2018-03-17 08:56:00

Kifo cha Kristo ni kielelezo cha utii, upatanisho na uhai mpya!


Ndugu msomaji na msikilizaji wa Vatican News, karibu katika tafakari ya Neno la Mungu katika Dominika ya tano ya Kwaresima. Ni dominika inayotusogeza karibu kabisa na juma la mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo. Na kuanzia leo kwa kufuata desturi ya kale tunafunika misalaba na sanamu kutuonesha kuwa tunaingia hatua maalumu katika kipindi hiki cha Kwaresima, hatua ambapo tunapotambua kuwa Kristo ameingia katika mateso hayo makali kwa sababu ya dhambi zetu, tunakosa uthubutu wa kumuangalia moja moja. Katika dominika hii tunaalikwa tuzidi kuingia ndani yetu kuitayarisha mioyo yetu kwa ajili ya kuyaadhimisha mafumbo makuu ya imani na wokovu wetu yaani mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo.

Masomo kwa kifupi: Somo la kwanza (Yer. 31:31-34). Nabii Yeremia alihubiri katika kipindi ambacho Israeli na mataifa ya jirani hawakuwa katika kipindi cha utulivu kisiasa. Tawala ziliingia katika mapigano kutafuta ukuu na kupanua makoloni ya kutawala. Katika Israeli kilikuwa pia ni kipindi ambacho ambapo waisraeli walilegea sana katika kulishika Agano lao na Mungu. Mahubiri ya toba ya Nabii Yeremia hayakupokeleka (7:1-8:3), yeye mwenyewe alipingwa sana (11:18-23) na hata kuteswa. Aliisikitikia na kuililia sana hali hii kwamba waisraeli hawalitii tena Agano na ndiyo maana nabii Yeremia huitwa pia “nabii anayelia”. Ni katika mazingira haya anatoa unabii kuwa siku zinakuja ambapo Mungu atafunga nao Agano Jipya. Agano hili hataliandika kwenye mbao kama ilivyokuwa awali bali ataliandika katika moyo wa kila mmoja. Atafanya hivi ili kila mmoja ndani yake mwenyewe awe na uwezo wa kulijua Agano na Mungu na hivi aweze kulitii na kulishika. Ni kwa kushika Agano wataendelea kuwa watu wa Mungu na Mungu ataendelea kuwa Mungu wao.

Somo la pili (Ebr. 5:7-9). Huu ni waraka ambao kama mojawapo ya dhamira zake kuu unakazia juu ya ukuhani wa Kristo na kazi yake ya ukombozi kwa mwanadamu. Kazi ya kwanza ya kuhani ni kusali - kwa ajili yake na kwa ajili ya wale aliokabidhiwa. Na somo letu hili linaonesha kuwa Kristo kama kuhani Mkuu alisali sana. Na katika kusali kwake huko aliweza kusikilizwa kwa sababu kama binadamu alimcha Mungu na alimtii. Na utii huu Kristo alijifunza kwa mateso; yaani alitii kuyapokea mateso kama mapenzi ya Mungu kwa ajili ya wokovu wa wanadamu na ulimwengu mzima na zaidi ya hayo aliendelea kutii hata katikati ya mateso hayo. Kumbe Kristo kuhani mkuu ni kuhani mchaji wa Mungu na ni kuhani mtii tangu mwanzo hadi mwisho.

Somo la Injili (Yoh. 12:20-33). Kristo anatambulisha kuwa saa yake imefika, saa ya kutukuzwa kwake Mwana wa Adamu yaani saa yake ya kuingia katika mateso na kifo kwa ajili ya kuukomboa ulimwengu. Yesu anatamka haya mara tu baada ya kusikia kuwa kuna wayunani wanaotafuta kumuona. Ni kana kwamba kitendo cha wayunani, watu waliokuwa wanakaa nje ya uyahudi, kuwa wameshasikia habari za Yesu kiliashiria tayari kusambaa kwa habari zake na pia kiliashiria utimilifu wa wakati wake “saa yake”. Kisha akaanza kutoa mafundisho ya mwisho mwisho kabla ya kuingia katika hiyo saa. Katika mafundisho haya anaeleza kuwa kifo chake ni lazima ili ulimwengu ukombolewe kama vile mbegu inavyokufa ardhini ili baadaye kutoa mazao mengi. Ni kifo kinachoanzia awamu mpya au agano jipya ambapo wale tu wanaomtumikia na kumfuata ndio watakuwa sehemu yake.

Tafakari: Katika dominika hii inayotusogeza karibu kabisa na Juma Kuu Maandiko Matakatifu yanatualika tutafakari kwa undani kidogo juu ya kifo cha Kristo na thamani yake kwetu wakristo na kwa ulimwengu mzima. Na hapa tunaweza kuona mambo matatu yanayofafanua maana na thamani ya kifo cha Kristo katika masomo ya leo: Kristo amepokea mateso na kifo chake kwa utii. Kama vile tangu mwanzo Neno wa Mungu alivyomtii Baba akatwaa mwili na kushuka ulimwenguni, ndivyo alivyomtii Baba kukipokea kikombe cha mateso na kifo. Ni utii wenye uhuru kamili katika kuyapokea mapenzi ya Baba. Ndiyo maana katika kifo chake yeye sio tu mhanga kama wanyama waliokuwa wanatolewa sadaka bali yeye mwenyewe alijitoa sadaka hiyo. Ndiye kuhani mkuu atoaye sadaka, ndiye altare inapotolewa sadaka na yeye mwenyewe ndiye sadaka inayotolewa.

Kifo cha Kristo ni kifo kinacholeta upatanisho. Ni kwa njia ya kifo cha Kristo Mungu ameamua kuunda Agano Jipya na watu wake, Agano ambalo aliliahidi tangu mwanzo kama ulivyokuwa unabii wa Nabii Yeremia. Agano ambalo halitaandikwa katika mbao bali katika moyo wa kila mwanadamu. Ni Agano linaloonesha upendo mkubwa wa Mungu kwa mwanadamu, upendo ambao Mungu hataki mtu apotee na hata pale anapopotea Yeye mwenyewe anamwinamia mwanadamu ili kuinua hadhi yake. Ni agano lililokuwa likisubiri kufika kwa “Saa” yake, ndiyo saa ya kutukuzwa mwana wa Adamu, saa ya kifo chake.

Kifo cha Kristo kinaleta uhai. Yeye mwenyewe anakifananisha na mbegu inayopandwa ardhini. Kwanza inakufa lakini baadaye inatoa mazao mengi. Ndivyo na kifo chake Kristo kinavyorudisha uhai katika ulimwengu. Kumbe uhai wetu kama wakristo unatokana na kifo cha Kristo na kadiri ambavyo siku kwa siku tunayasimika maisha yetu katika fumbo la kifo chake. Vipengele hivi vitatu vinavyofafanua thamani ya kifo cha Kristo vinatupatia pia changamoto ya kuyaongoza maisha yetu katika utii kwa sauti na mapenzi ya Mungu maishani mwetu; kudumu tumepatana na Mungu na jirani yetu na kuyasimika maisha yetu katika fumbo la kifo cha Kristo. Hiki ndicho kifo cha Kristo ambacho kama anavyotufundisha mtume Paulo kwa wayahudi ni kikwazo, kwa wayunani ni upuuzi bali kwetu ni nguvu ya Mungu na ni hekima ya Mungu (Rej. 1Kor. 1:24).

Bikira Maria mama wa tumaini jema, atuombee.

Na Padre William Bahitwa.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.