2018-03-24 14:38:00

Papa Francisko: Pandikizeni mbegu ya Injili ya upendo na ukarimu!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 24 Machi 2018 amekutana na kuzungumza na ujumbe wa Jumuiya ya Trentino iliyosindikiwa na Askofu mkuu Lauro Tisi wa Jimbo kuu la Trento, Kaskazini mwa Italia, kama sehemu ya kumbu kumbu ya maadhimisho ya ushirikiano na Serikali ya Vatican kwa kipindi cha miaka ishirini. Wanajumuiya hawa, wamekuwa ni wadau wakuu wa ushirikiano katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, ushuhuda na upendo wa familia ya Mungu kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro kutoka Trento!

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru wanajumuiya ya Trento kwa kusaidia kugharimia na kufadhili miradi mbali mbali inayotekelezwa na Vatican katika ujumla wake, lakini hasa kwa kuwapokea na kuwakarimia mahujaji na wageni wanaotembelea mjini Vatican. Huu ni ushuhuda wa Mapokeo, amana na utajiri wa tunu msingi za maisha ya imani, bidii ya kazi na mshikamano, utambulisho makini wa wananchi wa Trento!

Baba Mtakatifu anawaalika wanajumuiya wa Trento kuendelea kujizatiti zaidi katika kutangaza na kushuhudia utamaduni wa ukarimu na ushuhuda wa maisha yanayosimikwa katika ukweli, uwazi na udugu, kielelezo makini cha utu na heshima ya watoto wa Mungu. Familia za wanajumuiya wa Trento ziendelee kuimarika ili ziweze kuwa kweli ni “Makanisa ya nyumbani” yanayojikita katika: Neno la Mungu, Upendo kwa Kanisa na huduma makini ya Injili ya uhai. Kwa njia hii, familia zitaendelea kuwa kweli ni chemchemi na shule za tunu msingi za maisha ya kiutu na Kikristo kwa vijana wa kizazi kipya. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawataka wanajumuiya hawa kupandikiza mbegu ya Injili ya upendo katika maeneo yao kazi na utume! Amewatakia maandalizi mema ya maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, wakati huu, Mama Kanisa anapoanza Juma kuu. Amewaweka wanajumuiya hawa wote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa, anawaomba hata wao kumsindikiza katika sala na sadaka zao, ili aweze kutekeleza vyema utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro!

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.