2018-03-20 12:08:00

Maaskofu Poland wawapongeza wabunge kwa kusitisha utoaji mimba!


Baraza la Maaskofu Katoliki Poland, limewapongeza wabunge nchini humo walioamua kusimama kidete kupinga muswada wa sheria ya utoaji mimba kwa kutambua kwamba, ubaguzi na hatimaye, utoaji wa mimba kwa mtoto mwenye ulemavu ni uhalifu dhidi ya sheria na kinyume kabisa cha Katiba ya Poland inayotetea uhai wa binadamu! Pongezi hizi zimetolewa na Askofu mkuu Stanislaw Gadecki, wa Jimbo kuu la Poznan, nchini Poland. Baraza la Maaskofu Katoliki Poland linasema, maisha yanapaswa kulindwa na kudumishwa, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti ya kawaida yanapomsibu mtu! Maaskofu wanaipongeza tume ya haki msingi za binadamu nchini Poland kwa kutoa mapendekezo yanayositisha rasmi muswada wa sheria ya utoaji mimba, kwa kuheshimu utu wa binadamu pamoja na tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.

Wakleri, watawa na waamini wanaounga mkono Injili ya uhai wameshiriki kikamilifu katika majadiliano haya na matokeo yake ni Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, imeshinda. Inasikitisha kuona kwamba, utamaduni wa kifo unaanza kuinyemelea Poland hata katika masuala ya kifo laini. Maisha ya binadamu ni matakatifu tangu pale, mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida yanapomfika mtu! Juhudi za kulinda na kudumisha uhai wa binadamu zinapaswa pia kuvaliwa njuga na wahudumu katika sekta ya afya, ili kuboresha maisha ya wananchi wengi. Familia ziendelee kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.