Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa \ Kanisa Ulimwenguni

Yatakayojiri maadhimisho ya Siku ya IX ya Familia Duniani, Dublin!

Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland linawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujiunga nao ili kusherehekea Injili ya familia kwa mwaka 2018.

22/03/2018 09:20

Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland linaendelea na mchakato wa maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya IX ya Familia Duniani itakayofanyika kuanzia tarehe 21-26 Agosti, 2018 Jimbo kuu la Dublin, nchini Ireland. Sehemu kubwa ya maandalizi haya anasema Askofu mkuu Diarmuid Martin, yanajikita katika tunu msingi za maisha ya kiroho, ndoa na familia na kwamba, familia yote ya Mungu nchini Ireland inashirikishwa kikamilifu. Hili ni tukio ambalo litazikutanisha familia kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ili kuadhimisha Injili ya familia, kusali na kutafakari: ukuu, utakatifu na changamoto za maisha ya ndoa na familia katika ulimwengu mamboleo. Mama Kanisa anapenda kukumbusha kwamba, familia ni kitovu cha maisha, ustawi na maendeleo ya Kanisa na jamii katika ujumla wake.

Jumatano, tarehe 21 Machi 2018, Askofu mkuu Diarmuid Martin wa Jimbo kuu la Ireland akiwa ameambatana na familia ya Michael na Mary Bushell na watoto wao wawili pamoja na familia ya Bibi Tobin Brenda na Bryan waliokuwa wameambatana na watoto wao waliwasilisha Sanamu ya Familia Takatifu, iliyozinduliwa mwaka 2017 ambayo kwa sasa inatembezwa kwenye familia mbali mbali nchini Ireland ili iweze kubarikiwa na Baba Mtakatifu Francisko. Hija hii, ilikuwa ni sehemu pia ya maadhimisho haya kwa kupata baraka kutoka kwa Baba Mtakatifu ili kuendelea kutangaza na kushuhudia Injili ya familia, furaha ya ulimwengu.

Ni maadhimisho ambayo yatapambwa kwa matukio mbali mbali kuzunguka Jimbo kuu la Dublin kama kielelezo cha mshikamano. Ratiba elekezi inaonesha kwamba, tarehe 21 Agosti 2018 kutakuwa na ufunguzi wa maadhimisho ya Siku ya IX ya Familia Duniani katika ngazi ya kitaifa, na kwamba, wahusika wakuu ni waamini wote katika majimbo 26 yanayounda Kanisa Katoliki nchini Ireland. Tukio la pili ni kuanzia tarehe 22-24 Agosti, 2018, siku tatu za Kongamano la Kichungaji kuhusu Familia. Wajumbe kutoka sehemu mbali mbali za dunia, watapata nafasi ya kusali, kutafakari na kujadiliana kuhusu kauli mbiu “Injili ya familia, furaha ya ulimwengu”. Vijana wa kizazi kipya watapata nafasi ya kushirikisha mawazo, mang’amuzi, vipaumbele na changamoto wanazokabiliana nazo katika mchakato wa maandalizi ya kutangaza na kushuhudia Injili ya familia kama furaha ya ulimwengu! Hata watoto ambao ni matunda ya upendo kati ya bwana na bibi, zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, watahusishwa nao!

Tukio la tatu litakuwa ni tarehe 25 Agosti 2018, Siku ya Kuadhimisha Injili ya Familia. Utakuwa ni muda wa sala, tafakari; shuhuda za imani kutoka kwa wawakilishi wa familia mbali mbali duniani. Tukio hili litapambwa kwa uwepo na ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko. Kilele cha maadhimisho ya Siku ya IV ya Familia Duniani kwa Mwaka 2018 ni Jumapili tarehe 26 Agosti 2018. Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu. Padre Tim Barlett, Katibu mkuu wa Maadhimisho ya Siku ya IX ya Familia Duniani kwa Mwaka 2018 anasema, Injili ya Familia ni moto wa kuotea mbali na kwamba, waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa kushiriki kikamilifu kadiri ya uwezo na nafasi zao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

22/03/2018 09:20