Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Maisha Ya Kanisa Afrika

Jubilei ya Miaka 50 ya Waraka wa "Humanae vitae" na changamoto zake!

Waraka wa Kitume wa Mwenyeheri Paulo VI unaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuchapishwa kwake, hapo tarehe 25 Julai 1968. - REUTERS

27/03/2018 12:09

Mwenyeheri Paulo VI anayetarajiwa kutangazwa kuwa Mtakatifu mwaka huu, tarehe 25 Julai 1968 aliandika Waraka wa Kitume “Humanae Vitae” yaani “Maisha ya binadamu”, ambao unakazia pamoja na mambo mengine: dhamana na wajibu wa wanandoa kushiriki katika kazi ya uumbaji. Hii ni dhamana wanayoitekeleza kwa uhuru kamili na uwajibikaji, kwani wanashiriki katika mpango wa Mungu katika kazi ya uumbaji. Dhamana hii ni chemchemi ya furaha na matumaini, lakini wazazi wanakabiliwa na changamoto pevu wanapotekeleza wajibu huu kutokana na kuibuka kwa kasi kubwa dhana ya utamaduni wa kifo dhidi ya Injili ya uhai.

Waraka wa Maisha ya binadamu, mwaka huu unaadhimisha Jubilei ya miaka 50 tangu kuandikwa kwake na kilele chake ni tarehe 25 Julai 2018. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, limefanya maandamano makubwa yaliyowahusisha waamini na watu mbali mbali kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Waraka huu wa Kitume na unaotoa mafundisho tanzu kuhusu: mpango wa Mungu katika maisha ya ndoa na familia; upendo wa dhati kati ya bwana na bibi na dhamana na malezi na makuzi kwa watoto wao. Kauli mbiu ya maandamano haya ilikuwa Familia ni kitovu cha upendo na urithishaji wa maisha.

Maandamano haya yalilenga kupinga: nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo, kazi za suluba, utumwa mamboleo, ndoa za utotoni na mauaji ya watoto ambao pengine wanatolewa kafara. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, linawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwapokea, kuwalinda, kuwatunza na kuwaendeleza watoto kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Watoto wana haki ya kupata malezi bora na makini ili kuwajengea leo na kesho iliyo bora zaidi dhidi ya jamii inayoogelea katika rushwa, ufisadi,  udini na ukabila usiokuwa na mvuto wala mashiko kwa ustawi na maendeleo ya wengi!

Hii ni changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuendelea kujikita katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; kwa kuzingatia mpango wa uzazi kwa njia ya asili. Ili kufanikisha azma hii, wazazi wanapaswa kuwajibika barabara katika maisha ya ndoa na familia; kwa kuishi tunu msingi za Kikristo pamoja na kuhakikisha kwamba, familia zao zinakuwa kweli ni Kanisa dogo la nyumbani, mahali pa sala na utakatifu wa maisha. Vijana wanapaswa kufundwa vyema jinsi ya kuheshimu miili yao kwani ni Mahekalu ya Roho Mtakatifu. Vijana watambue, uzuri, utakatifu na changamoto za maisha ya ndoa na familia, ili waweze kuwa tayari kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.

27/03/2018 12:09