Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Vatican \ Hotuba

Vaeni silaha za mwanga ili kudumisha usafi wa moyo na utakatifu!

Kwaresima ni kipindi cha kujivika silaha za mwanga ili kutupilia mbali matendo ya giza, kwa lengo la kudumisha utakatifu wa maisha ya Kikristo.

23/03/2018 11:21

Vaeni silaha za mwanga ili kutupilia mbali matendo ya giza kwa njia ya toba na wongofu wa ndani, ili hatimaye, kukuza na kudumisha utakatifu wa maisha ya Kikristo yanayofumbatwa katika: usafi, uzuri na upendo kwa jirani. Utangazaji na ushuhuda wa Neno la Mungu unafumbatwa katika upyaisho wa maisha kiasi hata cha mwamini kuweza kuyamimisha maisha yake kama ushuhuda kwa Kristo na Kanisa lake. Wakristo wanahamasishwa kuwa na moyo safi kama sehemu muhimu sana ya Mafundisho ya Kristo Yesu. Kwa ufupi, haya ndiyo mawazo makuu yaliyotolewa na Padre Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa nyumba ya Kipapa; Ijumaa, tarehe 23 Machi 2018 katika mahubiri ya Kipindi cha Kwaresima, sehemu ya tano, yaliyohudhuriwa na Baba Mtakatifu Francisko, Sekretarieti kuu ya Vatican pamoja na wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume wanaoishi na kufanya utume wao mjini Roma.

Anasema, usafi wa moyo ni kati ya changamoto alizokabiliana nazo Mtakatifu Agostino, kiasi hata cha kukita maisha yake katika toba na wongofu wa ndani kama njia muafaka ya kukumbatia imani, kwa kuuvua utu wake wa kale, uliokuwa umechakaa kutokana na matendo ya giza! Neno la Mungu ni silaha ya mapambano dhidi ya matendo ya giza yanayouchafua na kuuvunjia mwili heshima yake, kiasi hata cha kutumbukia katika tamaa ya mwili, kwa kufuata akili chafu, uovu, tamaa mbaya pamoja na husuda. Mtume Paulo anasema, silaha za mwanga au tunda Roho Mtakatifu ni upendo, furaha, Amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi. Silaha hizi za mwanga ziwasaidie Wakristo kudumisha usafi wa moyo, kwani kuna uhusiano wa karibu sana kati ya usafi wa moyo, utakatifu na Roho Mtakatifu.

Ikumbukwe kwamba, maisha yanayompendeza Mungu yanafumbatwa katika utakatifu wa mwili na upendo wa kidugu kwa jirani, kwani lengo la Mungu ni utakaso wa mwili. Watu wawe na kiasi katika kula, kuzungumza lakini mkazo zaidi unawekwa katika usafi wa moyo, ili kutoigeuza miili yao kuwa ni sababu ya kutenda dhambi na hivyo kutumbukia katika matendo ya giza! Wakristo wa Kanisa la mwanzo walifundishwa kwamba, mwili si kwa ajili ya zinaa, kwani wao, ni sehemu ya viungo vya mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Kwa njia ya miili yao, waamini wanakuwa ni hekalu la Roho Mtakatifu waliye mpokea kutoka kwa Mungu na sasa anaishi ndani mwao na kwamba, Kristo ndiye Bwana anayepaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika maisha!  Vitendo vya zinaa vinalichafua hekalu la Roho Mtakatifu, ndiyo maana Paulo Mtume anawaalika Wakristo kumtukuza Mungu kwa njia ya miili yao, yaani, kwa njia ya Sakramenti ya Ndoa au kwa usafi wa moyo katika maisha kitawa na kipadre! Kila mtu kadiri ya wito na maisha yake.

Padre Raniero Cantalamessa, anaendelea kufafanua kwamba, kuna uhusiano wa karibu sana kati usafi, uzuri na upendo wa kidugu kwa jirani. Usafi wa moyo unapaswa kushuhudiwa na Wakristo wote, kila mstu kadiri ya wito na nafasi yake katika maisha na utume wa Kanisa kama ushuhuda wa uzuri wa mwili. Kristo Yesu anasema, heri wenye moyo safi, maana hao watamwona Mungu, changamoto ya kuepuka tamaa za mwili; fahari ya macho ambayo ni kuona pamoja na kusema ukweli. Jicho ni mwanga wa mwili unaofumbatwa katika usafi wa moyo, ukweli na uwazi. Zote hizi ni silaha za mwanga katika mapambano ya giza linalotaka kumwandama mwamini.

Fadhila za kikristo ziwawezeshe waamini kumvaa Kristo Yesu, ili kufikiri na kutenda vyema, kwa kuepuka dhambi na nafasi zake, daima wakijitahidi kuenenda kwa adabu na wala si kwa ulafi na ulevi; si kwa ufisadi ba uasherati; si kwa ugomvi na wivu! Usafi wa moyo ujenge na kudumisha upendo wa kidugu; ukuze uwajibikaji na uhuru kwa kusimamia haki msingi za binadamu. Usafi wa moyo ujenge upendo na mshikamano wa dhati dhidi ya vitendo vinavyochafua hekalu la Roho Mtakatifu. Usaidie mchakato wa upyaisho wa maisha unaofumbatwa katika kutangaza na kushuhudia tunu msingi za maisha ya Kikristo! Upendo wa kidugu na utakatifu wa maisha, viwasaidie waamini kuachana na dhambi. Mama Kanisa anapenda kuwakumbusha watoto wake kwamba, dhambi na ubaya wa moyo ni mambo yatakayowaandama siku zote za maisha yao, lakini cha msingi ni kuendelea kujizatiti katika kupambana na dhambi kwa kuvaa silaha za mwanga, ili kutokumezwa na malimwengu, daima wakiwajibika fika kwa mawazo na matendo yao.

Ulimwengu wa utandawazi unataka kuhalalisha kila kitu kwa kisingizio cha uhuru na haki msingi za binadamu hata mambo yale yanayokwenda kinyume cha mpango wa Mungu, kanuni maadili na utu wema. Katika changamoto kama hizi, Padre Raniero Cantalamessa anasema Wakristo wanapaswa kujenga moyo safi kwa kutangaza na kushuhudia uzuri wa maisha ya Kikristo unaofumbatwa katika unyenyekevu sanjari na kujivika silaha za mwanga. Roho Mtakatifu awasaidie waamini kuwa na moyo safi, ili waweze kumwona Mungu. Ili waamini waweze kutangaza na kushuhudia uzuri wa maisha ya Kikristo, kuna haja ya kufanya toba na wongofu wa ndani; kwa kuifia dhambi na kuambata Msalaba na Sheria ya Mungu, daima wakijitahidi kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao pamoja na kuepuka makwazo yanayotokana na ukosefu wa usafi wa moyo! Kwaresima iwe ni nafasi ya toba na wongofu wa ndani; kwa kufunga ili kutoangalia fahari za macho; kwa kufunga na kuratibu vileo na chakula; kwa kuvaa silaha za mwanga, ili kudumisha usafi wa moyo. Wakristo wawe na ujasiri wa kuomba neema ya Mungu, kwani bila neema yake, yote ni ubatili mtupu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

23/03/2018 11:21