2018-03-21 14:11:00

Adhimisho la Ekaristi Takatifu linapyaisha na kuchochea utakatifu!


Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanasimama kidete kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu! Kama ilivyo kwa mazingira, Wakristo ambao ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo wanapaswa kuhakikisha kwamba, wanarutubisha maisha yao ya kiroho kwa kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu. Ibada ya Misa Takatifu inapaswa kusaidia kukuza na kudumisha upendo wa kidugu, ili neema na baraka kutoka kwa Kristo Mfufuka ziweze kusaidia upyaisho wa maisha na utume wao! Kristo Yesu, anajitoa sadaka ili awe ni chakula kinachoponya dhambi na kuwakirimia waja wake utakatifu wa maisha, ili kuishi kadiri ya mapenzi ya Mungu. Ekaristi Takatifu iwasaidie waamini kukutana na Kristo Yesu pamoja na kutambua dhamana kwamba, wao ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani, Kanisa. 

Baba Mtakatifu ameyasema haya wakati wa Katekesi yake kuhusu Ibada ya Misa Takatifu, Jumatano, tarehe 21 Machi 2018 kwenye Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Komunyo Takatifu anasema Baba Mtakatifu, ni muungano wa maisha ya kiroho unaopata chimbuko lake katika ushiriki wa adhimisho la Misa Takatifu, kwa kumpokea Kristo Yesu anayejisadaka katika maumbo ya Mkate na Divai, yaani Mwili na Damu yake Azizi.

Liturujia ya Neno la Mungu na Liturujia ya Ekaristi Takatifu ni mambo msingi yanayowawezesha waamini kufanana na Kristo anayeendelea kujisadaka kwa njia ya Mapadre wanapoadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na Mashemasi wanaposhiriki katika kugawa Mafumbo ya Kanisa. Baada ya Padre kiongozi wa  Ibada ya Misa Takatifu kuvunja hostia na kuiweka katika kikombe na kusali kwa sauti ndogo, hatimaye, anawaalika waamini kwa kusema, “Huyu ndiye Mwana Kondoo wa Mungu aondoaye dhambi za ulimwengu, heri yao walioalikwa kwa kwenye karamu ya Bwana. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hii ni karamu ya harusi ya Mwana Kondoo, kwani Kristo Yesu, ni mchumba wa Kanisa, anayewaalika waja wake kujenga umoja na mshikamano wa dhati, kwa kujichotea furaha na utakatifu wa maisha kutoka kwake! Hii ni changamoto ya kuchunguza dhamiri katika mwanga wa imani ili kuangalia yale mambo yanayojenga ukuta kati yao na utakatifu wa Kristo, ili kuomba huruma, upatanisho na msamaha wa dhambi, kwa kutambua kwamba, huruma na upendo wake hauna mipaka.

Waamini wawe wepesi anasema Mtakatifu Ambrosi kukimbilia kwa Mwana Kondoo wa Mungu ili aweze kuwapatia dawa ya kuganga na kuponya dhambi na udhaifu wao wa kibinadamu! Waamini wanatambua kwamba, kwa hakika hawastahili Kristo Yesu aingie ndani mwao, lakini wanamwomba aseme neno moja tu na roho yao itapona! Waamini wanajipanga mstari ili kwenda kupokea Ekaristi Takatifu, lakini ukweli wa mambo ni kwamba, Kristo Yesu mwenyewe ndiye anayejitaabisha kuwaendea waja wake, ili kuwalisha na hatimaye, kuwakirimia upya wa maisha, ili walau kuweza kufanana na Kristo Yesu. Ndiyo maana, waamini wanapopokea Ekaristi Takatifu kwa imani wanaitikia! Amina!

Hii ina maana kwamba, waamini wanakuwa ni sehemu ya Kristo Yesu, kwa kumpokea katika maumbo ya Mkate na Divai. Mama Kanisa anatamani kwamba, waamini washiriki Ekaristi Takatifu iliyobarikiwa wakati huo huo wa Ibada ya Misa Takatifu na pale inapowezekana waamini wakomunishwe katika maumbo yote mawili: yaani Mkate na Divai: Mwili na Damu Azizi ya Kristo Yesu! Kanisa Katoliki linafundisha kwamba, hata kama mwamini akipokea umbo moja tu, anampokea Kristo Yesu. Kumbe, waamini wanaweza kupokea Ekaristi Takatifu kwa kusimama au kupiga magoti kadiri ya taratibu zilizotolewa na Maaskofu mahalia. Baada ya Komunyo Takatifu, waamini wanashauriwa kuwa na ukimya, ili kumshukuru Kristo Yesu aliyekubali kujisadaka kwa ajili yao. Pale inapofaa, waamini wanaweza kuimba pia wimbo wa kushukuru. Ibada ya Ekaristi Takatifu inahitimishwa kwa Sala baada ya Komunyo. Baada ya kuimarishwa katika imani, waamini wanatumwa kwenda kuzaa matunda mema kwa kuishi kama wafuasi wa Kristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.