Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Habari \ Habari kutoka Barani Afrika

Tanzania: Deni la taifa limefikia sh. 47, 756 bilioni, lakini...!

Hadi kufikia Desemba 2017 deni la taifa limefikia kiasi cha shilingi bilioni 47, 756 na kwamba, deni hili ni himilivu! - AFP

13/03/2018 14:03

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema hadi kufikia Desemba, 2017 deni la taifa limefikia sh.bil 47,756 . Kauli hiyo ilitolewa Jumatatu, tarehe 12 Machi 2018 na  Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango alipokuwa akiwasilisha Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na ya kiwango na ukomo wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2018/19 mjini Dodoma. Dk Mpango alisema kuwa hadi kufikia Desemba 2017 deni la Taifa limefikia Sh 47,756 bilioni na kwamba tathmini iliyofanyika Novemba, 2017 imeonyesha kuwa bado deni hilo ni himilivu.

Alisema deni la nje ya nchi ni Sh .bilion  34,148.6  sawa na asilimia 71.5 ya deni lote, deni la ndani lilikuwa Sh bilioni 13,607.7 sawa na asilimia 28.5 ya deni hilo na kwamba tathimini ya uhimilivu wa deni iliyofanyika Novemba mwaka jana inaonyesha kuwa deni ni himilivu kwa kipindi cha muda wa kati na muda mrefu. Mbali na hilo Dk. Mpango alisema uwiano wa deni la ndani na nje kwa pato la Taifa kwa mwaka 2017/18 ni asilimia 34.4, ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 56, hivyo deni bado lipo chini ya kiwango cha hatari. “Uwiano wa deni la nje na mauzo ya nje ni asilimia 81.1 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 150. Hii inamaanisha kuwa uwezo wetu wa kulipa deni bado ni imara,” alisema. Alisema, Serikali inaendelea kuchukua tahadhari kwa kukopa kwenye vyanzo vyenye masharti nafuu na kuhakikisha kuwa mikopo hiyo inaelekezwa kwenye miradi ya maendeleo.

Mfumuko wa bei: Kuhusu mfumuko wa bei, Dk. Mpango alisema kwa mwaka 2017 mwenendo wa mfumuko wa bei ulikuwa tulivu kutokana na kuimarika kwa upatikanaji wa chakula nchini. Alisema kuwa utulivu wa bei za nishati hasa mafuta katika soko la ndani na nje ya nchi na usimamizi thabiti wa sera za fedha na za bajeti. Alisema hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huo, mfumuko wa bei ulikuwa wastani wa asilimia 5.3 na umeendelea kupungua na kufikia asilimia 4.1 katika kipindi cha mwezi Februari 2018. Akiba ya fedha za kigeni: Akiendelea kutoa ufafanuzi Dk. Mpango alisema katika kipindi kinachoishia Desemba 2017, akiba ya fedha za kigeni ilifikia Dola za Marekani milioni 5,906.2 ikilinganishwa na Dola za Marekani milioni 4,325.6 katika kipindi cha mwaka 2016. Alisema kiasi hicho kilichofikiwa mwezi Desemba 2017 kilikuwa kinatosheleza kugharamia ununuzi wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa miezi 6 na hivyo kiwango cha angalau miezi 4.5 kilichowekwa kukidhi matakwa ya hatua za mtangamano wa umoja wa fedha kwa nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki,” alisema Dk Mpango.

Aidha, alieleza kuwa katika kipindi cha mwaka ulioishia Desemba 2017, mwenendo wa thamani ya Shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya Marekani uliendelea kuwa wa kuridhisha. Riba za amana “Kipindi cha mwaka unaoishia Desemba 2017, wastani wa riba za amana uliongezeka kufikia asilimia 9.6 kutoka wastani wa asilimia 8.8 Desemba 2016. “Viwango vya riba za amana za mwaka mmoja vilipungua kutoka asilimia 11 Desemba 2016 hadi asilimia 10.9 Desemba 2017,hata hivyo viwango vya riba za mikopo ya hadi mwaka mmoja viliongezeka kufikia asilimia 18.2 Desemba 2017 kutoka wastani wa asilimia 12.9 Desemba  2016.” Alifafanua Dk. Mpango. Alisema kuwa hali hiyo ilitokana na mabenki kuchukua tahadhari kubwa kwa wateja wanaoshindwa kurejesha mikopo. Aidha alieleza kuwa, riba katika soko la fedha baina ya mabenki ilipungua na kufikia wastani wa asilimia 3.3 Desemba 2017 kutoka asilimia 13.5 Desemba 2016. Alisema riba kwenye dhamana za serikali ilipungua kutoka asilimia 15.1 Desemba 2016 hadi asilimia 8.2 Desemba 2017.

NA DANSON KAIJAGE, DODOMA.

13/03/2018 14:03