Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Nyaraka

Papa Francisko: Vijana ni chachu ya mabadiliko katika Kanisa na Jamii

Papa Francisko anawataka vijana kupaaza sauti zao ili ziweze kuwafikia viongozi mbali mbali kabla ya kufanya maamuzi kuhusu hatima ya maisha yao!

20/03/2018 15:29

Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana inaongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito”. Kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho haya, hivi karibuni Baba Mtakatifu Francisko aliwaandikia barua vijana wa kizazi kipya akiwatangazia maadhimisho haya kwani wao ni sehemu muhimu sana ya maisha na utume wake na kwamba, anawabeba kama “mbereko” moyoni mwake yaani hakuna hata mfano! Barua hii kwa mara ya kwanza ilichapishwa tarehe 13 Januari 2017 na kusambazwa sehemu mbali mbali za dunia.

Baba Mtakatifu anawataka vijana kujihusisha kikamilifu katika maandalizi ya Sinodi hii kama sehemu ya mchakato unaowapatia nafasi ya kutafakari wito wao kama ilivyokuwa kwa Mzee Abramu, Baba wa imani aliyeamriwa na Mwenyezi Mungu kutoka katika nchi yake, jamaa na nyumba ya baba yake aende katika nchi atakayomwonesha! Vijana wanahamasishwa kutoka ili kujiandaa kwa ajili ya maisha wasiyoyafahamu bado, lakini kwa kujenga mahusiano salama kwani Mwenyezi Mungu ndiye anayewasindikiza. Huu ni mwaliko wa kusikiliza sauti ya Mungu inayosikika nyoyoni mwao kwa njia ya Roho Mtakatifu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Mwenyezi Mungu alipomwambia Abramu “Ondoka” hakumtaka kukimbia ulimwengu, bali huu ulikuwa ni mwaliko wa wito wa kuacha yote na kwenda mahali ambapo Mwenyezi Mungu angemwonesha! Na kwa vijana mahali hapa ni Jamii inayosimikwa katika haki na udugu, jambo ambalo vijana wengi wanalitamani kutoka katika sakafu ya nyoyo zao. Lakini, kwa bahati mbaya neno “Ondoka” linapata maana mpya katika ulimwengu mamboleo kwani ni kuondokana na tabia ya kutenda mabaya, ni kutoka katika hali ya ukosefu wa haki na zaidi ya hayo ni kutoka katika vita!

Kuna umati mkubwa wa vijana unaojikuta ukiogelea katika “mtutu wa bunduki” na wengi wao wanalazimika kukimbia kutoka katika nchi walikozaliwa! Lakini, Baba Mtakatifu anasema, kilio chao kinasikika hadi mbele ya Mungu kama ilivyokuwa kwa Waisraeli. Huu ni mwaliko wa kumwendea Kristo Yesu na kuona mahali anapoishi ili kuweza kushinda pamoja naye kama walivyofanya wale Mitume wa kwanza wa Yesu. Mwaliko huu, bado unaendelea kusikika masikioni mwa vijana wengi ili hatimaye, waweze kushiriki katika furaha ya kweli.

Jambo hili linawezekana kwa kuanza hija ya mang’amuzi ili kutambua mpango wa Mungu katika maisha yao! Hii ni safari yenye milima na mabonde, kuna kusimama na kuanguka chali kama mende! Lakini Mwenyezi Mungu, ni mwingi wa huruma na mapendo, atawanyooshea mkono na kuwainua tena! Baba Mtakatifu anawakumbusha kwamba, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani nchini Poland aliwauliza ikiwa kama mambo yanaweza kubadilika na wao kwa jeuri wakamjibu wakisema “Ndiyo”. Kilio hiki kinapata chimbuko lake kutokana na ukosefu wa haki na kamwe hakiwezi kushikishwa adabu na utandawazi pamoja na utamaduni usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine!

Baba Mtakatifu anawaalika vijana kusikiliza sauti ya Mungu kutoka katika undani wao, bila kuogopa kwani yupo pamoja nao ili kuwalinda na kuwategemeza! Ulimwengu bora unajengwa na kudumishwa kutokana na mchango wa vijana wa kizazi kipya wanaoonesha ukarimu, kwa kutaka mabadiliko, changamoto ni kusikiliza kwa makini sauti ya Roho Mtakatifu na dhamiri nyofu, tayari kujisadaka kwa ajili ya kumfuasa Kristo, Bwana na Mwalimu. Kanisa linataka kuwasikiliza vijana, kuguswa na unyenyekevu, imani; mashaka na “madongo” yao!

Baba Mtakatifu anawataka vijana kupaaza sauti zao kwenye Jumuiya, kiasi hata cha kuwafikia viongozi wa Kanisa, ili kabla ya kufanya maamuzi muhimu ya maisha, vijana nao wapate nafasi ya kutoa maoni yao, kwani mara nyingi Mwenyezi Mungu anawapatia vijana suluhu bora zaidi. Baba Mtakatifu anahitimisha barua yake kwa vijana wa kizazi kipya kwa kuwaambia kwamba, Kanisa linataka kuwa chombo cha furaha ya vijana na anapenda kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, ili aweze kuwashika mkono na kuwaongoza kwenye chemchemi ya furaha timilifu na ukarimu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.

20/03/2018 15:29