2018-03-24 08:47:00

Je, wewe unachukua nafasi na dhamana gani katika Mateso ya Yesu?


Ndugu msomaji na msikilizaji wa Vatican News, karibu katika tafakari ya Neno la Mungu katika Dominika ya Matawi. Hii ni dominika inayotuingiza katika Juma Kuu, ambamo Kanisa linaadhimisha kwa ukaribu zaidi na kwa namna ya pekee mafumbo makuu ya wokovu wetu. Adhimisho la leo, dominika ya matawi ni adhimisho la Yesu kuingia katika mji wa Yerusalemu. Njia hii anayoianza leo ndio njia itakayomfikisha kwenye karamu ya mwisho, kwenye mlima wa mizeituni na hatimaye, itamfikisha mikononi mwa watesi ambapo atachukua msalaba wake hadi mlima ule wa kalvari atakapoyakamilisha yote. Leo pia ni siku ya 33 vijana duniani na kwa mwaka huu inaadhimishwa kwa ngazi ya kijimbo kama maandalizi pia kwa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana itakayoadhimishwa mwezi oktoba mwaka huu. Pamoja na vijana wanaowazunguka Maaskofu wao mahalia, tumfuate Yesu katika safari yake hii kwa maadhimisho ya Juma hili kuu ili tufe na hatimaye tufufuke pamoja naye kwa utukufu.

Masomo kwa ufupi: Somo la injili linalosomwa kabla ya maandamano (Mk 11:1-10 au Yoh. 12:12-16) linaeleza namna Yesu alivyoingia Yerusalemu. Aliingia kwa shangwe na watu walimpokea kama mfalme wakimwita “mwana wa Daudi” jina linaloashiria cheo hicho cha ufalme. Kutoka kwake walitegemea ukombozi ndio maana waliimba “hosanna, hosanna” yaani  “utuokoe, utuokoe.  Naye Yesu kutaka kuonesha aina yake ya pekee ya ufalme aliungia mji amepanda punda, badala ya farasi kama walivyofanya wafalme. Tayari hii ilionesha ujio wa unyenyekevu na ujio wa amani. Injili hii inaunganishwa katika liturujia ya leo na historia ya mateso ya Kristo kuonesha wazi kwamba Yesu anaingia Yerusalemu ili ateswe na afe msalabani.

Somo la kwanza (Isa. 50:4-7) ni sehemu ya utenzi kumhusu yule anayetajwa kuwa Mtumishi wa Bwana ambaye pia ni Mtumishi mteswa. Mtumishi huyu anateseka kama sehemu ya utii alionao kwa mapenzi ya Mungu “sikuwa mkaidi” (a. 4); anayapokea mateso na anatambua kuwa katika mateso yake hateseki bure, mapenzi ya Mungu yana lengo lake. Somo la pili (Fil. 2:6-11) ni sehemu ambayo pia tunaweza kuuiita utenzi kumhusu Kristo. Utenzi huu unamuelezea Kristo kama mtumishi aliyejishusha, akajinyenyekeza hadi akatolea maisha yake yote kwa ajili ya wengine. Kwa kufanya hivyo, alitukuzwa na akapewa hadhi iliyo ya juu mno.

Tafakari: Tunaweza kujiuliza, Yesu aliingia miji na vijiji vingi wakati wa utume wake, kwa nini kuingia kwake Yerusalemu tunakuadhimisha kwa adhimisho kubwa namna hii? Upekee wake ni kwa sababu ya kile kilichotendeka Yerusalemu. Ni katika mji huo ambapo Yesu amedhihirisha kiini cha ujio wake ulimwenguni. Yesu alishuka duniani ili kumkomboa mwanadamu katika enzi ya mauti, kumpatanisha na muumba wake na kumrejeshea hadhi ya mwana wa Mungu. ukamilifu wa haya yote umetekelezwa pale msalabani aliposema “yametimia” alipokipokea kifo kwa kumwaga damu yake. Kumbe Yesu anapoingia Yerusalemu anaingia kukamilisha kile kilichomleta hapa duniani. Waraka wa Mtume Paulo kwa Wafilipi katika sehemu tuliyoisoma kwenye somo la pili unaunganisha pamoja mwanzo wa Yesu kuja ulimwenguni  katika Fumbo la Umwilisho na mwisho wa utume wake ulimwenguni unaojionesha dhahiri katika Fumbo la Pasaka: kutukuzwa  huku ndiko kutukuzwa katika namna inayotufanya tuelewe zaidi uhusiano uliopo kati ya mwanzo na mwisho wake.

