Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu, tarehe 19 Machi 2018 katika hotuba elekezi amewataka vijana wanaoshiriki katika maadhimisho ya utangulizi wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, kuanzia tarehe 19-25 Machi 2018 hapa mjini Vatican kushirikisha mawazo yao kwa ujasiri bila kuogopa pamoja na kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini. Kardinali Lorenzo Baldisseri aliwakaribisha wajumbe wa vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia na kuwafafanulia wajibu wao kama wawakilishi wa vijana wenzao! Bara la Afrika linawakilishwa na wajumbe kutoka katika nchi 34.
Vijana katika ushuhuda wao mbele ya Baba Mtakatifu Francisko pamoja na umati wa vijana uliokuwa unafuatilia ufunguzi huu kwa njia ya mitandao ya kijamii, wameelezea kuhusu matatizo yanayowakumba vijana pamoja na matarajio yao kwa siku za usoni! Mipasuko na kinzani za kijamii, kisiasa na kidini inayopelekea wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji, wengi wao wakiwa ni vijana. Kuyumba kwa imani, maadili na utu wema miongoni mwa vijana wa kizazi kipya pamoja na changamoto ya kujizatiti katika upyaisho wa maisha na utume wa vijana!
Kilio cha vijana ni kutaka kupata elimu bora; ustawi na maendeleo yao; changamoto pevu ya utandawazi na maendeleo ya sayansi ya mawasiliano ya jamii pamoja na utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba na kifo laini dhidi ya Injili ya uhai na matumaini! Ukanimungu, vitendo vya kigaidi na uvunjwaji wa sheria na haki msingi za binadamu zinazofanywa na vijana; mahusiano tenge kati ya vijana na wasichana na matokeo yake ni mimba za utotoni zinazozima ndoto za wasichana wengi kupata maisha bora zaidi kwa siku za usoni!
Tendai Karombo, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Wakatoliki Zimbabwe, amewawakilisha wajumbe kutoka Barani Afrika kwa kudadavua changamoto zinazowakumba vijana Barani Afrika katika masuala ya kiuchumi na kijamii hasa kutokana na idadi kubwa ya vijana kutokupata fursa za ajira na matokeo yake ni uwezo mdogo sana wa kiuchumi unaowatatiza vijana wengi kiasi cha kujikuta wakiwa ni tegemezi kwa wazazi na walezi wao. Kazi za suluba kwa watoto wadogo; kuporomoka kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na mshikamano wa kijamii ni kati ya mambo ambayo yanaendelea kuleta athari kubwa kwa maisha ya vijana wengi Barani Afrika.
Matokeo yake ni umaskini, wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kutoka Barani Afrika; vita, kinzani na mipasuko ya kidini, kisiasa na kikabila bila kusahau kwamba, leo hii vijana wengi wamekumbwa na tamaa ya malimwengu, wanataka mambo makubwa, lakini, hawana uwezo wa kiuchumi, matokeo yake ni utumwa mamboleo na biashara ya ngono! Vijana Barani Afrika, wanawaomba Mababa wa Kanisa kuwapatia majiundo makini na endelevu katika maisha ya kiroho na kiutu; kuwapatia jukwaa la kuweza kushirikisha uzoefu na mang’amuzi yao katika maisha na utume wa Kanisa pamoja na kuhakikisha kwamba, vijana Barani Afrika wanaendelezwa zaidi ili kuchangia, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!
Vijana wanatumaini kuona Bara la Afrika likiwa katika amani, utulivu, upendo na mshikamano, kwani wamechoka kusikia milio ya bunduki kila siku. Wanapenda kupata elimu itakayowajengea uwezo wa kupambana na mazingira badala ya mfumo wa sasa wa elimu unaowaandaa kwa ajili ya kazi za ofisini tu! Kanisa liendelee kuwa ni sauti ya kinabii, kwa kuzungumza ukweli na uwazi, kwa kuwatetea wanyonge na kusimamia haki msingi za binadamu, utu na heshima yake!
