2018-03-22 09:00:00

Vijana "wamtwanga" maswali mazito na tete Baba Mtakatifu Francisko!


Baba Mtakatifu Francisko tarehe 19 Machi 2018 katika ufunguzi wa maadhimisho ya utangulizi wa Sinodi ya Maaskofu amepata fursa ya kusikiliza maswali makavu bila kupindisha maneno kutoka kwa vijana watano, waliokuwa wana wawakilisha vijana wenzao kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu anasema, Kanisa linataka kusikiliza kilio cha wasichana, wanawake na watoto wanaotumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu, viungo na utumwa mamboleo, mambo ambayo yanadhalilisha utu na heshima ya binadamu! Kuna watu ambao wamefilisika kiutu na kimaadili, kiasi kwamba, biashara ya binadamu imekuwa ni mahali pa kujipatia utajiri wa kupindukia.

Waathirika wa biashara ya binadamu na utumwa mamboleo ni watu wanaorubuniwa kwa ahadi ya kupatiwa kazi nzuri zaidi, matibabu au fursa za masomo, lakini wanapofika Ulaya na Marekani wanajikuta wakitumbukizwa katika biashara ya binadamu na utumwa mamboleo. Katika hali na mazingira kama haya, wasichana na wanawake wengi wanalazimika kukaa kimya kwa kuogopa kuzungumza ukweli, kwa ajili ya kuhifadhi heshima na staha ya familia zao na wakati mwingine, fedha chafu wanayoipata kutokana na biashara ya ngono inatumwa kwa wazazi na walezi wao na hivyo kuendelea “kutanua” bila kufahamu kwamba, watoto wao wananyanyasika na kudhalilishwa sana!

Ni watu wanaopata mateso makali, ikiwa kama hawawezi kutimiza masharti ya watu wanaowatunza! Baba Mtakatifu anawashukuru viongozi wa Kanisa, Serikali na Mashirika mbali mbali yanayoendelea kujizatiti kwa ajili ya kuwakomboa wasichana na wanawake kutoka katika utumwa mamboleo pamoja na kuwajengea uwezo wa kuanza tena maisha yao kwa imani na matumaini thabiti! Haiwezekani kuendeleza mfumo wa dume kwa kuwanyanyasa na kuwanyonya wanawake, kiasi hata cha kudharau utu na heshima yao kama watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Biashara na dhuluma hii inafanywa hata na Wakatoliki anasikitika kusema Baba Mtakatifu Francisko! Hapa kinachotafutwa ni fedha na wala si utu wa mtu!

Vijana wanasema, wamekosa dira na mwongozo sahihi katika maisha, kiasi hata cha kushindwa kujenga na kudumisha uhusiano mwema na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani zao! Baba Mtakatifu anawataka vijana kuangalia matatizo, changamoto na fursa zilizoko mbele yao kwa macho makavu bila kuzunguka zunguka kwani, wanaweza kutumbukia katika mazoea ya rushwa na ufisadi! Vijana watambue karama, vipaji na mapungufu yao, tayari ya kuyafanyia marekebisho kwa njia ya msaada wa vijana wenzao, wazazi na walezi. Vijana wawe na ujasiri pamoja na kuthubutu kujenga utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kupata mang’amuzi sahihi katika maisha na wito wao. Wakuze ndani mwao uhuru wa kweli na sanaa ya kusikiliza kwa makini, ili hatimaye, kufanya maamuzi sahihi katika maisha!

Vijana wanalishukuru Kanisa kwani kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko, wameweza kubadili na kupyaisha maisha yao kwa kuambata tunu msingi za maisha ya Kiinjili, kiutu na kitamaduni! Hii inatokana na ukweli kwamba, baadhi yao wamebahatika kupata elimu na malezi kutoka katika taasisi zinazoongozwa na kusimamiwa na Kanisa. Baba Mtakatifu anasema, shule panapaswa kuwa ni mahali pa malezi na majiundo makini ya binadamu katika medani mbali mbali za maisha. Vijana wanapaswa kutumia akili zao ili kujifunza vyema, wadumishe uhuru wa mawazo kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya wengi sanjari na kuratibu hisia na matamanio yao!