Mtume Paulo anatuonesha kuwa Yesu ambaye tangu mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu hakuona kitu hicho kuwa ni cha kung’ang’ania, bali kwa utashi wake mwenyewe alijishusha, akajinyenyekeza na akayatolea maisha yake kwa ajili ya ukombozi wa ulimwengu. Tunaona hapa uwiano na Adamu ambaye naye tunaweza kusema kuwa alikuwa yuna namna ya Mungu kwa maana aliumbwa kwa sura na mfano wa Mungu (Mwanzo 1:26). Kwa kukosa unyenyekevu na kwa kutamani “kufumbuliwa macho ili awe sawa na Mungu..” (rej. Mwanzo 3:5) alikula tunda la mti uliokatazwa. Mwanzo huo ambao ulimwingiza mwanadamu katika giza, katika dhambi na katika enzi ya mauti Yesu kwa umwilisho wake tayari anaonesha njia ifaayo ielekezayo katika mwanga, katika neema na katika uzima wa milele, njia ya unyenyekevu na utii kwa Mungu.

Katika safari yake ya kuingia Yerusalemu tunaziona zile sifa za mtumishi wa Bwana kama alivyotabiri nabii Isaya zikijidhihirisha kwake. Kwanza anayakabili mateso. Yesu aliingia Yerusalemu akiwa anafahamu fika ni nini kinachomsubiri huko, alikwisha waambia wanafunzi wake kwamba atauawa na aliwakumbuka manabii waliokuwako kabla yake ambao waliuawa Yerusalemu (rej. Lk 19:41). Pamoja na hayo yote bado aliukabili mji wa Yerusalemu. Anajiaminisha kwa Mungu katika yote anayopitia kwa utii na unyenyenyekevu akijua kwamba mwisho wa yote hayo upo wokovu.

Kristo anapotukuzwa na anapokirimiwa jina lile lipitalo kila jina, jina ambalo nasi tunaitwa kwa ubatizo wakristo, anaanzisha enzi mpya ya watu waliokombolewa. Watu ambao kama katika Adamu wanapewa hadhi ya kimungu lakini wanajifunza kutii na kunyenyekea mbele ya Mungu; watu ambao kama yeye mtumishi wa Bwana wanajifunza kujiaminisha kwa Mungu na kuyakambili yote ambayo Mungu anawapitisha wakiamini kuwa wote wanojiaminisha kwake hawapotei bure.

Turejee tena mwaliko wa kuambatana na Yesu katika juma hili kuu. Tunapoisikiliza historia ya mateso yake tunayakumbuka maneno ya Papa Francisko; ninachukua nafasi gani katika majina mengi yanayotajwa katika historia ya mateso ya Yesu, ninataka kuchukua nafasi gani? Je, ni kati ya wale wanaomshangilia Yesu aingiapo Yerusalemu, niko tayari kuonesha ninavyomfurahia Yesu au ninarudi nyuma? Nipo katika kundi la wafarisayo na waalimu wa sheria wanaokusudia kumwua Yesu? Niko sawa na wao?

Au niko kama Yuda Iskarioti anayejiandaa kumsaliti Yesu kwa vipande 30 vya fedha? Nipo kama wale wafuasi ambapo Yesu anapoteseka wao wamelala usingizi? Nipo kama nani? Nipo kama Pilato ambaye anapoona mambo yanakuwa magumu ananawa mikono, anakimbia wajibu wake wa kutetea haki, naruhusu watu wahukumiwe au nawahukumu mwenyewe? Au niko kama maaskari wanaomtemea mate Yesu na kumchapa kwa viboko yaani ninaona furaha kwa kuwatesa wengine? Niko kama wale kinammama walikuwapo pembeni ya Yesu wakilia na kuteseka naye kimya kimya? Niko kama nani Tuyatafakari haya katika juma hili kuu na Mateso ya Kristo yatutie nguvu na kutuunda upya.

Bikira Maria Mama wa Mateso, atuombee!

Na Padre Wiliam Bahitwa.

VATICAN NEWS








All the contents on this site are copyrighted ©.