Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Majadiliano ya kiekumene

Makanisa Ulimwenguni yawe ni: vyombo vya haki, amani na upendo!

Makanisa ulimwenguni yanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa uinjilishaji na utamadunisho; haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. - REUTERS

13/03/2018 08:10

Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC., linaloyajumuisha Makanisa wanachama zaidi ya 348, kuanzia tarehe 8-13 Machi 2018; limeadhimisha Mkutano mkuu wa Uinjilishaji Ulimwenguni, uliokuwa ukifanyika kwenye kilima cha Ngurdoto, Jijini Arusha, Tanzania, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Kutembea katika Roho: tunaitwa kuwa wafuasi wanaobadilika”. Mkutano ulifunguliwa kwa hamasa kubwa kwa wajumbe kuchangia: mawazo, maoni na ushuhuda wao katika mchakato mzima wa uinjilishaji ulimwenguni. Wamekazia: haki, amani, utu, heshima na haki msingi za binadamu zinazopaswa kufanyiwa kazi na Makanisa haya katika ulimwengu unaobadilika kwa kasi kubwa.

Ni changamoto ya kuendeleza majadiliano ya kiekumene, kidini na kisiasa, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki na amani duniani. Penye vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, ni vigumu sana kwa imani, matumaini na mapendo kuweza kupenya katika sakafu ya nyoyo za watu, kama ilivyo kwa sasa nchini DRC na katika nchi ambamo mtutu wa bunduki umekuwa ni chakula chao cha kila siku! Matokeo yake ni watu kuendelea kutumbukia katika umaskini wa hali na kipato, magonjwa na ujinga na hata kulazimika kuzikimbia nchi zao, ili kutafuta:usalama, hifadhi na maisha bora zaidi! Makanisa yanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini kwa wale waliokata tamaa katika maisha.

Mkutano huu, imekuwa ni nafasi kwa wajumbe kushirikisha ukweli na uwazi wa maisha ya watu wanaowahudumia katika uhalisia wake bila kumung’unya maneno! Wajumbe wa wanawake kutoka katika nchi 170 wameonesha na kushuhudia kwamba, bado ni “majembe” ya nguvu yanayotegemewa na Makanisa katika dhamana ya uinjilishaji kwa sababu wao ni walezi na warithishaji wakuu wa tunu msingi za kiinjili, kiutu na kimaadili, lakini wanapaswa kujengewa uwezo na kupatiwa nafasi katika maisha na utume wa Makanisa ulimwenguni! Wanafunzi kutoka katika Taasisi ya Taalimungu ya Kiekumene Kimataifa, “Global Ecumenical Theological Institute” GETI, 2018 wamepanda miti 12 kama sehemu ya kumbu kumbu ya maadhimisho ya miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Makanisa Ulimwenguni. Tukio hili litapambwa pia kwa uwepo na ushuhuda wa Baba Mtakatifu Francisko kwenye Makao Makuu ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni huko Geneva, Uswiss, hapo tarehe 21 Juni 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu "Kutembea, Kusali na Kufanya kazi kwa pamoja".

Dr. Olav Fyske Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC., anasema, wafuasi wa Kristo Yesu, tangu mwanzo wamekuwa wakihimizwa kubadilika kwa kusoma alama za nyakati na uhalisia wa maisha na utume wao, tangu wakati ule walipoanza kumfuasa Kristo Yesu, kila mmoja wao akiwa na mawazo na matamanio binafsi. Baada ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, wafuasi wa Yesu walikuwa na mwelekeo mpya kabisa katika maisha na utume wao, wakapata ari, nguvu na ujasiri wa kutoka kimasomaso kutangaza na kushuhudia Fumbo la Pasaka.