Vijana kutoka Amerika wanasikitika kusema kwamba, kuna mpasuko mkubwa miongoni mwa vijana Amerika kutokana na tamaduni, uwezo wa kiuchumi na changamoto wanazokabiliana nazo! Wanakabiliwa na ubinafsi na uchoyo, hali ambayo vijana wanaweza kuivuka kwa kujenga umoja, udugu na mshikamano wa dhati. Kuba mabadiliko makubwa ya kijamii, yanayowaacha vijana wengi wakiwa bado legelege katika maisha yao ya kiroho na kiutu! Vijana wakiwezeshwa na kushirikishwa katika maisha na utume wa Kanisa wataweza kuchangia kwa kiasi kikubwa!
Kanisa liwasaidie vijana katika safari ya mang’amuzi ya miito yao, ili waweze kuichagua kwa hekima na busara, ili hatimaye, waweze kudumu katika utakatifu, ukweli na uaminifu! Ukosefu wa utawala bora, athari za myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa, ubaguzi, umaskini, athari za mabadiliko ya tabianchi, vita, biashara ya binadamu na matumizi haramu ya dawa za kulevya; utumwa mamboleo pamoja na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji. Zote hizi ni changamoto zinazopaswa kupewa majibu muafaka, ili kuwajengea vijana matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi!
Vijana kutoka Asia, wanasikitishwa sana na mfumo dume, unaowabagua watoto wa kike kiasi cha kuwafanya kuwa ni vitendea kazi na vyombo vya kuzima kiu na matamanio ya wanaume. Kuna madhara makubwa ya mafungamano ya kijamii, tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii. Matokeo yake ni vijana wengi kukumbwa na ugonjwa sonona na wengi wao kutema zawadi ya maisha kwa kujinyonga hadi kufa! Kinzani na mipasuko ya kijamii; utamaduni wa kifo; malumbano ya kidini yasiyokuwa na tija, ustawi na mafao ya wengi pamoja na wimbi kubwa la matamanio ya ndoa za watu wa jinsia moja, hali ambayo inakwenda kinyume kabisa cha utu na heshima binadamu, lakini baadhi ya jamii zinataka kuhalalisha mambo haya kwa kisingizio cha haki msingi za binadamu! Ikumbukwe kwamba, ushoga si sehemu ya haki msingi za binadamu!
Vijana kutoka Barani Ulaya wanakwazika kutokana na ongezeko la ukanimungu, wimbi la uvunjifu wa haki msingi za binadamu kutokana na vitendo vya kigaidi; utamaduni wa kifo pamoja na kuyumba kwa msingi ya utawala bora na utawala wa sheria; kashfa za nyanyaso za kijinsia ambazo zimelikumba Kanisa zimeacha machungu makubwa kwa vijana wengi Barani Ulaya kiasi hata cha kuyumba katika imani, maadili na utu wema! Vijana wanalitaka Kansa Barani Ulaya kujikita katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda kama kielelezo cha imani tendaji, changamoto kubwa kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu! Waamini nao wanapaswa kupyaisha maisha na utu wao mintarafu tunu msingi za Kiinjili.
Kwa upande wa vijana kutoka Oceania, wanakabiliwa zaidi na: umaskini wa hali na kipato; wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji; changamoto ya majadiliano ya kidini na kiekumene; athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na ukosefu wa utambulisho wao ni kati ya mambo makubwa yanayowatatiza vijana wengi. Vijana wa Oceania wanasema, wana matumaini makubwa kwa Kanisa kama Sakramenti ya umoja, upendo na mshikamano dhidi ya utamaduni wa kifo. Kwa ufupi, huu ndio ushuhuda kutoka kwa wajumbe wa vijana wanaoshiriki katika utangulizi wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, itakayotimua vumbi rasmi mwezi Oktoba, 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Vijana: Imani na mang’amuzi ya miito”.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©. |