2018-03-28 08:07:00

Mchango wa Ijumaa Kuu kwa Nchi Takatifu ni ushuhuda wa imani


Kipindi cha Kwaresima ni safari ya maisha ya kiroho inayorutibishwa kwa: Sala, tafakari ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na Matendo ya huruma kama kielelezo makini cha imani tendaji. Ni wakati muafaka kwa waamini kutambua udhaifu wao wa kibinadamu na dhambi zinazowaandama, tayari kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, kwa njia ya: toba na wongofu wa ndani. Kristo Yesu aliyekuwa tajiri katika mambo yote, alijinyenyekesha ili waja wake, waweze kuwa matajiri katika Yeye!

Kwaresima ni hija ya upendo na mshikamano, kama ilivyokuwa kwa Msamaria mwema kwa: kuwaganga, kuwaponya na kuwahudumia maskini na wale wote wanaoteseka kwa mafuta ya faraja kutoka kwa Mwenyezi Mungu na divai ya huruma na upendo, ili wale wote waliopondeka moyo waweze kusimama tena na kusonga mbele kwa imani na matumaini. Mchango wa Ijumaa kuu unaotolewa na waamini kutoka katika Makanisa mahalia kwa ajili ya Nchi Takatifu ni kielelezo cha ushuhuda wa imani, umoja na mshikamano na familia ya Mungu katika Nchi Takatifu na huko Mashariki ya Kati, wanakoendelea kuteseka, kunyanyasika na kudhulumiwa.

Hawa ni watu ambao utu na heshima yao vimewekwa rehani; wamevunjika moyo, kiasi kwamba, upendo na mshikamano wa dhati kutoka kwa wakristo sehemu mbali mbali za dunia, unakuwa ni chemchemi ya matumaini mapya katika safari yao! Hii ni sehemu ya ujumbe ulioandikwa na Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki, kwa ajili ya kuwahamasisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuchangia kwa hali na mali ili kusaidia maisha na utume wa Kanisa huko katika Nchi Takatifu na Mashariki ya kati, kama sehemu ya utekelezaji wa kilio cha Kristo Yesu aliyejinyenyekesha, akateswa na hata kufa kifo cha aibu pale Msalabani. Kilio cha Wakristo katika Nchi Takatifu na Mashariki ya Kati, bado kinaendelea kusikika kila kukicha, lakini kwa bahati mbaya, hakuna wa kuwasikiliza.

Hii ni changamoto kwa Wakristo kuendelea kuhifadhi kumbu kumbu ya Fumbo la Umwilisho, Mateso na Kifo cha Kristo Yesu kama kielelezo cha ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na kifo! Kumbe, Mchango wa Ijumaa kuu unaotolewa na waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ni alama ya upendo na mshikamano, ili kusaidia mchakato wa kugharimia maisha na utume wa Kanisa katika sera na mikakati yake ya shughuli za kichungaji katika maeneo haya. Makanisa mengi huko Yerusalemu yanaendelea kuboreshwa, alama hai ya majadiliano ya kidini na kiekumene, daima kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini.

Lengo ni kuendelea kuwekeza katika sekta ya elimu, afya pamoja na ustawi wa jamii, kama daraja ya kuwakutanisha waamini wa dini mbali mbali, ili kwa pamoja waweze kujenga matumaini kwa siku za usoni kwa kuheshimiana na kushirikiana katika utekelezaji wa huduma mbali mbali. Itakumbukwa kwamba, wananchi wengi kutoka Mashariki ya Kati, wamelazimika kuyakimbia makazi yao ili kutafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi hasa nchini Yordani na Lebanon, wanakohudumiwa na Makanisa mahalia. Huduma ya upendo kwa maskini na wahitaji ni sehemu muhimu sana ya utambulisho wa Wakristo anasema Baba Mtakatifu Francisko.

Katika ujumbe wake wa Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2018 anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuonesha moyo wa huruma na mapendo watu wanaokimbia vita na baa la njaa; watu wanaoteswa na kunyanyaswa; watu wanaokabiliwa na umaskini wa hali na kipato, bila kuwasahau waathirika wa mabadiliko ya tabianchi yanayoendea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Kuna matumaini ya wananchi wa Siria na Iraq kuanza kurejea tena katika makazi yao ya zamani, ambayo kwa sasa yamebaki kuwa magofu kutokana na vita ambayo imedumu kwa muda wa miaka saba sasa. Hakuna tena shule, hospitali wala Makanisa kwa ajili ya huduma endelevu ya binadamu. Hawa ndiyo watu wanaotumaini ushuhuda wa mshikamano wa huruma na upendo unaooneshwa kwa njia ya Mchango wa Ijumaa Kuu kwa mwaka 2018.

Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki, linawaalika na kuwahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kufanya hija kwenye Nchi Takatifu, ili kuunga mkono pamoja na kuzitegemeza familia ambazo zimebaki katika maeneo matakatifu. Kipindi cha Kwaresima kinachowaandaa waamini kuadhimisha Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, iwe ni nafasi ya kushinda chuki kwa njia ya upendo; machungu moyoni kwa njia ya furaha pamoja na kuendelea kusali ili kuombea amani ya kudumu inayopata chimbuko lake kutoka katika undani wa moyo wa mwanadamu, hasa kwa wananchi wanaoishi katika Nchi Takatifu na huko Mashariki ya Kati. Mwishoni, Kardinali Sandri anasema, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwashukuru kuanzia sasa, wale wote watakaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mchango wa Ijumaa Kuu utakaopelekwa kusaidia mchakato wa maisha na utume wa Kanisa huko Nchi Takatifu na Mashariki ya Kati.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.