Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa \ Kanisa Ulimwenguni

Papa Francisko ni shuhuda wa majadiliano ya kiekumene katika huduma

Papa Francisko ni shuhuda na chombo cha majadiliano ya kiekumene kinachowawezesha Wakristo kutembea, kusali na kufanya kazi katika umoja kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia.

13/03/2018 07:47

Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 70 tangu kuanzishwa kwake anasema, Baraza limekuwa mstari wa mbele kusimamia na kudumisha haki msingi za binadamu, utu na heshima yake, kwa kutambua kwamba, mwanadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Baraza litaendelea kuwa mstari wa mbele kutetea haki msingi za binadamu sehemu mbali mbali za dunia. Litaendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene na kidini kwa kuwashirikisha viongozi wa dini na Makanisa mbali mbali duniani, lakini zaidi kwa kuwashirikisha vijana wa kizazi kipya, ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na mshikamano kati ya watu wa Mataifa.

Maadhimisho haya, yatapambwa kwa namna ya pekee kabisa, na uwepo pamoja na ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 21 Juni 2018, kwa kutembelea Makao Makuu ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni, huko Geneva, nchini Uswiss. Hii ni alama muhimu sana kwa watu wote wanaoendelea kusimama  kidete: kwa ajili ya kutafuta na kudumisha umoja, amani na haki msingi za binadamu katika ulimwengu wa utandawazi unaogubikwa na blanketi la vita, chuki, ghasia, ubinafsi na uchafuzi mkubwa wa mazingira nyumba ya wote.

Hii ni changamoto kwa Makanisa kusimama kidete ili kuweza kuihudumia familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia kwa kujikita katika uekumene wa huduma, umoja, upatanisho na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Makanisa yanaweza kuendeleza uekumene wa huduma hata katika utofauti wao, jambo la msingi ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Katika kipindi cha miaka 70 ya uwepo wake, Baraza la Makanisa Ulimwenguni limekuwa ni jukwaa makini la kushirikishana: utajiri, amana na tunu msingi za maisha ya Kiinjili na kiutu. Limeendelea kudumisha mapokeo ya Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo  sanjari na kudumisha uekumene wa maisha ya kiroho; uekumene wa damu, uekumene wa huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na sababu mbali mbali.

Hija ya Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho haya ni kutambua na kuthamini kazi kubwa ya wakristo kutoka Makanisa mbali mbali ambao wameendeleza uekumene wa sala na wako tayari kufanya hija ya pamoja kutafuta umoja, haki na amani mintarafu tunu msingi za Kiinjili na ushuhuda unaofumbatwa katika Injili ya maisha na matumaini, kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Kauli mbiu inayoongoza hija hii ya kiekumene ni “Kutembea, kusali na kufanya kazi kwa pamoja”.

Dr. Olav Fykse Tveit anakaza kusema, Baraza limeendelea kujizatiti katika kukuza na kudumisha sera na mikakati ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Tangu mwaka 1992, Baraza la Makanisa Ulimwenguni limeragibisha haki ya mazingira kwa kutambua kwamba uchafuzi wa mazingira una maadhara makubwa kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Hiki ni kielelezo cha umoja na mshikamano katika huduma ya maendeleo endelevu ya binadamu kama kinavyodadavuliwa na Baraza la Makanisa Ulimwenguni kwa kushirikiana na Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Majadiliano ya Kiekumene.

Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake, ameendelea kujipambanua kuwa ni kiongozi anayetoa kipaumbele cha pekee katika majadiliano ya kiekumene. Ameonesha ushirikiano na mshikamano wa dhati na Patriaki Bartolomeo wa kwanza katika kupanga sera na mikakati ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Amejizatiti kikamilifu kwa kushirikiana na Askofu mkuu Justin Welby, Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani duniani katika kutafuta amani katika nchi zenye vita, chokochoko na ghasia kama Sudan ya Kusini, Siria, Korea ya Kusini, Nigeria na katika nchi kadhaa Barani Ulaya zinazoogelea katika kinzani za kisiasa na kijamii. Viongozi wa Makanisa kwa pamoja wametetea utu, heshima na haki msingi za wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia pamoja na kuendelea kushikamana katika mapambano ya biashara ya binadamu na utumwa mamboleo.

Ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani, huko Lund, nchini Sweden, ni tukio ambalo limeacha alama ya kudumu katika akili na nyoyo za waamini wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Duniani. Baada ya vuta nikuvute, kinzani na migogoro ya kidini, Waluteri na Wakatoliki, wakakutana mubashara na hatimaye, kuamua kushirikiana katika huduma za kijamii, ili kuendeleza uekumene wa huduma kwa maskini, wakimbizi, wahamiaji na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Huu ndio ushuhuda wa uekumene wa huduma unaopewa msukumo wa pekee na viongozi wa Makanisa!

Baba Mtakatifu Francisko ameonesha umakini na ushirikiano wa pekee na Patriaki Tawadros II ambao wametambua Ubatizo mmoja kwa maondoleo ya dhambi! Dr. Olav Fykse Tveit anaendelea kufafanua kwamba, katika kipindi cha miaka 50 tangu baada ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, kumekuwepo na ushirikiano wa dhati katika medani mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa hasa katika masuala ya haki, amani, ustawi, mafao na maendeleo ya wengi, dhamana ambayo kwa sasa inatekelezwa na Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu chini ya uongozi wa Kardinali Peter Turkson.

Katika mwelekeo huu, Mwezi Septemba, 2018, Baraza la Makanisa Ulimwenguni kwa kushirikiana na Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu litafanya mkutano wa kimataifa kuhusu: ”Wasi wasi usiokuwa na mashiko, Ubaguzi wa rangi na umaarufu wa baadhi ya wanasiasa ambao wamewatumbukiza wananchi wao katika majanga makubwa, umaskini na fedheha.  Umoja, ushirikiano na mshikamano kati ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni pamoja na Kanisa Katoliki anasema Dr. Olav Fykse Tveit ni cheche za moto wa matumaini, si tu, kwa ajili ya Makanisa ulimwenguni, bali kwa watu wa Mungu wanaoteseka kutokana na ukosefu wa haki msingi za binadamu, vita na ghasia; ujinga, umaskini na maradhi. Uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Makanisa Ulimwenguni linaloyajumuiya Makanisa wanachama 348 ni alama ya matumaini, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, Makanisa yanapoendeleza hija ya haki na amani, kwa kusali na kuendelea kushikamana katika upendo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

13/03/2018 07:47