2018-03-20 14:55:00

Tanzia: Kardinali Keith Patrick O'Brien amefariki dunia!


Baba Mtakatifu Francisko katika salam zake za rambi rambi kwa Askofu mkuu Leo W. Cushley, wa Jimbo kuu la St. Andrews na Ednburgh, anasema, amepokea taarifa za Msiba wa Kardinali Keith O’Brien kwa masikitiko makubwa na kwamba, anamwomba awafikishie salam zake za rambi rambi ndugu, jamaa na wale wote walioguswa na msiba huu mzito! Anamwombea huruma ya Mungu pamoja na kuendelea kuwakumbuka katika sala na sadaka yake, familia ya Mungu Jimbo kuu St. Andrews na Ednburgh.

Kardinali Keith Michael Patrick O’Brien, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Saint Andrews na Ednburgh, Scotland, amefariki dunia, tarehe 19 Machi 2018. Alizaliwa tarehe 17 Machi 1938 huko Ireland ya Kaskazini. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, akapewa Daraja takatifu ya Upadre tarehe, 3Aprili 1965. Baadaye alijiendeleza katika masomo na hatimaye kujipatia diploma katika elimu kutoka Chuo kikuu cha Ednburgh. Akateuliwa kuwa Askofu mkuu na kuwekwa wakfu mwaka 1985. Kati ya mwaka 1996-1999 aliteuliwa kuwa Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Argyll na Isles.

Aliteuliwa kuwa Kardinali kunako mwaka 2003 na Mtakatifu Yohane Paulo II. Kati ya mwaka 2002 hadi mwaka 2012 alikuwa ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Scotland.  Mwaka 2013 akang’atuka kutoka madarakani. Hayati Kardinali Keith Michael Patrick O’Brien alikabiliwa na shutuma za kimaadili na Papa Francisko alipoingia madarakani, wakakubaliana kwamba, atoke nchini Scotland na kwenda mahali pa faragha kwa ajili ya kusali, kutafakari, toba na wongofu wa ndani na hatimaye, akaamua kung’atuka kutoka madarakani baada ya muda mrefu wa sala na tafakari ya kina! Hakushiriki katika mkutano wa Baraza la Makardinali kwa ajili ya uchaguzi wa Papa Francisko kutokana na sababu za kimaadili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.