Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Mahubiri

Jipatanisheni na Mungu ili kuonja huruma na upendo wake wa daima!

Papa Francisko anawaalika waamini kujipatanisha na Mungu ili kuonja uaminifu, huruma na upendo wake wa daima!

22/03/2018 14:20

Mwenyezi Mungu daima ni mwaminifu kwa ahadi zake, changamoto na mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanakimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, ili aweze kuwasafisha na kuwatakasa na hatimaye, aweze kuwakumbatia kwa upendo wake usiokuwa na kifani! Wakristo wanapokaribia kuanza maadhimisho ya Juma kuu, Kanisa linapotafakari kuhusu: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, wanahamasishwa kwa namna ya pekee, kutafakari kuhusu upendo wa Mungu unaojidhihirisha katika Agano la Kale, pale Mwenyezi Mungu alipofunga Agano na Abramu na kumpatia jina jipya la Ibrahim. Agano hili limekuwa ni endelevu katika katika maisha na historia ya Wayahudi, licha ya dhambi na ibada kwa miungu wa kigeni!

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamis, tarehe 22 Machi 2018 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican. Anaendelea kufafanua kwamba, upendo wa Mungu unaweza kulinganishwa na upendo wa wazazi kwa watoto wao. Mwenyezi Mungu kamwe hawezi kuwasahau watoto wake ndiyo maana ameendelea kuwa mwaminifu kwa Agano lake, licha ya udhaifu, dhambi na mapungufu yaliyooneshwa na watoto wake.

Katika hali ya dhambi na ulegevu wa moyo, mwamini anahamasishwa na Mama Kanisa kukimbilia katika huruma na upendo wa Mungu, chemchemi ya matumaini ya maisha mapya kwani, Mwenyezi Mungu, daima anawangojea waja wake ili aweze kuwatakasa na kuwafunika kwa upendo wake wa daima, kielelezo makini cha uaminifu wake. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Kristo Yesu katika Injili ya siku, anasema, furaha ya kweli inafumbatwa katika matumaini kama ilivyokuwa kwa Ibrahimu alivyoshangilia kwa vile alivyoiona siku yake, akafurahi. Ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu ni kiini na chemchemi ya furaha kwa waja wake. Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha mahubiri yake kwa kuwataka waamini kuchunguza dhamiri zao, ili kuona ikiwa kama bado ni waaminifu, kwa huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, Mungu ambaye kamwe hawezi kuwaacha pweke. Waamini wanapaswa kuonesha furaha yao katika ufufuko wa Kristo Yesu, kwani Mwenyezi Mungu anawapenda jinsi walivyo kama wazazi wanavyowapenda watoto wao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

22/03/2018 14:20