Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Maendeleo

Maaskofu Katoliki Tanzania: Kwani mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linaialika familia ya Mungu kujiuliza swali la msingi, Je, ndugu yako yuko wapi? - AFP

22/03/2018 15:05

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika ujumbe wake wa Kwaresima kwa Mwaka 2018 unaoongozwa na kauli mbiu “Basi enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi wangu” katika sura ya tatu, waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanaalikwa kutafakari wajibu wao kwa watanzania wenzao kwa kujitahidi kusoma alama za nyakati. Maaskofu wanaitaka familia ya Mungu nchini Tanzania kujiuliza maswali msingi kuhusu masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, ili kujenga umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa, kwa kutambua kwamba wote ni ndugu wamoja, tofauti zao msingi si mali kitu!

Moja ya majibu ya kukatisha tamaa kabisa katika Maandiko Matakatifu ni hili jibu la Kaini anapoulizwa na Mungu baada ya kuwa amemwua ndugu yake Abeli, “Yuko wapi Abeli ndugu yako?” (Mwa 1:9), Kaini anajibu, “Sijui, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?” (Mwa 4:9b). Kaini hajali na haoni kuwajibika kwa namna yoyote juu ya mustakabari wa ndugu yake. Lakini zaidi sana, anakuwa ni kielelezo cha dhamiri iliyokufa, kwani anajua kilichotokea na hajali lolote kuhusu hali ya ndugu yake! Ni kwa mtazamo huo basi nasi tujitathmini na tuwe wa kweli kwa dhamiri zetu. Je, kama wamisionari tunaowajibika kwa ndugu zetu, tunaelezaje hali ilivyo sasa katika jamii yetu ya Tanzania? Je, tunasoma alama za nyakati zetu vema kiasi kwamba tunaguswa kama wamisionari na tunapeleka Habari Njema inayoonesha kuwa sisi ni walinzi wa ndugu zetu?

Dalili za Nyakati Zetu Tanzania

Ili kuweza kuleta mabadiliko katika nafsi zetu na katika jamii yetu, Kanisa siku zote linatufundisha, kwa busara na hekima ya Roho wa Mungu, ulazima wa kusoma ishara za nyakati ili kujua ni nini kinachoendelea katika jamii. Kuhusu nchi yetu ishara za nyakati tutaziangalia katika maeneo matatu, yaani kisiasa, kijamii na kiuchumi, kwa lengo la kujitathimini.

Kisiasa: Kikatiba, nchi yetu inafuata mfumo wa demokrasia ya vyama vingi. Katiba na Sheria mbalimbali zimeainisha utaratibu wa kazi na shughuli za vyama vya siasa. Ili kuhakikisha kwamba kazi na shughuli za vyama vya siasa zinakuwa endelevu, vyama vyenye kukidhi vigezo hupewa ruzuku kupitia Bajeti ya Serikali inayopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania. Hata hivyo, shughuli za siasa bado zinaendelea kuzuiwa kwa kutumia vyombo vya dola.  Maana yake ni kwamba shughuli za kiuenezi za vyama vya siasa,  kama vile mikutano ya hadhara, maandamano, makongamano, mijadala na hata mikutano ya ndani, ambayo ni haki ya kila raia, zimekoma mpaka uchaguzi mwingine. Kisheria, huu ni uvunjifu wa Katiba na Sheria za nchi.

Vile vile baadhi ya vyombo vya habari vimefungiwa au kusimamishwa kwa muda, na hivyo kupunguza uwigo wa uhuru wa wananchi wa kupata habari, maoni na wa kujieleza. Kufungiwa huku kwa vyombo vya habari kumeenda sambaba na kuminya uhuru wa mahakama na bunge kwa njia ya kuminya haki wabunge na kutowapa nafasi ya mikutano ya hadhara kama haki yao ya msingi ya Kikatiba. Katika mazingira haya ni rahisi kwa jamii kufarakana na hata kujenga chuki kiasi cha kuhatarisha amani, usalama na hadhi ya uhai wa binadamu. Kumekuwapo pia hali ya vurugu katika chaguzi mbalimbali. Chaguzi hizi zinaacha nyuma uchungu, hasira, tama ya kulipa kisasi na hata kususia chaguzi nyingine. Hali hii ni hatari kwa mustakabali wa Taifa letu. Tukiiachia hali hii izoeleke tushishangae huko mbeleni kujikuta katika mifarakano mikubwa zaidi itakayobomoa misingi ya amani na umoja wa kitaifa.

Kiuchumi: Hapa ni vema tukajiuliza maswali ya msingi kabisa kuhusu kujali katika maisha ya walio wanyonge ili umisionari wetu ulete nafuu katika mahitaji ya lazima kwa wale wanyonge, maskini na walio pembezoni mwa jamii. Hebu tujiulize: Tunazitumuaje mali na rasilimali nyingine tulizokabidhiwa na Mungu kama mawakili wake? Tunalipa kodi stahiki kwa ajili ya kugharamia huduma za jamii ambazo serikali inapaswa kutoa kwa ajili ya wananchi? Wale ambao tu waajiri, tunawajali wafanyakazi na wahudumu wetu kwa kuwalipa mishahara ya halali? Wale ambao tu wafanya biashara, tunalipa kodi zote kihalali? Wale ambao tumepewa jukumu la kukusanya kodi, ushuru na ada nyingine tunafanya hivyo kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu husika? Tunaepukanaje na kishawishi cha rushwa, hongo, mulungula, magendo au aina yoyote ya ufisadi?

Kijamii: Sasa hivi bado kuna kishawishi cha kupingana na azma ya kuboresha maisha ya kijamii. Hii inajidhihirisha kwa njia ya uhasama, ugomvi, ukatili kwa watoto na wanawake, ujambazi, na maovu mengine kiama hayo miongoni mwa jamii yetu. Kama wamisionari tunaopaswa kuleta habari njema kwa ndugu zetu, kwa nini turuhusu roho ya namna hii ambayo kwa kweli ni roho ya Kaini inayouliza kwa jeuri kabisa: ‘Mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?’

Ujumbe wa Kwaresima kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa mwaka 2018.

 

 

22/03/2018 15:05