2018-03-19 13:50:00

Papa Francisko awataka vijana kushirikisha yale yaliyomo ndani mwao!


Utangulizi wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu wa ajili ya Vijana kwa mwaka 2018, umeanza kutimua vumbi mjini Vatican kwa wajumbe wa vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, Jumatatu, tarehe 19 Machi 2018 kukutana na Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu hapa mjini Vatican. Baba Mtakatifu anawataka vijana kuzungumza kwa kujiamini na kwa ujasiri pasi na woga; wakuze pia ndani mwao sanaa ya kusikiliza kwa makini kwani kila mtu anayo haki ya kuzungumza na kusikilizwa mawazo yake kwa unyenyekevu mkuu.

Baba Mtakatifu anasema, vijana ni changamoto ya maisha na utume wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo! Kanisa limedhamiria kuwasindikiza vijana kwa uvumilivu, weledi na upendo mkuu katika safari ya mang’amuzi ya miito yao, ili waweze kuipokea kwa upendo na hatimaye, kupata utimilifu wa maisha! Vijana wanapaswa kutambua kwamba, wao ni jeuri na chachu inayoweza kupyaisha uso na moyo wa Kanisa.Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza vijana wote waliokuwa wamejiunga na wenzao katika udinduzi wa utangulizi wa maadhimisho ya Sinodi ya Vijana kwa mwaka 2018. Hawa ni vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wenye tamaduni na dini zao, wanaopania kushirikisha mang’amuzi yao katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu ili kweli Kanisa liweze kuibua mbinu mkakati wa maisha na shughuli za kichungaji kwa vijana wa kizazi kipya. Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu inaendelea kuzama zaidi na zaidi katika ugunduzi kwa kutumia njia za mawasiliano ya jamii ili kuweza kuwafikia vijana wengi, ambao ndio walengwa wakuu!

Baba Mtakatifu anasema, Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana itakayoadhimishwa mwezi Oktoba, 2018 ni muda muafaka wa kufanya mang’amuzi ya miito mbali mbali kama inavyofafanuliwa kwenye Maandiko Matakatifu. Vijana wana ujasiri wa kuzungumza ukweli hata kama bado wanaweza kuelemewa na mapungufu katika maisha na ujana wao! Vijana wanao ujasiri wa kusikiliza, kufurahia na hata wakati mwingine kutoa machozi. Vijana wanatakiwa kutoa maoni yao pasi na woga kwani wao ni changamoto kubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Ni watu wenye nyuso, historia, matatizo, fursa na changamoto zinazowaandama.

Vijana wanapaswa kusikilizwa, kuthaminiwa na kusaidiwa kufanya maamuzi mazito katika maisha yao, kwani wakati mwingine, wamekuwa wakisukumizwa pembezoni mwa maisha na vipaumbele vya jamii. Kuna idadi kubwa ya vijana ambao hawana fursa za ajira na matokeo yake ni vijana kukosa dira na mwelekeo wa maisha, kiasi cha kujikuta wakiteseka kwa: ugonjwa sonona, matumizi haramu ya dawa za kulevya, ulevi wa kupindukia, kujinyonga; biashara ya ngono, mauaji; matokeo yake ni dhambi jamii.

Baba Mtakatifu anawataka vijana kutaja mambo yanayowatumbukiza katika utamaduni wa kifo na utumwa mamboleo, ili kujenga jamii inayosimikwa katika ukweli na uwazi mintarafu mpango wa Mungu katika maisha yao. Vijana wanapaswa kutambua, kupokea wito wao kwa moyo wa upendo na hatimaye, kupata utimilifu wa maisha kwani Mungu anawapenda na Kanisa lina waamini vijana! Vijana watambue kile wanachotafuta katika hija ya maisha yao ya kila siku, ili kuwashirikisha wengine furaha ya kukutana na Kristo Yesu, ili kuweza kupata uzima wa milele.

Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana ni mwaliko wa kuwasikiliza, kuwa karibu na kuwaonesha ushuhuda wenye mvuto na mashiko, tayari kugundua utajiri unaofumbatwa katika maisha yao, ili uweze kutumika kwa ajili ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Vijana wanataka kusikilizwa kwa makini na sasa Kanisa limeanza mchakato wa kujenga utamaduni wa kuwasikiliza na kuwasindikiza vijana ili waweze kukabiliana na changamoto za maisha pasi na kukata wala kukatishwa tamaa. Kanisa linataka kuwakutanisha na kuwapeleka vijana kwa Kristo Yesu.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican waliwataka vijana kuondokana na ubinafsi, kwa kuwa na ujasiri ili kujenga ulimwengu ulio bora zaidi sanjari na kuendelea kuupyaisha uso na moyo wa Kanisa; kwa kuwa waaminifu kwa maisha na utume wa Kanisa, ili kuishi, kutangaza na kushuhudia Injili. Baba Mtakatifu anawataka vijana kushirikiana na kushikamana na Mama Kanisa ili kuleta mabadiliko katika maisha, imani, matumaini na mapendo, tayari kupiga moyo konde na kusonga mbele, hata kama ni kuhatarisha maisha!

Vijana ni chachu ya upya wa maisha na utume wa Kanisa unaolisukuma kutoka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa kujikita katika mambo msingi ya maisha! Vijana wanapaswa kushinda woga na wasi wasi katika maisha, vinginevyo, watazeeka hata kabla ya wakati wao! Kanisa linawahitaji vijana ambao ni mawe hai, ili kupyaisha uso, maisha na utume wa Kanisa, daima kwa kuzingatia Mapokea ya Kanisa yanayojikita katika kipaji cha ugunduzi. Ujenzi wa utamaduni mpya miongoni mwa vijana hauna budi kuwa na mizizi kutoka katika tunu msingi za maisha ya kijamii kwa kuthamini Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Ikumbukwe kwamba, wazee wanazo ndoto, lakini vijana wana unabii. Kanisa linahitaji vijana wenye sauti ya kinabii, wanaowathamini wazee ili kujenga utamaduni wa majadiliano. Mwishoni, Baba Mtakatifu anasema, utangulizi wa maadhimisho ya Sinodi za Vijana ni muda wa kuzungumza katika ukweli na uwazi; kwa kutambua kwamba, vijana ndio wahusika wakuu katika Sinodi na kwamba, mchango wao utapewa uzito wa pekee, katika Hati ya Kutendea Kazi, “Instrumentum Laboris”. Baba Mtakatifu pia amesikiliza shuhuda kutoka kwa vijana watano kutoka Oceania, Ulaya, Asia, Amerika na Bara la Afrika limewakilishwa na Tendai Karombo, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Katoliki nchini Zimbabwe.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.