2018-03-27 13:56:00

TEC: Kwaresima 2018: Jubilei ya Miaka 150, Maendeleo & Haki msingi!


Kwa mwaka huu wa 2018 kipindi hiki, cha kujitafakari mbele ya Mungu na kufanya toba hususan uhai wa imani yetu kwa njia ya matendo ya huruma, haki, upendo na amani kwa jirani zetu, ni kipindi chenye upekee wa aina yake kwa sababu kuu tatu: 1) Ni katika mwaka huu ambapo Kanisa Katoliki Tanzania  linaadhimisha na kusherehekea miaka 150 ya Ukatoliki Tanzania Bara, na kilele chake kitakuwa tarehe 7 Oktoba; 2) Mwaka huu pia utakuwa ni mwaka wa 50 tangu Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania watoe tamko rasmi kuhusu mwelekeo na hatima ya nchi yetu; na 3) Mwaka huu ni mwaka wa maandalizi ya utekelezaji wa haki ya msingi ya kidemokrasia ya raia wote ya kuchagua viongozi wa serikali zetu za mitaa, vijiji na vitongoji  hapo mwakani 2019.

Kwa sababu kuu hizo tatu, ni vema tafakari yetu ya Kwaresima ikalenga katika swali ambalo, kwa namna moja au nyingine, linahusu sababu hizo tatu. Kwa njia ya swali hilo mwanadamu hudiriki kumhoji na kumuuliza Mungu na Muumba wake kuhusu hali ya binadamu mwenzake. Swali hilo ni “Je, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?” (Mw. 4:9).  Hali halisi ya nchi yetu, kwa yeyote anayesoma ishara za nyakati kwa makini, inalifanya swali hilo liwe na uzito wake kuendana na sababu hizo kuu tatu zilizotolewa. Lakini pia, tukumbuke kuwa mwaka 2018 ni mwaka wa sabini (70) tangu Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa walipotamka rasmi na kujifunga kuhakikisha kuwa Tamko la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu la mwaka 1948 linatekelezwa. Na sasa tuone ni kwa namna gani swali hilo linatuhusu kwa kuangalia misingi ya sababu hizo kuu tatu.

HITIMISHO: Tukiwa tunaaadhimisha miaka 150 ya umisionari na uinjilishaji nchini Tanzania, tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa upendo wake usiokuwa na mpaka, si tu kwa kumtoa Mwanae wa pekee awe Mkombozi wetu, lakini pia kwa Mwanae mpendwa kuwa sababu ya kumfahamu Mungu. Hivyo basi, tunapofanya adhimisho hili kubwa la Kristo kati yetu, ni fursa ya kumrudia Mungu kwa moyo wa shukrani.  Sisi tulioujua upendo wa Kristo, sisi tunaoonja katika maisha yetu nguvu na uzuri wa imani ya Kikristo hatuna budi kumshukuru Mungu.  “Nimrudishie Bwana nini kwa Ukarimu wake wote.  Nitakipokea kikombe cha wokovu na kulitangaza jina la Bwana” (Zab 116:12). Shukrani ya kweli inadhihirika katika kuwa tayari wa kukipokea kikombe cha wokovu na kulitangaza jina la Bwana.  Kwa maneno mengine, huu ni mwaliko wa kuwa “katika hali ya umisionari daima” (EG, 25), unaopingana kabisa na swali alilodiriki Kaini kumuuliza Mungu, ‘Mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?’ Tofauti kabisa na swali hilo la Kaini, ushuhuda wa imani unadai ujasiri na unabii, kama walivyo wale wamisionari waliotuletea imani. Pale tulipolegelega tunapaswa “tuvumbue tena upya na kuongeza shauku yetu ile furaha ya kuinjilisha yenye kuburudisha na kufariji, hata pale ambapo tunapaswa kupanda kwa machozi” (EG, 10).

Baada ya miaka 150, uinjilishaji bado upo na unahitajika. Wewe Mkristo, unaitikiaaje? Kwa michango na sadaka zetu zinazofanikisha waseminari kusoma na kuwa mapadri, watawa kupata mahitaji yao, wagonjwa kupewa neno la upendo na faraja, wafungwa kutembelewa, mayatima na wajane kupewa haki zao. Watu kuhudumiwa vizuri katika vituo vya kazi na huduma, hata kuiona sura ya Mungu kupitia sisi, huo ndio uinjilishaji mpya na wa sasa. Katika kipindi hiki cha Kwaresima, ni muhimu kutafakari ni kwa namna gani tunamuishi Kristo, na kwa namna gani tunashindwa kumuishi Kristo na kuomba neema na msamaha wake. Tunahitaji kutambua ya kwamba sisi sote tu wamisionari wa Kristo, kwa wenzetu wapate kumjua kama ambavyo kwa sadaka za watu wengine sisi nasi tulipata kumjua Yesu.

Ni rahisi zaidi kuona kama si kitu sana kuwa Mkristo Mkatoliki kwakuwa tu ndani na tunabahati hiyo. Hatuoni kama bahati tena wala ajabu ya upendo wa Mungu kwetu. Lakini kuna watu wengi sana wanaotamani kumjua Kristo na hawajapata nafasi hiyo, na wengine wanaipata ilihali jua limekwisha kutua. Katika kipindi hiki cha Toba, tukae chini tena na kutafakari kwa upya, ni kwa namna gani maisha yetu yanamuishi Kristo, na tudhamirie kujirudi na kutaka kufanya mapenzi ya Mungu. Hivyo basi, Wapendwa Familia ya Mungu, kwa moyo wa upendo na kuwajali tunawahimiza waamini mfanye toba ya kweli ili Mungu aguse na abadilishe mioyo yetu, ya raia wengine na viongozi wa nchi. Tuichukulie Kwaresima ya mwaka huu (2018) kuwa ni sehemu ya maandalizi ya adhimisho la Jubilee lenye lengo la kujenga upya Kanisa Katoliki Tanzania na lenye wamisionari wengi watakaoweza kutumwa popote ulimwenguni. Na, mwisho tunapenda kuwatia moyo zaidi ili mshiriki zaidi katika katika maswala ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni, na kwa ukristo wenu muwe chumvi na mwanga kwa wote.

 Kristo Mfufuka awape amani!

Barazala Maaskofu Katoliki Tanzania, 2018.








All the contents on this site are copyrighted ©.