2018-03-21 15:40:00

Papa Francisko kuadhimisha Ibada ya Alhamisi Kuu, Gerezani, R. Coeli


Mama Kanisa anafundisha kwamba, Kristo Yesu aliwapenda watu wake upeo na alipokuwa anakaribia “Saa yake” ili kutoka hapa ulimwenguni na kurudi kwa Baba yake wa mbinguni, Siku ile ya Alhamisi kuu, walipokuwa wakila, aliwaosha mitume wake miguu yao na kuwapatia Amri ya upendo inayomwilishwa katika huduma ya upendo, hasa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Akataka pia kuwapatia amana ya upendo huu na kuendelea kubaki kati yao na na kuendelea kuwashirikisha Fumbo la Pasaka, aliweka Sakramenti ya Ekarissti Takatifu, kielelezo cha sadaka, shukrani, kumbu kumbu endelevu na uwepo wake kati yao katika alama ya Mkate na Divai!

Kumbe, Ekaristi Takatifu ni kumbu kumbu endelevu ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu inayoadhimishwa na Mama Kanisa hadi Kristo Yesu atakaporudi tena kuwahukumu wazima na wafu na wala Ufalme wake hautakuwa na mwisho! Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ni Sakramenti Pacha na Daraja Takatifu ya Upadre. Mapadre hutekeleza kazi takatifu hasa katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, wakitenda kwa nafsi ya Kristo, wakitangaza fumbo lake pamoja na kuyaunganisha maombi ya waamini pamoja na sadaka ya Kristo Msalabani inayoadhimishwa katika Ibada ya Misa Takatifu.

Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua na kuthamini amana na utajiri unaofumbatwa katika maadhimisho ya Alhamisi Kuu, na kadiri ya utaratibu wake, tarehe 29 Machi 2018, majira ya saa 10:00 jioni kwa saa za Ulaya, anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, Sherehe ya Karamu ya Bwana, kwenye Gereza kuu la “Regina Coeli” lililopo mjini Roma. Baba Mtakatifu atapata nafasi ya kukutana na kusalimiana na wafungwa wagonjwa na baadaye ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kuwaosha miguu wafungwa 12, kielelezo cha upendo wa Kristo unaomwilishwa katika huduma ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baadaye, Baba Mtakatifu atakutana na kuzungumza na wafungwa katika eneo la VIII la Gereza kuu la “Regina Coeli”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.