Baba Mtakatifu anawataka vijana kujifunza lugha ya moyo ambayo ni amana na urithi kutoka katika Maandiko Matakatifu, wazazi na walezi. Mchakato wa elimu unajikita katika maisha ya mtu binafsi, familia, shule na jamii inayowazunguka wahusika, ili kwa pamoja waweze kusaidia kutoa elimu endelevu! Vijana wajenge utamaduni wa kutumia vyema mitandao ya kijamii ili kujipatia elimu dunia, lakini wasikubali kamwe kuwa ni watumwa na waathirika wa mitandao ya kijamii! Vijana wasibaki wakielea kwenye ombwe, bali wakite miguu yao katika mambo halisi! Wajenge mahusiano na mafungamano ya kijamii na watu halisi wanaowazunguka, kuliko wale wanaopatikana kwenye mitandao ya kijamii na mara nyingi hawa ndio wale “watu wasiofahamika”.

Majandokasisi wanaojiandaa kwa ajili ya maisha, wito na utume wa Kipadre wanapaswa kujiandaa kikamilifu ili kukabiliana na changamoto zinazoendelea kuibuliwa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Mapadre wajitahidi kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa watu wake. Baba Mtakatifu anawataka Mapadre wawe ni mashuhuda wa mashauri ya Kiinjili, kwa kukumbatia na kuambata: utii, ufukara na usafi wa moyo! Wawe ni watu wema, waadilifu, wachapa kazi na wachamungu kwa maneno na maisha yao. Maisha na utume wa kipadre una changamoto nyingi, kumbe, ni wajibu na dhamana ya Maaskofu kuwa karibu sana na Mapadre wao vijana, ili wasimezwe na malimwengu,  kwani huko watakiona cha mtema kuni!

Mapadre wakumbuke daima kwamba, wametwaliwa kutoka miongoni mwa watu kwa ajili ya watu na kwa mambo matakatifu! Mapadre wajenge utamaduni wa maisha ya kijumuiya kwa kusaidiana, kuonyana na kutakatifuzana katika ukweli na uwazi; kwa upendo na kuthaminiana, kwani “majungu si mtaji na kama kweli ungekuwa mtaji, wangetajirika watu wengi”. Majandokasisi wajifunze utamaduni wa vijana wa kizazi kipya, lakini, wasitumbukie na kumezwa na malimwengu, wawe kweli ni vyombo na mashuhuda wa tunu msingi za Kiinjili tangu mwanzo wa malezi na majiundo yao ya Kipadre!

Watawa wa kike wanasikitika sana katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa kwamba, wamesahauliwa kwani, daima wamekuwa wakiambulia “makombo ya elimu” ambayo hata wakati mwingine yamepitwa na wakati! Baba Mtakatifu anazitaka familia kuwa ni chemchemi ya furaha ya Injili na warithishaji wa tunu msingi za maisha kwa watoto wao. Katika malezi na makuzi ya wito na maisha ya kitawa, kuna haja ya kuzingatia sana: majiundo ya kiakili, maisha ya kiroho na kitume; maisha ya kijumuiya pamoja na majiundo ya maisha ya kiutu ili kukuza na kudumisha: umoja, upendo, mshikamano na mafungamano katika maisha na utume wa kitawa! Uhuru wa kweli, dhamiri nyofu pamoja na nia ya dhati ni mambo yanayopaswa kuzingatiwa kabla ya mtu kuruhusiwa kuweka nadhiri zake. Majiundo makini katika hisia na vionjo ni muhimu sana. Kila hatua ya malezi inapaswa kupewa uzito wake ili kusaidia ukuaji wa mtu mzima: kiroho na kimwili.

Huu ndio mwelekeo sahihi katika malezi na majiundo ya kipadre, kitawa na hata kwa waamini walei! Baba Mtakatifu anawataka vijana watakapokuwa wazazi na walezi, wajizatiti katika kuwalea vyema watoto wao, ili waweze kukomaa vyema! Wawajengee mazingira yatakayowawezesha kukua vyema na hatimaye kujitegemea! Watawa na mapadre kamwe wasiwe ni watumwa wa fedha na mali, bali yote haya wayatumie kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu! Mwenyezi Mungu apewe kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wa Kanisa. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawataka viongozi wa Kanisa kuhakikisha kwamba, wanawapatia watawa wa kike fursa za elimu bora na majiundo makini, ili waweze kukabiliana na changamoto za utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia kwa imani, matumaini na uthabiti wa maadili na utu wema! Kanuni iwe ni kuwalinda, kuwasindikiza, kuwaelimisha, kuwasaidia, lakini zaidi kuwapenda ili waweze kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.