2018-03-19 14:34:00

Kardinali Baldisseri asema, Sinodi ni kwa ajili pamoja na vijana!


Vijana zaidi ya mia tatu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wako mjini Vatican kushiriki katika maadhimisho ya utangulizi wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana. Mama Kanisa anataka kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mradi wa maisha ya vijana katika maisha na utume wa Kanisa zima. Hii ni Sinodi ambayo Baba Mtakatifu Francisko anataka iwe kwa ajili pamoja na vijana, ili kweli waweze kujisikia kuwa ni wahusika wakuu, tayari kushirikisha yale yanayofumbatwa katika sakafu ya mioyo na maisha yao ya ujana.

Hii inatokana na ukweli kwamba, kila kijana analo jambo ambalo anaweza kuwashirikisha vijana wenzake, wakleri, watawa na kwa namna ya pekee, Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Vatican wakati wa ufunguzi wa utangulizi wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana. Hii ni hatua muhimu sana itakayowawezesha vijana ambao wanashiriki moja kwa moja katika maadhimisho haya hapa mjini Roma, na wale ambao wako nje, lakini wanafuatilia tukio hili kwa njia ya mitandao ya kijamii. Vijana wanaendelea kujadiliana na kushirikishana uzoefu na mang’amuzi yao, ili hatimaye, kuchangia mawazo na mapendekezo yatakayotumiwa kuandaa “Hati ya Kutendea Kazi”.

Kardinali Baldisseri kwa niaba ya washiriki wote amemtakia Baba Mtakatifu Francisko heri na matashi mema, Mama Kanisa anapoadhimisha Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, Mume wake Bikira Maria, sanjari na miaka mitano, tangu alipoanza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Katika kipindi cha miaka mitano, Baba Mtakatifu Francisko ameonesha upendeleo wa pekee kwa maisha na utume wa vijana kwa kuwaalika kuchangia katika maisha na utume wa Kanisa hata katika shida na mahangaiko yao. Wawakilishi wa vijana hawa ni wale walioteuliwa na Mabaraza ya Maaskofu kutoka katika medani mbali mbali za maisha pamoja na wawakilishi wa dini na madhehebu mbali mbali ya Kikristo!

Lengo la maadhimisho haya ni kulisaidia Kanisa kujenga utamaduni na sanaa ya kuwasikiliza vijana na hati itakayotolewa katika maadhimisho haya itaingizwa kwenye Hati ya Kutendea Kazi, itakayotumiwa na Mababa wa Sinodi. Mapendekezo haya yatawasilishwa kwa Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili ya Matawi, wakati Mama Kanisa atakapokuwa anaingia kwenye Juma Kuu kwa kukumbuka, mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Haya ni matarajio, imani na matumaini ya vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, watakayowasilisha kwa Mababa wa Sinodi, mwezi Oktoba, 2018.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News








All the contents on this site are copyrighted ©.