2018-03-26 07:49:00

Papa Francisko: Vijana msipopiga kelele, mawe yatapiga badala yenu!


Baba Mtakatifu Francisko, ameongoza Ibada ya Misa Takatifu, Jumapili ya Matawi, tarehe 24 Machi 2018 sanjari na maadhimisho ya Siku ya XXXIII ya Vijana Duniani kwa ngazi ya kijimbo, ambayo kwa mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu “Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu” Lk. 1:30. Baba Mtakatifu amebariki matawi na baadaye, kuongoza maandamano makubwa ya vijana kutoka ndani na nje ya Roma kuelekea katika maadhimisho ya Misa ya Mateso ya Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Mama Kanisa anakumbuka siku ile Kristo Yesu alipoingia mjini Yerusalemu kwa shangwe kama Mfalme na Masiha na kushangiliwa kama Mwana wa Daudi anayeleta wokovu. Hii ndiyo maana ya wimbo wa Hosana. Ni Mfalme wa utukufu anayeingia Yerusalemu akiwa amepanda mwana punda na kushangiliwa na Watoto wa Wayahudi kama kielelezo cha unyenyekevu wake. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amekazia furaha ya watu walioguswa na maisha na utume wa Kristo Yesu, mateso na mahangaiko ya watu; mafanikio na kushindwa katika maisha, ili waamini waweze kujifunza kupenda kwa dhati; kushinda chuki, kujisadaka bila ya kujibakiza; kuwajibika kikamilifu pasi na kukwepa wajibu na dhamana kwa kunawa mikono sanjari na kuendelea kubaki waaminifu hata pale, mtu anaponekana kutengwa na kusalitiwa! Simulizi la mateso ya Kristo Yesu linaonesha furaha inayobubujika kutoka kwa Yesu, lakini kwa watu wengine, hili ni chimbuko la chuki na hasira!

Yesu aliingia mjini Yerusalemu huku akiwa anashangiliwa kwa nyimbo na vigelegele. Baba Mtakatifu anasema, pengine hii ni furaha ya wale walioguswa na utume na maisha ya Yesu, wakaonja huruma, upendo na msamaha wa Mungu katika maisha yao kama ilivyokuwa kwa Mwana mpotevu aliyesamehewa dhambi zake, mgonjwa wa ukoma aliyeponywa kwa kuguswa na huruma ya Mungu na mfano wa kondoo aliyepotea! Hizi ni kelele za watu waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii, waliohesabiwa kuwa wadhambi na watu wachafu! Hawa ndio waliothubutu kupiga kelele na kushangilia “Mbarikiwa yeye ajaye kwa jina la Bwana”! Haikuwa rahisi kuwanyamazisha watu waliorejeshewa tena utu na heshima yao kama binadamu; watu walioaminiwa na kutangaziwa Injili ya matumaini.

Baba Mtakatifu anaendelea kudadavua furaha hii kwa kusema, iligeuka kwa ni kikwazo na kashfa ya mwaka kwa wale waliokumbatia “Sheria na mapokeo ya ibada”! Ni watu ambao hawakuguswa hata kidogo na umaskini, mateso na mahangaiko ya watu; wakasahau hata kushangilia ufunuo wa huruma ya Mungu. Hii ni kwa sababu, wao walijiaminisha katika nguvu na uwezo wao wa kibinadamu, wakajiona kuwa ni bora zaidi kuliko ya watu wengine, kiasi hata cha kuwabeza, kuwadhihaki na kuwatolea ushuhuda wa uwongo. Ni watu ambao wanataka kuwatumbukiza wenzao katika shida na magumu, kwa kunyamazisha wale wote wanaodhani kwamba, ni wapinzani wao. Ni watu wanaowapaka wenzao “mafuta kwa mgongo wa chupa” kiasi hata cha kumfanya Yesu kuonekana kuwa ni mhalifu wa kutupwa!

Hawa ndio wale waliotaka kulinda nafasi na mafao yao binafsi, kwa kujiona kuwa ni watu wanajitosheleza, watu wenye kiburi na majivuno wanaothubutu hata kupiga kelele: Msulubishe, msulubishe! Hii ndiyo sauti iliyozima furaha ya watu waliokuwa wanamshangilia Kristo Yesu; wakawapoka matumaini na kufifisha ndoto zao, kiasi cha kuzika furaha iliyokuwa inabubujika kutoka nyoyoni mwa watu! Matokeo yake, moyo unasinyaa na upendo unatoweka kama ndoto ya mchana! Jiokoe mwenyewe ni sauti inatotaka kufisha mshikamano, kuzamisha mawazo ya watu na kufunika nyuso za watu kwa “blanketi la uchoyo” ili kufutilia mbali Injili ya upendo!

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na kusikiliza sauti zote hizi zinazokinzana katika undani na maana yake, lakini zaidi sana wasikilize sauti ya Kristo Yesu anayelia kwa ajili ya upendo; kwa vijana na wazee; watakatifu na wadhambi; huu ni upendo kwa watu wa nyakati zote. Kwa njia ya Fumbo la Msalaba, wote wamekombolewa na Kristo na kwamba, hakuna anayeweza kuthubu kuzima furaha ya Injili, kwani kila mtu na kwa nafasi yake anaguswa na Uso wa huruma ya Mungu. Msalaba uwasaidie waamini kuweka bayana: vipaumbele, maamuzi na matendo yao, tayari kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Ni muda muafaka kwa waamini kujiuliza, Je, Kristo Yesu, bado anaendelea kuwa ni sababu na chemchemi ya furaha ya maisha? Au waamini wanakwazika kwa Kristo Yesu kutoa kipaumbele kwa watenda dhambi, maskini na wale waliosahauliwa? Baba Mtakatifu anawauliza vijana wa kizazi kipya, Je, furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu ndani mwao, imekuwa ni sababu ya udhia, chuki na hasira? Hii ni kwa sababu, kijana mwenye furaha ya kweli si rahisi kuweza “kuchakachuliwa!”

Baba Mtakatifu anasema, kilio cha kundi la tatu ni kile kinachotoka kwa baadhi ya Mafarisayo waliokuwa kwenye mkutano wakamwambia “Mwalimu, uwakanye wanafunzi wako.” Naye akawajibu akisema, wakinyamaza hawa, mawe yatapiga kelele! Kishawishi cha kutaka kuwafumba mdomo vijana na hatimaye, kutoonekana daima kimekuwepo, kwa kutowapatia nafasi ya kuuliza maswali na kujadiliana pamoja nao! Kwa njia hii, ndoto za vijana wengi zinazima kama “kibatari” na matokeo yake vijana wanabaki wakiwa wanaelea katika ombwe pasi na furaha ya kweli! Mwishoni mwa mahubiri yake, Baba Mtakatifu anawataka vijana kupiga kelele ili kumshangilia Kristo Yesu kwa kuimba Hosana bila kutumbikia katika kundi la wale waliokuwa wanalalama kwa nguvu zote, Asulubiwe siku ile Ijumaa kuu! Vijana pazeni sauti zenu kabla ya mawe kuanza kupiga kelele, anasema Baba Mtakatifu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.