2018-03-16 08:22:00

Bara la Afrika na changamoto ya teknolojia ya mawasiliano ya jamii!


Shirikisho la Mtandao wa Vituo vya Radio Barani Afrika, kuanzia tarehe 12 hadi 16 Machi 2018 limekuwa likiadhimisha mkutano wake mkuu wa kumi na moja huko Kigali, nchini Rwanda. Tangu tarehe 12-13, wajumbe wamejikita zaidi kuhusu mabadiliko ya teknolojia kutoka katika ulimwengu wa “analogia” kuingia katika ulimwengu wa “digitale”. Tangu tarehe 15-16 Machi 2018, wajumbe wamedadavua kuhusu “Luninga: wakimbizi na wahamiaji kutoka Barani Afrika. Padre Bernardo Suate amemwakilisha Monsinyo Dario Edoardo Viganò, Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Mawasiliano ya Vatican katika mkutano huu na kusoma ujumbe aliowaandikia washiriki wa mkutano huu, kwa kukazia kuhusu: huduma mpya ya mawasiliano kwa njia ya satelite kwa Bara la Afrika, majibu muafaka ya changamoto za mawasiliano ya jamii Barani Afrika. Amekazia umuhimu wa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu kama kiini cha mawasiliano ya jamii katika huduma ya ukweli na amani kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wa Siku ya 52 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa mwaka 2018 unaoongozwa na kauli mbiu “…kweli itawaweka huru: Habari za kughushi na uandishi wa habari wa amani.”

Monsinyo Dario Edoardo Viganò, katika ujumbe huu anafafanua kwamba, Baba Mtakatifu Francisko katika mchakato mzima wa mabadiliko ya Sekretarieti kuu ya Vatican, ameonesha jicho la pekee kwa Bara la Afrika. Kanisa linatambua na kuthamini mchango mkubwa unaoendelea kutolewa na Vatican News katika masafa mafupi mintarafu mgawanyo wa lugha katika maeneo husika. Matangazo kwa lugha ya Kiarabu kutoka Vatican yanarushwa moja kwa moja kwenye eneo la Afrika ya Kaskazini na huko Mashariki ya Kati. Vipindi vingine kama vile vya muziki, vimesitishwa kwa muda kutokana na kupungua kwa ubora wa matangazo yanayorushwa kwa njia ya Masafa Mafupi na badala yake, vipindi cha Liturujia vimepewa kipaumbele cha kwanza ikilinganishwa na vipindi vya habari!

Kuanzia Januari mwaka 2018, Bara la Afrika limeanza kupata huduma mpya ya matangazo kwa njia ya Satelite inayorusha moja kwa moja matangazo kwa njia ya sauti, maarufu kama “Audio Stream” na hapo vituo mbali mbali vya Radio kutoka Barani Afrika, vinaweza kupata huduma ya mawasiliano moja kwa moja kutoka Vatican kwa kutumia programu “Vatican Media Radio Feed Africa”. Hii ni huduma ya mawasiliano kwa njia ya televisheni inayotolewa katika lugha ya: Kiingereza, Kifaransa, Kireno na Kihispania kwa sasa. Lengo ni kuhabarisha zaidi. Kinachozingatiwa hapa ni maudhui. Kuna mpango mkakati wa kugawa vitendea kazi 200 vitakavyowezesha Vituo vya Radio kupata matangazo moja kwa moja kutoka Vatican kwa njia ya Satelite na internet. Huu ni mradi unaofanikishwa na Sekretarieti ya Mawasiliano ya Vatican kwa kushirikiana na “Signis” pamoja na Kituo cha SatADSL ili kuwezesha mchakato wa ushirikiano wa mawasiliano kwa njia ya sauti. Sekretarieti ya Mawasiliano ya Vatican itakuwa inatuma program ambazo zinaweza kutumiwa pia na Radio mahalia kwa njia ya Masafa ya FM. Radio hizi pia zitakuwa na uwezo wa kushirikiana mnoja kwa moja na Sekretarieti ya Mawasiliano ya Vatican, ili sauti ya kinabii inayotolewa na Makanisa mahalia, iweze kusikika kwa watu wengi zaidi.

Monsinyo Dario Edoardo Viganò anaendelea kudadavua kwa kusema kwamba, kuna changamoto kubwa ya maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii inayopaswa kuvaliwa njuga na familia ya Mungu Barani Afrika kwa kutoa majibu muafaka na kuendelea kusoma alama za nyakati! Shirikisho la Mtandao wa Radio Katoliki Burkina Faso limekuwa na mafanikio makubwa katika mchakato wa matumizi ya maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano, daima kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Bara la Afrika linahamasishwa kuendelea kujizatiti ili kuhakikisha kwamba, linakuwa ni mdau wa karibu sana na Sekretarieti ya Mawasiliano ya Vatican. Hii ni changamoto pevu, inayohitaji rasilimali fedha na watu walioandaliwa barabara, kwa kuwekeza zaidi katika mchakato wa maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii. Rasilimali watu, ifundwe vyema Kikanisa, kitaalimungu na kisayansi, ili kuwasilisha vyema mchango wa Mama Kanisa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi: kiroho na kimwili anasema Monsinyo Dario Edoardo Viganò.

Utu, heshima, ustawi wa wengi ni kiini cha mawasiliano endelevu ya jamii, ili kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana na kushirikiana; daima watendaji wakuu wa vyombo vya mawasiliano ya jamii wakiwajibika vyema. Waandishi wa habari wanapaswa kuwa makini kwa kuzingatia: nidhamu, uadilifu, weledi na uwajibikaji wanapotekeleza dhamana hii nyeti, ili watu wasilishwe kwa habari za kughushi ambazo zimekuwa zinazagaa sana kiasi cha kuhatarisha mafungamano ya kijamii. Kwa njia hii, mawasiliano yatasimikwa katika ukweli kwa ajili ya ustawi, ustawi na maendeleo ya wengi. Kinachohitajika zaidi ni mawasiliano katika ukweli na ujenzi wa Amani duniani, daima binadamu akipewa kipaumbele cha kwanza ili kudumisha uhuru dhidi ya chuki na uhasama; kwa kujenga madaraja ya watu kukutana na kusikilizana; pamoja na kujadiliana katika uwazi, ili ukweli uweze kung’aa na kutawala katika nyoyo za watu, ili waweze kuwa huru kweli kweli!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.