2018-03-13 10:36:00

Miaka 7 ya Vita Siria, watoto zaidi ya 2, 500 wameuwawa kikatili!


Imegota miaka saba tangu vita ya wenyewe kwa wenyewe ianze kutimua vumbi nchini Siria! Kila siku kuna watu wanaopoteza maisha kutokana na vita hii, lakini waathirika wakubwa ni watoto, wanawake na wazee. Umoja wa Mataifa unasema kwamba, watoto milioni 8.6 wanahitaji msada wa dharura; watoto milioni 6 hawana makazi salama na wengine 2, 500 wameuwawa kikatili kati ya mwaka 2014- 2017. Hii inaonesha kwamba, kwa hakika vita haina pazia na wala si mchezo. Miundo mbinu ya huduma ya elimu, afya na makazi ya watu imeharibiwa kiasi kwamba watu zaidi ya 18, 500 hawana mahali pa kuishi katika eneo la Ein Terma kutokana na mapigano kuendelea kupamba moto kwa siku za usoni!

Kuna zaidi ya familia 1, 400 zinazoishi kwenye maandaki, bila ya kuwa na huduma msingi ya maji safi na salama pamoja na huduma ya afya, hali inayosababisha mateso na milipuko ya magonjwa kwa watoto wadogo nchini Siria. Taarifa ya Shirika la Kimataifa la “Save the Children” inaonesha kwamba, watoto wameathirika sana kutokana na vita huko Siria na pengine itawachukua muda mrefu kuweza kupata tiba muafaka ya madhara haya! Taarifa za Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya watu milioni 6 wasiokuwa na makazi maalum nchini Siria. Watu zaidi ya 385, 000 walilazimika kuyakimbia makazi yao katika kipindi cha Mwaka 2017 ili kutafuta: hifadhi na usalama wa maisha yao. Kati yao kuna watoto 3, 500 ambao hatima ya maisha yao iko mashakani sana. Watoto wanaendelea kuteseka kwa njaa na utapia mlo wa kutisha hasa katika maeneo ambayo si rahisi sana kufikiwa na Mashirika ya Misaada ya kiutu na kwamba, watoto wengi wanaokumbwa na utapiamlo wa kutisha wako eneo la Ghout, hali ambayo inaathari kubwa hata katika ukuaji wao!

Yote haya yanachangiwa pia na ukosefu wa huduma bora ya afya, kiasi kwamba, watoto wanajikuta wamehukumiwa kifo linasema Shirika la “Save the Children” kutokana na ukosefu wa dawa muhimu na huduma bora ya afya. Asilimia 43% ya miundo mbinu ya elimu haitumiki tena kutokana na kuharibiwa vibaya sana kwa vita na wengi wao wamepoteza maisha kwa kushambuliwa wakiwa shuleni! Kiwango cha watoto wa Siria kujua kusoma na kuandika kinaendelea kushuka kila kukicha. Hawa ni watoto ambao wamezaliwa na kukulia katika vita na migogoro ya kijamii. Familia tena si mahali salama pa malezi na makuzi ya watoto kwani wanatumiwa kama chambo cha kupata chakula na misaada ya kiutu! Ni wajibu kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, suluhu ya amani inapatikana nchini Siria, ili kuokoa maisha ya watu wanaoteseka kutokana na vita, ghasia na mipasuko ya kijamii!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.