2018-03-19 07:59:00

Papa Francisko awaandikia wananchi wa Argentina barua ya shukrani!


Baba Mtakatifu Francisko tarehe 19 Machi 2018, Kanisa linapoadhimisha Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, Mume wake Bikira Maria, anafanya kumbu kumbu ya miaka mitano tangu alipoanza rasmi kuliongoza Kanisa la Kristo. Baba Mtakatifu katika barua aliyowaandikia wajumbe wa Shirikisho la Wafanyakazi na Uchumi nchini Argentina: anawashukuru, anawaomba msamaha na sala katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu anasema, anaipenda Argentina na watu wake; anawashukuru kwa salam na matashi mema, wakati huu, anapoadhimisha kumbu kumbu ya miaka mitano tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa. Anawashukuru viongozi mbali mbali wa kidini, kisiasa na kiserikali ambao wanamkumbuka na kumsindikiza kwa sala na matashi mema.

Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, kila siku ya maisha yake, anaikumbuka na kuiombea Argentina na watu wake. Anaomba msamaha kwa baadhi ya matendo yake, ingawa Mwenyezi Mungu amemdhaminisha utume huu na kwamba, ataendelea kumtegemeza, kwani licha ya majukumu yote haya, lakini bado anaelemewa na udhaifu wake wa kibinadamu! Anawaalika wananchi wa Argentina kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wake kwa kufurahia yale mambo mazuri anayotenda, kwa kutambua kwamba, wao ni watu wake, waliomlea na kumkuza hadi kufikia jinsi alivyo, na sasa wamemtoa sadaka kwa ajili ya utume kwa Kanisa la Kiulimwengu.

Baba Mtakatifu anawakumbusha kwamba, Mwenyezi Mungu amemwita na kumchagua mmoja kati yao ili kuwa ni mjumbe wa imani, huruma na udugu kwa watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Anawahimiza wananchi wa Argentina kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wema na uzuri, kwa kusimama kidete kulinda Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo pamoja na kudumisha haki, amani na udugu kama sehemu ya maboresho ya ulimwengu huu, ili kweli uweze kujizatiti katika kuwahudumia maskini na wanyonge, wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Baba Mtakatifu anahitimisha barua yake kwa kuwaomba wananchi wa Argentina kusali na kumwombea mema katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro na ndugu yao wa damu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.