Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Maisha Ya Kanisa Afrika

Askofu mkuu Ruwaichi: Alhamisi Kuu: Shukrani, uaminifu na miito!

Askofu mkuu Ruwaichi: Alhamisi kuu ni Siku ya: shukrani kwa zawadi ya wito wa kipadre; ni muda wa kuchunguza dhamiri kuhusu ahadi za kipadre katika ukweli na unyenyekevu; ni siku ya kuombea, kukuza na kudumisha miito! - AP

29/03/2018 13:55

Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya sadaka: Shukrani, Kumbu kumbu na Uwepo na upendo endelevu wa Kristo kati pamoja na watu wake. Ni Sakramenti ya uchaji na kielelezo cha umoja na kifungo cha upendo. Mababa wa Kanisa wanasema, Sakramenti ya Daraja Takatifu ambayo kwayo utume uliokabidhiwa na Kristo Yesu kwa mitume wake huendelea kutekelezwa katika Kanisa hadi mwisho wa nyakati; hivyo hiyo ni Sakramenti ya huduma ya kitume kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu ndiye chemchemi ya huduma ndani ya Kanisa, kwani amelianzisha, akalipatia mamlaka, utume, mwelekeo na lengo msingi, yaani wokovu na maisha ya uzima wa milele! Huduma ya Sakramenti ya Daraja Takatifu ndani ya Kanisa ni utumishi ambao ulishuhidiwa na Kristo Yesu mwenyewe kwa kuwaosha miguu mitume wake, huduma inayopaswa kumwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa!

Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo Kuu ya Mwanza, Tanzania katika mahojiano maalum na Vatican News, Mama Kanisa anapoadhimisha Alhamisi Kuu, anawataka Mapadre kufanya kumbu kumbu ya kuwekwa kwa Sakramenti ya Ekaristi, Daraja Takatifu na Huduma ya upendo kwa moyo wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu. Amewajalia kwanza kabisa zawadi ya wokovu, akawakirimia wito, maisha na utume wa Kipadre bila hata masitahili yao, bali wamestahilishwa na Kristo Yesu mwenyewe, Kuhani mkuu. Mapadre wanapaswa kuishi maisha na wito wao kwa moyo wa shukrani, ukarimu na furaha.

Askofu mkuu Ruwaichi aanatambua fika matatizo na changamoto katika maisha na utume wa Kipadre, lakini anawataka Mapadre kutambua kwa dhati kabisa neema kuu waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu na kwa furaha kuu inayobubujika kutoka katika kina cha moyo wao, wathubutu kumshukuru na kumtukuza Mwenyezi Mungu, huku wakijiuliza swali la msingi na Mzaburi kwa kusema, “Nimrudishie Bwana mimi kwa ukarimu na wema wote alionitendea katika maisha?”

Askofu Mkuu Ruwaichi anaendelea kudadavua kwa kusema kwamba, Alhamisi Kuu iwe ni fursa kwa Mapadre kurudia tena ahadi zao za kipadre kwa moyo wa unyofu na ukweli, wakikumbuka ahadi zao walizotoa mbele ya Kristo na mbele ya Kristo Yesu na Kanisa lake! Iwe ni fursa ya kutambuana na kuthaminiana kama Mapadre katika urika wao. Mapadre wapendane na kusaidiana kwa hali na mali; wapokeane katika utajiri na mapungufu katika maisha yao, tayari kutubu na kumwongokea Mungu, ili kuanza upya safari ya kuelekea katika utakatifu wa maisha. Mapadre katika hija ya maisha na utume wao, wajengane na kuimarishana katika yote yaliyo mema, ya kweli na matakatifu. Askofu mkuu Ruwaichi katika mahojiano haya na Vatican News anakaza kusema, mavuno ni mengi, lakini watenda kazi katika shamba la Bwana ni wachache. Basi, Mapadre na familia ya Mungu katika ujumla wake, iwe mstari wa mbele kuombea baraka na neema ya wito wa upadre, lakini kila padre anapaswa kujitosa bila ya kujibakiza ili kuwa mlezi mzuri wa miito!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

29/03/2018 13:55