2018-03-26 11:35:00

Hati ya utangulizi wa Sinodi ya Vijana ni muhtasari wa maisha yao!


Vijana waliokuwa wanashiriki maadhimisho ya awali ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kuanzia tarehe 19-25 Machi 2018, Jumapili ya Matawi, wakati wa maadhimisho ya Siku ya XXXIII ya Vijana Duniani katika ngazi ya Kijimbo, wamewasilisha “Hati ya Utangulizi wa Sinodi” kwa Baba Mtakatifu Francisko. Vijana wametumia nafasi hii kumshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwatia shime kuzungumza, kusikiliza na kushirikisha mawazo yao.

Vijana wanakiri kwamba, kweli wameonja umoja, upendo na mshikamano wa kidugu licha tofauti zao za kidini, kiimani, kitamaduni na kwamba, umekuwa ni mkutano unaolenga ustawi, maendeleo na mafao ya vijana wengi. Vijana wanasema, Hati ya Utangulizi wa Sinodi” si tu ni muhtasari wa mambo msingi waliyojadili, kwa hakika ni muhtasari wa maisha na matamanio halali yanayobubujika kutoka katika undani wa maisha yao. Ni matumaini ya vijana kwamba, Mama Kanisa ataendelea kujenga na kudumisha utamaduni na sanaa ya kuwasikiliza vijana na kwamba, hati hii itakuwa ni mwanga wa majadiliano kwa Mababa wa Sinodi na familia ya Mungu katika ujumla wake katika mchakato mzima wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana. Vijana wamemhakikishia Baba Mtakatifu Francisko na Kanisa katika ujumla wake, kutumainia sala ya vijana!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.