Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Maisha Ya Kanisa Afrika

Askofu Mkuu Cristobal: Nataka kuwa daraja na shuhuda wa Injili!

Askofu mkuu Cristobal Lopez Romero anasema katika maisha yake ya kuongoza, kufundisha na kutakatifuza watu wa Mungu anapenda kuwa ni daraja ya majadiliano na shuhuda wa Injili ya upendo na mshikamano. - AP

15/03/2018 10:26

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanafundisha kwamba, Uaskofu ni utimilifu wa Sakramenti ya Daraja Takatifu, kielelezo cha Ukuhani mkuu cha huduma takatifu. Askofu anapewa dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu na hivyo, kushika nafasi ya Kristo mwenyewe, aliye: mwalimu, mchungaji na kuhani na kwamba, wanatenda kazi hii katika nafsi yake. Kwa njia ya karama za Roho Mtakatifu, Maaskofu ndio wanaofanywa kuwa walimu kweli na halisi wa imani, makuhani na wachungaji.

Kila Askofu, kama wakili wa Kristo, ana kazi ya kichungaji ya Kanisa mahalia ambalo ameaminishwa, lakini papo hapo, kiurika, pamoja na ndugu zake katika uaskofu, anajishughulisha kwa ajili ya Makanisa yote. Askofu kwa namna inayoonekana anamwakilisha Kristo Yesu, Mchungaji Mwema, na Kichwa cha Fumbo la Mwili wake, yaani Kanisa. Mheshimiwa Padre Cristobal Lopez Romero, S.D.B. aliyeteuliwa hivi karibuni kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Rabat, tarehe 10 Machi 2018 amewekwa wakfu kuwa Askofu mkuu. Hadi kuteuliwa kwake, Askofu mkuu Lopez Romero alikuwa ni Mkuu wa Kanda ya Wasalesiani wa Maria Auxialiadora, nchini Hispania. Katika hotuba yake ya shukrani, Askofu mkuu Cristobal Lopez Romero amesema, anapenda kuwa ni chombo na daraja linalowaunganisha: Wakristo na Waislam; maskini na matajiri; vijana na wazee na kwamba, angependa kujikita zaidi katika huduma ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Anasema, angependa endelee kuitwa Baba Cristobal, ili kumkumbusha dhamana na wajibu wake kama shuhuda na chombo cha Injili ya upendo inayofumbatwa katika unyenyekevu!

Kardinali Juan Josè Omella Omella, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Barcelona, ndiye aliyemweka wakfu Askofu mkuu Cristobal Lopez Romero kwa kumkumbusha kwamba, amefungua ukurasa mpya wa maisha na utume wa Jimbo kuu la Rabat, Morocco. Hii ni changamoto ya kujenga na kudumisha sanaa na utamaduni wa kusikiliza kwa maskini na kujibu kilio na mateso ya watu wa Mungu kwa njia ya tunu msingi za maisha ya Kiinjili. Askofu mkuu ametakiwa kukuza na kudumisha ari na mwamko wa kimisionari, kwa kuwa ni kiongozi na mchungaji wa wate; mchungaji anayejizatiti katika mchakato wa majadiliano ya kidini, ili kudumisha haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mungu.

Itakumbukwa kwamba, alizaliwa tarehe 19 Mei 1952 huko Hispania. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kitawa, akaweka nadhiri zake za daima tarehe 2 Agosti 1974 na kupewa Daraja takatifu ya Upadre tarehe 19 Mei 1979. Tangu wakati huo, katika maisha na utume wake kama Padre amekuwa: mhudumu wa wakimbizi na wahamiaji; amejihusisha na utume kwa vijana; Paroko na Mkurugenzi mkuu wa Jalida la Wasalesiani huko Asunciòn. Padre Mkuu wa Kanda na Mkuu wa Jumuiya. Mara kadhaa amekuwa pia katika malezi na Jaalim kwenye vyuo vikuu kadhaa ndani na nje ya Morocco. Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni ameridhia ombi la kung’atuka kutoka madarakani lililowasilishwa kwake na Askofu mkuu Vincent Landel wa Jimbo kuu la Rabat, Morocco.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

15/03/2018 10:26