Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Nyaraka

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Siku ya 33 ya Vijana Duniani, 2018

Papa Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya 33 ya Vijana Duniani kwa mwaka 2018 anawataka vijana kuorodhesha mambo yanayowaogofya katika hija ya maisha yao hapa duniani.

21/03/2018 07:08

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya 33 ya Vijana Duniani ambayo kwa Mwaka 2018 inaadhimishwa kwa ngazi ya kijimbo, inaongozwa na kauli mbiu “Usiogope Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu”. Lk. 1:30. Huu ni ujumbe wa pili kuandikwa na Baba Mtakatifu kwa ajili ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kuanzia tarehe 22 -27 Januari 2019 huko Panama. Maadhimisho ya Mwaka 2018 kwa ngazi ya Kijimbo yatafanyika tarehe 25 Machi, Mama Kanisa anapoadhimisha Jumapili ya Matawi, mwanzo wa maadhimisho ya Juma kuu, Kanisa linapofanya kumbu kumbu ya: Mateso, kifo na Ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu!

Baba Mtakatifu katika ujumbe wake, anapenda kukazia mambo makuu manne mintarafu maisha na utume wa Bikira Maria katika kazi ya ukombozi: yaani: Usiogope, Baba Mtakatifu anawaalika vijana kuorodhesha mambo yanayowaogofya katika safari ya maisha yao hapa duniani! Kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, kila mmoja wao anaitwa kwa jina na kwamba, vijana wamepata neema kwa Mungu. Vijana wawe na ujasiri ili kukabiliana na changamoto mamboleo.  Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha vijana kwamba, maadhimisho ya Mwaka 2018 ni sehemu ya maandalizi ya Siku ya  34 ya Vijana Duniani itakayoadhimishwa nchini Panama sanjari na maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana inayoongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya miito”.

Mama Kanisa anataka kuwasikiliza na kutembea na vijana katika hija ya maisha yao, kwa kutambua kwamba, wao wana thamani kubwa sana mbele ya Mungu, Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Wakumbuke kwamba, katika hija ya maisha yao, daima wanasindikizwa na Bikira Maria ambaye Mwenyezi Mungu alimtendea makuu katika maisha yake. Anawafundisha vijana kuangalia historia yao ya nyuma, kusikiliza kwa makini sauti ya Mungu inayowatia shime pamoja na kuwapatia neema ili kuweza kujibu kwa makini “Usiogope Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu”.

Baba Mtakatifu anafanya tafakari ya kina kuhusu maneno ya Malaika Gabrieli kwa Bikira Maria aliyemwambia kuwa usiogope Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Ni maneno ambayo yalimshtua sana Bikira Maria, kwa kutambua unyonge wake na ukuu wa Mungu katika maisha yake. Aliona changamoto kubwa mbele ya maisha yake, kama ilivyo hata leo hii kwa vijana wanapoangalia hali ya maisha yao ya mbeleni pamoja na wito wao. Katika mazingira kama haya, watu wote wanakumbwa na hofu pamoja na mashaka, kwani hili ni jambo la kawaida.

Hata vijana wa kizazi kipya leo hii, wanayo mambo ambayo wanayaogopa: Pegine, hawaeleweki au kupendwa; ni watu wasiokuwa na utambulisho makini, kiasi cha kujikuta wakiwa wanajificha kwenye vinyago, ili kutoonesha ule udhaifu wao. Vijana wengine wanashindwa kupata usalama katika hisia zao, kiasi cha kuendelea kuandamwa na upweke hasi; kuna baadhi ya vijana hawana fursa za ajira, kiasi kwamba, wanashindwa kufanya maamuzi magumu katika maisha ili kutekeleza ndoto zao. Hata wale wanao amini barabara, nao pia wanakumbana na hofu na wasi wasi katika maisha. Katika msongo wa mawazo na mashaka, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika vijana kufanya mang’amuzi, ili kutenda kwa haki na busara, kwa kutambua hofu na mashaka yanayowazunguka kiasi cha kuwa ni kizuizi cha maendeleo yao kiroho na kimwili.

Papa Francisko anawataka vijana kukabiliana na changamoto hizi katika msingi wa ukweli na uwazi, kwani haya ni mambo ya kawaida ambayo yaliwakumba hata watu maarufu katika Maandiko Matakatifu. Hata Kristo Yesu alipambana na hofu na woga katika maisha na utume wake! Vijana watambue sababu zinazowafanya kuwa na hofu! Je, ni kwa sababu hawana imani? Au wanataka kukimbia hali yao? Mang’amuzi yanawasaidia vijana kupambana vyema na hali yao kwa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu atakayewaongoza hadi kwenye ukamilifu wa maisha. Mang’amuzi yawasaidie vijana kuangalia undani wa maisha yao, lakini daima wakumbuke kwamba, wito ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Hapa, vijana wajenge na kudumisha moyo wa sala na tafakari kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria ili kujenga mahusiano mema na Mwenyezi Mungu. Vijana wajenge ari na moyo wa kusoma na kutafakari Maandiko Matakatifu; wakimbilie kwenye Mahakama ya huruma ya Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho na kupata chakula cha maisha ya kiroho kwa njia ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Vijana wajenge na kudumisha utamaduni wa kukutana na vijana wenzao katika safari ya maisha yao ya imani, kwani hawa pia wanaweza kuwa ni msaada wa kufanya maamuzi ya busara kama ilivyokuwa kwa kijana Samueli na Mzee Eli aliyemwezesha Samuel kusikiliza na kujibu kwa ukamilifu wito wa Mungu katika maisha yake.

