2018-03-15 10:08:00

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya: Ni muda wa uponyaji na upatanisho


Mtume Paulo katika Waraka wake wa Warumi anasema kwamba, kwa maana ikiwa tulipokuwa adui tulipatanishwa na Mungu kwa mauti ya Mwana wake, zaidi sana baada ya kupatanishwa tukaokolewa katika uzima wake. Huu ni ujumbe mzito kutoka kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya katika kipindi hiki cha Kwaresima, ambamo waamini wanaalikwa kuchunguza dhamiri zao, kutubu na kumwongokea Mungu, ili kuanza hija ya maisha mapya. Maaskofu Katoliki nchini Kenya, wanapenda kutambua na kuthamini sana mwelekeo mpya ambao umeoneshwa na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya pamoja na Bwana Raila Odinga, kiongozi mkuu wa upinzani, kwa kukutana, kujadiliana na hatimaye, kutoa tamko la pamoja linalopania kuanzisha mchakato wa umoja na upatanisho wa kitaifa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na hivyo kusonga mbele kwa Imani na matumaini.

Maaskofu wanakiri kwamba, kampeni na hatimaye, uchaguzi mkuu uliohitimishwa hivi karibuni nchini humo, umeacha mpasuko mkubwa miongoni mwa familia ya Mungu. Tukio hili ni muhimu sana katika mchakato mzima wa kutafuta suluhu ya matatizo na changamoto ambazo zimekuwa zikiwaandama wananchi wa Kenya, mara kwa mara wakati na baada ya chaguzi. Maaskofu wanasema, huu uwe ni mwanzo kwa familia ya Mungu nchini Kenya kujizatiti zaidi katika ujenzi wa jamii inayosimikwa katika misingi ya haki, amani, demokrasia na fursa ya maendeleo endelevu kwa kila mwananchi.

Hiki ni kielelezo kwamba, majadiliano katika ukweli na uwazi ni jambo linalowezekana kabisa kama njia ya kutafuta ufumbuzi wa matatizo na changamoto zinazowakabili wananchi wa Kenya. Hii ni fursa kwa wananchi wote kujikita katika mchakato wa umoja, upatanisho na ushirikiano kwa kuangalia kwa macho makavu mustakabali wa maisha ya wananchi wa Kenya katika ujumla wao! Maaskofu wanahimiza kwamba, mchakato huu, uwe ni shirikishi kwa kuanzia katika maisha ya wananchi wa kawaida kama ambavyo, kampeni ya Kwaresima kwa mwaka 2018 inavyohimiza.

Kanisa kwa upande wake, linawataka waamini kushiriki kikamilifu katika mchakato huu, wanapokutanika kusali kwenye Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo. Maaskofu wanavihamasisha vyama vyote vya upinzani kushiriki katika mchakato huu kwa kujadiliana na serikali katika ukweli na uwazi, ili kukuza na kudumisha demokrasia ya kweli inayopania kutoa huduma makini kwa wananchi. Katika mazingira kama haya, daima utawala wa sharia unapaswa kuzingatiwa na wote. Maaskofu wanakaza kusema, ukosefu wa usalama wa raia na mali zao ni kati ya mambo yanayowatis shaka sana kwa wakati huu.

Ikumbukwe kwamba, serikali inayo dhamana ya kulinda maisha ya raia na mali zao. Matukio ya uvunjifu wa amani huko Mlima Elgon, baadhi ya sehemu za Kaskazini mwa Kenya na Mikoa iliyoko kwenye mwambao wa Bahari ya Hindi. Mwishoni, Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linaitaka familia ya Mungu nchini humo kuendelea kujikita katika mchakato wa haki, amani, upatanisho na maridhiano ya kitaifa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.


 








All the contents on this site are copyrighted ©.