2018-03-23 14:37:00

Mchakato wa uinjilishaji mpya India unaojikita katika Neno la Mungu


Askofu mkuu Giovanni Pietro Dal Toso, Katibu Mwambata, Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu na Rais wa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari, katika mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu iliyoandaliwa na Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari huko Bangalore, India, kuanzia tarehe 7- 9 Machi, 2018, amekazia umuhimu wa kusikiliza kwa makini Neno la Mungu, kama sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa utume wa Mama Kanisa ulimwenguni. Anawataka waamini kujenga tabia na utamaduni wa kusikiliza kwa makini, kile ambacho Mwenyezi Mungu anataka Kanisa lifanye kwa wakati huu kama sehemu ya utekelezaji wa mapenzi yake.

Hii inatokana na ukweli kwamba, Kanisa linatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, iliyoipokea kwa kumsikiliza kwanza kabisa Mwenyezi Mungu, ambaye amejifunua kwa njia ya Kristo Yesu, Uso wa huruma na upendo wa Baba wa milele! Kumbe, Kristo ni kielelezo na dira katika mchakato mzima wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Baada ya kusikiliza kwa makini, waamini wanaweza kujiunga na Mtakatifu Toma aliyekuwa anaonesha mashaka makubwa juu ya Ufufuko wa Kristo Yesu hata baada ya kusimliwa na mitume wengine, lakini, baada ya kugusa madonda Matakatifu ya Yesu, akapigwa na mshangao mkubwa kwa kusema, “Bwana wangu na Mungu wangu”, ungamo la imani kutoka katika undani wa maisha ya mtu, baada ya kukutana mubashara na Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Ungamo hili na imani, linaondoa shaka na wasi wasi moyoni, tayari kwa kwa mwamini kutangaza na kushuhudia Fumbo la Pasaka. Kadiri ya Mapokeo ya Kanisa, inasadikiwa kwamba, Mtakatifu Toma, ndiye aliyeinjilisha Bara la Asia na kwa namna ya pekee, nchini India. Huu ni wakati muafaka kwa Kanisa nchini India, kumwilisha Habari Njema ya Wokovu kwa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya Kristo Yesu. Utume wa Kanisa utaweza kuzaa matunda yanayokusudiwa yaani: toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha, ikiwa kama waamini watasikiliza kwa makini Neno la Mungu lililofunuliwa kwao kwa njia ya Kristo Yesu ambaye ni kiini cha Habari Njema ya Wokovu.

Hii ni changamoto kwa mwamini binafsi na Jumuiya ya Wakristo katika ujumla wao, kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Yesu katika maisha yao. Muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo umedadavuliwa kwenye Amri kuu ya Upendo kwa Mungu na jirani. Waamini wajifunze maana halisi ya upendo na sadaka kwa ajili ya Mungu na jirani zao. Ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia una kiu ya upendo wa Mungu unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, ili kuzima kiu ya njaa, umaskini, magonjwa na ukosefu wa haki msingi za binadamu.

Upendo wa Mungu kwa binadamu uwe ni chachu ya ujenzi wa dunia inayosimikwa katika haki, amani, umoja, mshikamano na udugu. Mama Theresa wa Calcutta ni mfano bora wa kuigwa katika mchakato mzima wa kumwilisha upendo wa Mungu kwa jirani, lakini hasa, kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na sababu mbali mbali. Mama Theresa wa Calcutta alichota daima ari, nguvu na mwamko wa upendo wake kutoka katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa.

Askofu mkuu Giovanni Pietro Dal Toso anakaza kusema,  Fumbo la Ekaristi Takatifu ni uwepo endelevu wa Kristo Yesu kati ya waja wake. Mama Theresa wa Calcutta, amefanikiwa kuwa ni chombo na shuhuda wa upendo na huruma ya Mungu kwa maskini kutokana na bidii, juhudi na mwamko wa kutaka kumwambata Kristo daima, kwa kusikiliza Neno la Mungu na kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa, chemchemi ya imani, matumaini na mapendo kwa Mungu na jirani! Habari Njema ya Wokovu iwasaidie waamini kutambua dhamana na wajibu walioupokea wakati walipobatizwa, kwani  kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo wameshirikishwa: ukuhani, unabii na ufalme wa Kristo, kumbe wanatumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo hadi miisho ya dunia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.