2018-03-28 08:54:00

Familia ya Mungu Nchi Takatifu inashukuru kwa ukarimu na mshikamano


Mama Kanisa amelikabidhi Shirika la Ndugu Wadogo wa Mtakatifu Francisko dhamana ya: kulinda, kutunza na kuendeleza maeneo matakatifu yaliyoko kwenye Nchi Takatifu na huko Mashariki ya Kati katika ujumla wake. Shirika hili limekuwa ni chombo cha huduma ya maendeleo endelevu: kiroho na kimwili katika maeneo haya. Mchango wa Ijumaa Kuu kwa mwaka 2017 uliotolewa kwa Shirika hili na Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki umetumika kwa ajili ya maboresho ya Mji wa Yerusalemu kama kivutio cha mahujaji katika maeneo matakatifu. Fedha imetumika kwa ajili ya huduma kwa familia ya Mungu katika Makanisa mahalia kwa kusaidia hasa vijana wa kizazi kipya, kuendelea na masomo ya sekondari, vyuo na vyuo vikuu.

Mchango wa Ijumaa kuu, umekuwa ni msaada mkubwa na kielelezo cha upendo na mshikamano katika maboresho ya masuala ya kitamaduni; maendeleo endelevu ya binadamu na kama sehemu ya majadiliano ya kidini yanayofumbatwa katika huduma makini inayopania kujenga na kudumisha haki, amani, upendo na maridhiano kati ya watu! Itakumbukwa kwamba, Lebanon na Yordani zilielemewa sana na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kutoka Siria, kumbe, fedha hii imesaidia kuonesha upendo na mshikamano wa Kanisa.

Taarifa ya Mhudumu Mkuu wa Nchi Takatifu kwa mwaka 2017 inaonesha kwamba, kumekuwepo na maboresha makubwa katika maeneo yanayopokea mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wanaotembelea Yerusalemu hasa zaidi. Kwenye Kaburi Takatifu, Bustani ya Mizeituni, Njia ya Msalaba, Konventi na Jumba la Makumbusho ya Nchi Takatifu, yameboreshwa kwa kiwango cha hali ya juu kabisa. Ni maeneo ambayo yanaweza kutumiwa na wasomi, wanaotaka kujiendeleza zaidi katika Sayansi ya Biblia na Mambo ya Kale.

Ain Karem, mahali alipozaliwa Yohane Mbatizaji pameboreshwa sana, bila kusahau Kanisa kuu la Bethlehemu, mahali alipozaliwa Kristo Yesu, Mkombozi wa dunia. Madhabahu ya Wafuasi wa Emau, waliomtambua Kristo Yesu alipokuwa anawafafanulia Neno la Kuumega Mkate, yameboreshwa pia, ili yaweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi na kivutio kwa mahujaji kuendeleza hija ya maisha yao kwa imani na matumaini katika tafakari na maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Maeneo mengine yaliyoboreshwa ni pamoja na mji wa Nazareth, Mlima Tabor, mahali amapo Kristo Yesu, aligeuka Sura, kielelezo cha utimilifu wa Agano la Kale, Unabii na Sheria.

Mchango wa Ijumaa Kuu umekuwa ni kielelezo cha mshikamano wa Kanisa la Kiulimwengu na Makanisa mahalia katika huduma ya elimu kwa vijana wa kizazi kipya kwa kuzingatia kwamba, Kanisa linataka kuwajengea vijana uwezo wa kielimu ili kukabiliana vyema na mazingira yao. Shule za msingi na sekondari zimeboreshwa pamoja na ujenzi wa Hosteli kwa ajili ya wanafunzi na makazi kwa ajili ya familia maskini. Maboresho ya vyombo vya mawasiliano ya jamii yamezingatiwa pia, kama sehemu ya mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu yanayofumbatwa katika ukweli na ujenzi wa amani, upendo na maridhiano kati ya watu. Huduma kwa wakimbizi na wahamiaji, mishahara ya wafanyakazi na wahudumu mbali mbali ni kati ya mambo ambayo yamefanyiwa kazi katika kipindi cha mwaka 2017. Familia ya Mungu kutoka Nchi Takatifu na Eneo la Mashariki ya Kati, inawashuruku Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema, wanaoendelea kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi katika Nchi Takatifu na huko Mashariki ya Kati.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.