile ya Alhamisi Kuu.

Yesu alisadaka maisha yake, akainamisha kichwa kilichokuwa kimevikwa taji la miiba! Yesu alithubutu kuhatarisha maisha yake, ili kuwatafuta kondoo waliokuwa wamepotea na hatimaye, akapenda kuwaachia waja wake kumbu kumbu ya sadaka na upendo wake usiokuwa na kifani katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Baba Mtakatifu wakati wa kutakiana amani, amewataka wafungwa kuonesha moyo wa upendo kwa watu wote, wanaowapenda na kuwaombea mema, bila kuwasahau hata wale wanaowachukia na kuwatakia mabaya katika maisha; watu ambao pengine hata wakiwaona wangethubutu kuwalipizia kisasi, wote hawa wajaliwe kupata amani inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake!

Mwishoni wa Ibada, Baba Mtakatifu Francisko amesema kwamba, katika maisha na uzee, kuna magonjwa yanayowaandama kiasi hata cha kushindwa kuona vyema! Kumbe, mwakani, 2019 anatarajiwa kufanyiwa operesheni ya jicho ili kuondoa “mtoto wa jicho” anayeweza kusababisha upofu! Hii ni changamoto inayoapaswa kufanyiwa kazi katika maisha ya kiroho, eneo la kazi kutokana na mchoko, makosa na udhaifu wa mwanadamu, hali ya kukata na kukatishwa tamaa, mwanadamu anakabiliwa na utando katika maisha na hatimaye, kukosa mwelekeo. Maandalizi ya Pasaka iwe ni fursa mpya ya “kusafisha macho” ili kuwa na macho ya matumaini kwa Kristo Mfufuka. Mwishoni kabisa, Baba Mtakatifu amewataka wafungwa kutokata tamaa ya kupyaisha mtazamo wao wa maisha, kwa kufanya operesheni ya maisha ya kiroho ili kuondoa ukungu wa maisha, kwa hakika, hii ni changamoto endelevu katika maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.