2018-03-19 10:09:00

Papa Francisko urithi wa Padre Pio: Sala, unyenyekevu na hekima!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe 18 Machi 2018 amewashukuru kwa dhati kabisa waamini pamoja na viongozi wa Kanisa kutoka katika Majimbo ya Benevento na Manfredonia, ambako, Jumamosi, iliyopita, tarehe 17 Machi 2018 alipata bahati ya kutembelea huko. Amewashukuru pia viongozi wa serikali kwa ukarimu na upendo waliomwonesha katika hija yake ya kichungaji katika majimbo haya mawili.

Lakini kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu amewakumbuka wagonjwa wanaohudumiwa kwenye Hospitali ya San Giovanni Rotondo maarufu kama “Casa Sollievo della Sofferenza”, wazee pamoja na vijana. Anawashukuru wote waliofanikisha hija hii pamoja na kumsindikiza kwa sala na majitoleo yao. Baba Mtakatifu anasema, kwa hakika hataweza kuisahau hija hii katika maisha na utume wake! Itakumbukwa kwamba, hija hii ya kitume huko Pietrelcina na San Giovanni Rotondo ni sehemu ya maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 50 tangu Padre Pio alipofariki dunia na miaka mia moja, tangu Padre Pio alipopata Madonda Matakatifu mwilini mwake.

Baba Mtakatifu amebahatika kukutana na bahari ya watu, akatembelea na kusalimiana na wagonjwa; akakutana na kuzungumza na Wakapuchini na hatimaye, akaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu. Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu amesema, kwamba, Padre Pio alikuwa na upendo mkubwa kwa Kanisa la Kristo; alitambua dhambi na mapungufu ya watoto wa Kanisa, akajitahidi kuwa ni chombo na shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Katika maisha na utume wake, akajaribiwa katika imani, lakini akajichotea nguvu kutoka katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu.

Padre Pio alipambana na hali yake, kwa kujizatiti katika sala, usikivu na kutoa ushauri kwa watawa wenzake, ili kuwaponya kutoka katika dhambi zao kwa mafuta ya upendo na huruma ya Mungu. Ameitaka familia ya Mungu nchini Italia kujikita katika umoja, mshikamano, majadiliano, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, ili iweze kusonga mbele zaidi na kuachana na malumbano yasiyokuwa na tija wala mashiko kwa wananchi wa Italia katika ujumla wao!

Baba Mtakatifu Francisko katika kumbu kumbu ya miaka mia moja tangu Padre Pio alipobahatika kupata Madonda Matakatifu ya Yesu mwilini wake amekazia kwa namna ya pekee: umuhimu wa sala; unyenyekevu na Hekima ya Mungu inayofumbatwa katika Fumbo la Msalaba. Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, sala ni majadiliano kati ya Mwenyezi Mungu na mwamini. Ni kielelezo cha upendo na mshikamano kati ya Mungu na jirani. Kuna aina mbali mbali za sala, yaani: kuabudu, kushukuru, kutukuza, kuomba na kusifu. Sala ina nguvu ya kuganga na kuponya; inatakatifuza kazi ya mikono ya mwanadamu na kumwinua mnyonge aliyepondeka moyo. Sala inakuza na kuimarisha maisha adili na utu wema.

Baba Mtakatifu amefafanua umuhimu wa kuwa wadogo, alama ya unyenyekevu unaowawezesha waamini kutambua siri ya Mungu katika maisha yao. Kristo Yesu, ni mfano wa unyenyekevu na utii unaofumbatwa katika uhuru kamili. Unyenyekevu huu unajionesha katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake kwenye Fumbo la Pasaka, yaani: Mateso, Kifo na Ufufuko wake, kielelezo cha hali ya juu katika unyenyekevu. Kristo Yesu akaamua kubaki katika Maumbo ya Mkate na Divai, Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Mwili na Damu ya Kristo Yesu. Hiki ni kielelezo cha upendo wake wa daima, chakula na kinywaji cha maisha ya kiroho.

Baba Mtakatifu anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo na utandawazi usiojali wala kuguswa na utu, heshima, ustawi na maendeleo ya binadamu. Amewakumbusha kwamba, Hekima ya Mungu inafumbatwa katika upendo unaorutubishwa na fadhila ya imani, utii na unyenyekevu na kwamba, Fumbo la Msalaba ni ushuhuda wa hali ya juu kabisa wa Hekima ya Mungu. Kumbe, waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wamwombe Mwenyezi Mungu ili awasaidie kuambata amana na utajiri wa maisha ya kiroho na kiutu kutoka kwa Padre Pio ili kweli waweze kuwa ni watu wa sala, kwa kujisadaka katika utume kwa wagonjwa, daima wakikimbilia kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao katika Sakramenti ya Upatanisho, mambo mazito yaliyopewa kipaumbele cha pekee na Padre Pio wa Pietrelcina.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.