Hawa ni kama vile: mapadre, watawa na waamini walei wanaoweza kuwasaidia kutambua utajiri wa neema na maisha ambayo Mwenyezi Mungu amewakirimia. Vijana wajenge utamaduni wa kutengeneza nafasi katika maisha na mazingira yao, ili waweze kukua na kukomaa; waendelee kuwa na ndoto katika maisha, daima wakifurahia kuwa pamoja na wengine, bila kuwaogopa wala kuwabeza, ili kujenga umoja, udugu na mshikamano; mambo yanayofukuzia mbali giza katika moyo wa vijana. Vijana wajitahidi kujenga na kudumisha mahusiano mema yanayofumbatwa katika ukweli na uwazi wa maisha!

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika vijana kumwangalia Bikira Maria kwa kutambua kwamba, hata wao wanaitwa kwa majina, kielelezo cha uhusiano wao wa pekee na Muumba! Majina yao yanafumbata kwa namna ya pekee maana na fumbo la maisha; wito na utume wake kama sehemu ya kushiriki katika mchakato wa utakatifu wa maisha unaomwezesha kijana kuwa ni zawadi safi inayompendeza Mungu na jirani. Huu ndio mzizi wa mapokeo ya watawa kupewa majina mapya wanapoweka nadhiri zao. Wito wa Mungu ni kwa ajili ya mtu binafsi, ili kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa kama zawadi safi kabisa! Vijana wanakumbushwa kwamba, kuitwa kwa majina ni heshima kubwa sana machoni pa Mwenyezi Mungu, watambue kwamba, wanapendwa na kuheshimiwa sana, changamoto na mwaliko kwa vijana kukaribisha majadiliano na Mwenyezi Mungu kwa moyo wa furaha na bashasha, pale wanaosikia kwamba, wanaitwa kwa majina!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Bikira Maria hakuwa tena na sababu ya kuogopa kwani alipewa neema inayo maanisha kwamba, alipata upendo wa pekee kutoka kwa Mungu, unaoendelea pia kufunuliwa miongoni mwa vijana. Neema itaendelea kuwaambata vijana hasa katika majaribu na kipindi cha giza katika maisha yao, ili kuwajengea imani na ujasiri; mambo yanayopaswa kupyaisha kila siku ya maisha ili kukabiliana na changamoto za maisha! Mwenyezi Mungu ana mpango na kila mtu katika maisha yake, changamoto ni kwa vijana kushirikiana na Mungu katika kutekeleza ndoto zao halali sanjari na kushirikiana na watu wengine ndani ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake.

Baba Mtakatifu anawataka vijana kuwa na ujasiri katika kupambana na changamoto mamboleo, bila kuzikimbia au kuzikwepa, kwani Mungu akiwa upande wao, ni nani aliye juu yao? Licha ya hofu na mapungufu ya kibinadamu, vijana wanapaswa kuwa na ujasiri kwa kutambua kwamba, Khalifa wa Mtakatifu Petro na Kanisa lina watumainia sana kwamba, ni zamu yao kuweka matumaini yao kwa Kanisa. Vijana wahakikishe kwamba, wanatumia nguvu ya ujana wao kuleta mageuzi katika maisha, kwa kujiandaa kuwajibika barabara; kwa kuwa na upendo wa dhati kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria; upendo unaowajalia kuwa ni zawadi kwa wengine!

Sifa na ukuu wa Bikira Maria vitalisaidia Kanisa kusonga mbele daima licha ya mapungufu yake ya kibinadamu, jambo la msingi ni kumwachia nafasi Bikira Maria ili aweze kuligusa kwa fadhila ya upendo, ili kuwamegea wengine pia! Upendo huu unapaswa kumwilishwa katika huduma na majitoleo makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; upendo uwe ni chachu inayogeuza nyuso za watu kuwa na furaha. Mwenyezi Mungu anasubiri jibu makini kutoka kwa vijana wa kizazi kipya kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawataka vijana kujiandaa kikamilifu katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 huko Panama. Haya ni maadhimisho ya kuonesha ujasiri na kukabiliana na changamoto mamboleo kwa imani na matumaini bila kubweteka hata kidogo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

21/03/2018 07:08