Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Hotuba

Papa Francisko: Mkazo: Huruma, Maskini, Pembezoni, Kutoka & Ibilisi

Papa Francisko katika kipindi cha miaka mitano ya maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro amekazia zaidi kuhusu: Huruma ya Mungu, Maskini kama amana na utajiri wa Kanisa, Umuhimu wa kutoka kwenda kuinjilishaji, Pembezoni mwa Jamii na uwepo wa Ibilisi, shetani!

14/03/2018 08:20

Baba Mtakatifu Francisko, mwezi Machi 2018 anaadhimisha kumbu kumbu ya miaka mitano tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki na kuanza utume wake rasmi, tarehe 19 machi 2013 kwa kujikita katika mambo makuu matatu: amani, maskini na mazingira. Hii ikawa kama dira na mwongozo wa maisha na utume wake chini ya ulinzi na tunza ya Mtakatifu Yosefu, Baba mlishi wa Kristo Yesu na Mtakatifu Francisko wa Assisi, aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya maskini, amani katika Nchi Takatifu na Utunzaji bora wa mazingira, chimbuko la Waraka wa kitume wa “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”.

Katika kipindi cha miaka mitano ya maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, Baba Mtakatifu Francisko amekazaia sana juu ya “huruma ya Mungu” katika maisha na utume wa Kanisa, mwaliko na changamoto kwa Mama Kanisa kulitafakari tena “Fumbo la Huruma ya Mungu kama chemchemi ya furaha, utulivu wa ndani na amani na kwamba, huruma ni sharti muhimu sana la wokovu na ufunuo wa Fumbo la Utatu Mtakatifu. Hili ndilo chimbuko la maadhimisho ya Mwaka wa Huruma ya Mungu kama sehemu ya kumbu kumbu endelevu ya kufunga maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Itakumbukwa kwamba, Ibada ya huruma ya Mungu imepata msukumo wa pekee kutoka kwa Mtakatifu Faustina Kowalska na kuvaliwa njuga na Mtakatifu Yohane Paulo II aliyethubutu hata kuanzisha Jumapili ya Huruma ya Mungu, changamoto na mwaliko kwa waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu Francisko akataka waamini kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo cha imani tendaji, kwani huruma ya Mungu inawaambata na kuwakumbatia wote pasi na ubaguzi! Kama mwendelezo wa ushuhuda huu, akaanzisha Ijumaa ya huruma ya Mungu. Hii ni siku ambayo, Baba Mtakatifu anapopata nafasi, anaitumia katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Baba Mtakatifu Francisko katika utume anakaza kusema “Maskini ni amana na utajiri wa Kanisa”: Hawa ni walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu inayopaswa kutangazwa na kushuhudiwa kwa watu wa Mataifa. Mtakatifu Francisko akawa ni mfano wake wa kuigwa katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa kutambua wazi kwamba, si rahisi sana kuiga mfano wa maisha ya Mtakatifu Francisko ambaye alichezea sana ujana wake, lakini alipokutana na Uso wa huruma ya Mungu, akatubu, akaongoka na kujisadaka kwa ajili ya kulipyaisha tena Kanisa la Mungu.

Tangu siku ile ya kwanza kuchaguliwa kwake, alikumbushwa na Kardinali Claudio Hummes kwamba, asiwasahau maskini katika utume wake! Hawa ni maskini wa hali, kipato, tunu msingi za maadili na utu wema! Ni wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi ugenini hata kiasi cha kuhatarisha maisha yao! Ni waathirika wa biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo unaonyanyasa na kudhalilisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Maskini ni watoto wanaodhalilishwa kijinsia, wanaotumikishwa kwenye kazi za suluba na hata kubebeshwa mtutu wa bunduki, kama chambo cha vita! Maskini ni wafungwa magerezani wanaotamani kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Magereza yawe ni nafasi ya kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuandika tena kurasa  mpya zinazofumbatwa kwenye Injili ya furaha na matumaini!

Kutokana na changamoto ya umaskini Baba Mtakatifu Francisko akaamua kwamba, makazi yake hadi wakati huu yawe kwenye Nyumba ya wageni ya Mtakatifu Martha, iliyoko mjini Vatican na wala si Jumba la Kipapa. Anasema, hii ni nafasi ya kujenga madaraja ya kukutana na watu, ili kuwashirikisha Injili ya furaha inayobubujika kutoka katika undani wa maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro! Hii ni changamoto kwa Mama Kanisa kujikita katika mchakato wa kupambana na umaskini wa hali na kipato; mmong'onyoko wa maadili na utu wema; baa la njaa, ujinga na maradhi kwa kuwa ni chombo na shuhuda wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, rushwa na ufisadi!

Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, anaendelea kutoa kipaumbele cha kwanza kwa watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii na mambo msingi ya maisha kutokana na hali zao mbali mbali, ili waweze kuonjeshwa mambo msingi katika maisha na utume wa Kanisa. Itakumbukwa kwamba, safari yake ya kwanza kutoka mjini Vatican kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, ilikuwa ni kwenda kwenye Kisiwa cha Lampedusa, Kusini mwa Italia, mahali ambapo wahamiaji na wakimbizi wanaoweza “kupiga chenga mauti” wanapatiwa hifadhi ya muda! Bahari ya Mediterrania anasema Baba Mtakatifu, imekuwa ni kaburi lisilo kuwa na alama kwa wakimbizi na wahamiaji wanaoteseka kutoka na vita, athari za mabadiliko ya tabianchi, biashara haramu ya binadamu pamoja na utumwa mamboleo. Hata ndani ya Kanisa, kuna watu wanaosukumizwa pembezoni mwa maisha na utume wa Kanisa. Hawa ni wakleri, watawa na waamini walei wanaopaswa kuheshimiwa, kuthaminiwa na kusikilizwa na kushirikishwa katika maisha na utume wa Kanisa!

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili”: Muhtasari wa sera na mbinu mkakati wa maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Anakazia ari na moyo wa kimisionari kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Huu ni mwaliko kwa Kanisa kutoka huko Sakristia na kuanza kwenda kuwatafuta hasa wale ambao wamesahau mlango wa Kanisa; waamini ambao wamebaki kuhudhuria Ibada wakati wa Sherehe za Pasaka na Noeli; na wakati wa Ibada za mazishi, lakini wakiwa wamekaa mbali kama "watazamaji wa soka na wala si waamini"!

Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha waamini kwamba, Ibilisi, shetani ambaye ni “baba wa ubaya na maafa ya binadamu yupo kama kawa”! Wanapaswa kupambana naye kwa kushiriki kikamilifu katika Sakramenti za Kanisa; kwa kufunga na kusali ili kuratibu vilema vyao; kwa kusoma na kulitafakari Neno la Mungu wanalopaswa kulimwilisha katika uhalisia wa maisha yao, daima wakijitahidi kujenga na kukuza dhamiri nyofu. Waamini wasizoee kukaa katika dhambi kwa muda mrefu, bali wajenge utamaduni na mazoea ya kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika Mahakama ya huruma ya Mungu inayowaonjesha matumaini na upya wa maisha unaobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Kristo Yesu! Waamini wawe ni mashuhuda na vyombo vya haki, amani, upendo na mshikamano, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi!

Kwa ufupi, haya ndiyo mambo msingi ambayo Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwashirikisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, katika maisha na utume wake, ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya furaha; huruma na upendo wa Mungu, tayari kutoka kimasomaso kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

14/03/2018 08:20