Huu ni mwaliko kwa wakristo kujenga na kudumisha umoja na mshikamano, ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Mwenyezi Mungu, chemchemi ya maisha anaendelea kufanya mabadiliko ulimwenguni kwa kuumba, kukomboa, kuokoa na kupyaisha tena na tena! Kanisa linahamasishwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuleta mageuzi ulimwenguni kwa kujikita katika upendo, umoja na mshikamano kama kielelezo cha ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Wakristo wawe tayari kumsikiliza Roho Mtakatifu anayeliongoza Kanisa katika utekelezaji wa dhamana na utume wake wa uinjilishaji ulimwenguni, ili kutambua: fursa zilizopo, changamoto na matatizo wanayoweza kukumbana nayo katika maisha na utume wa Kanisa. Haya ni mabadiliko yanayowezekana kwa watu kujenga utamaduni wa kukutana, kujadiliana na kutekeleza maamuzi katika umoja, upendo na mshikamano.

Dr. Olav Fyske Tveit anaendelea kufafanua kwamba, katika kipindi cha miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, mabadiliko yamekuwa ni kati ya mambo makuu yaliyofanyiwa kazi, ili kujenga Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika: upendo, haki, amani, utu na heshima ya binadamu. Baraza la Makanisa bado linaendelea kujizatiti katika kukuza na kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwa Makanisa wanachama kwa njia ya majadiliano ya kiekumene na kidini na waamini wa dini mbali mbali duniani. Wakristo wanahamasishwa kuwa ni vyombo na chachu ya mabadiliko ulimwenguni, kwa kushuhudia imani, matumaini na mapendo. Wakristo wanayo fursa ya pekee ya kuweza kushiriki kikamilifu katika utume wa Mungu, ikiwa kama watakuwa wameungana katika umoja, upendo na mshikamano!

Kwa upande wake, Adi Mariana Waga katika hotuba yake elekezi, amewataka viongozi wa Makanisa kuishi na kutembea katika mwanga wa Roho Mtakatifu, kwa kutambua kwamba, wameitwa, wakapakwa mafuta na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Wakristo wanahamasishwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Kristo ili kuleta mabadiliko yanayofumbatwa katika upendo, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Waamini waendelee kujizatiti katika kulinda na kudumisha utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, ili kuzima kiu ya haki, uponyaji na upatanisho. Ni mwaliko wa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji inayotekelezwa na Makanisa sehemu mbali mbali za dunia. Makanisa hayana budi kuendelea kujikita katika utume wa huduma kama ushuhuda wa kinabii unaopania kuwakomboa binadamu kutoka katika umaskini, ujinga na maradhi, ili kuwajengea uwezo wa kujiletea maendeleo endelevu yanayogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Adi Mariana Waga ambaye ni mwanataalimungu kijana kutoka Fiji anasema, Kanisa liwe ni chachu ya mabadiliko katika ulimwengu wa upashanaji habari, maendeleo ya sayansi na teknolojia pamoja utandawazi. Lengo liwe ni kupambana na utandawazi usioguswa na mahangaiko yaw engine kutokana na ubinafsi, uchu wa mali na madaraka, vita, kinzani na nyanyaso za kila aina. Kanisa liwe ni nguvu ya kutambua makosa yaliyofanywa katika mchakato mzima wa uinjilishaji uliofumbatwa pia katika ukoloni mkongwe, ambao umesababisha baadhi ya nchi kunyonywa kwa kiasi kikubwa; kudharau tamaduni, mila na desturi njema za watu mahalia na matokeo yake ni mwendelezo wa ukoloni mamboleo, usiozingatia utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Huu ni wakati wa Makanisa kujikita katika uinjilishaji unaofumbatwa katika mchakato wa utamadunisho, ili kuwawezesha watu mahalia kujipatia mabadiliko ya kweli kadiri ya tunu msingi za kiinjili na kiutu! Watu mahalia wawezeshwe kusimamia rasilimali na utajiri wao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kuliko hali ilivyo kwa wakati huu, kwani utajiri na rasilimali za nchi maskini duniani, zinaendelea kuyanufaisha mataifa makubwa na mashirika ya kimataifa. Wananchi wajengewe uwezo wa kiuchumi na kisiasa ili kuleta mabadiliko katika mustakabali wa maendeleo yao. Wananchi mahalia hata katika umaskini wao, bado ni watu wenye thamani kubwa sana mbele ya Mungu kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

13/03/2018 08:10