Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Tafakari ya Neno la Mungu

Kristo Yesu akishakuinuliwa juu ya nchi, atawavuta wote kwake!

Kristo Yesu akiinuliwa juu ya nchi, atawavuta wote kwake, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha utii kwa Baba yake wa mbinguni, mwanzo wa Agano Jipya na la milele. - AFP

13/03/2018 14:46

Tunaona katika somo kwanza, kuwa Nabii Yeremia anaitwa na Mungu akiwa kijana kabisa. Aliitwa wakati utawala wa Yuda ukiwa katika mazingira magumu kabisa – 627-587. Kila mmoja – makuhani, wafalme na watu walielekeza maisha yao katika mambo ya siasa zaidi na kumsahau Mungu. Hivyo wanajikuta utumwani Babeli, wanalipa kodi n.k. Wakitazama nyuma, wanadhani pengine wangehitaji msaada toka Misri. Nabii Yeremia anapinga mtazamo huu wa kipagani wa kutaka kurudi katika hali ya dhambi iliyowamalizia mbali. Nabii anaongea wazi wazi ubaya wa dhambi zao, anawakumbusha kosa lao lililopelekea kuharibu mji na hekalu lao. Walivunja agano na Mungu, wakaenda utumwani. Sasa wanaahidiwa Agano Jipya lakini litakaloandikwa katika mioyo yao, linaongozwa na moyo na si sheria au amri. Na anaongea kuhusu wakati wa Kimasiya.

Hapa kuna hitaji la Agano Jipya kwa sababu walipoteza dira, wakageukia miungu mingine – Yer. 3:8-9; Ezek. 23:7; Hosea 2:1-13; 4:12-14. Hili agano jipya linafungwa katika mioyo yetu na uhusiano unakuwa moja kwa moja na Mungu. Hakuna tena haja ya wajumbe wa kati. Mungu anaongea moja kwa moja na watu wake na atafahamika na watu wote na ataonekana katika utukufu wa Mwana. Hiki kipindi kipya, huu mwanzo mpya, ni kipindi cha msamaha wa dhambi na mwana Kondoo wa Mungu atachukua na kufuta dhambi zetu. Yoh. 1:29 – siku ya pili yake, alimwona Yesu anakuja kwake, akasema, tazameni Mwanakondoo wa Mungu aondaye dhambi za ulimwengu. Ni muda wa Agano Jipya, linalotufanga na Mungu. Ni Agano Jipya. Kwa hiyo kushika amri si tena jambo gumu na jambo la nje nje tu ila itaandikwa kwenye mioyo ya watu na Mungu mwenyewe, huku akitupatia msamaha wa dhambi.

Katika somo la Pili – kitabu ambacho kimendikwa na mfuasi wa Mtakatifu Paulo kwa baadhi ya waongofu: Kuhakikisha toka Agano la Kale kwamba Kristo ndiye yule aliyeahidiwa na Mungu. Yeye aliweka mwisho kwa yale ya zamani au yalipewa maana mpya katika uwepo wake. Katika siku hizi Yesu anashiriki nasi mwili na mateso lakini akijua kuwa Mungu atamwokoa na hali hiyo, katika hali ya kifo – Yoh. 12:27-32; 17:5; Mdo. 2:25-31. Alijifunza haya akiwa mwaminifu na mtii kwa Baba na hivyo akakwezwa katika utukufu. Kwa njia yake, sote tumekuwa warithi wa ufalme wa Mungu. Kuna haja ya kuishi hizo mbinu au njia za wokovu alizotufundisha Yesu kupata wokovu. Sehemu hii ya somo la leo yaongelea kuhusu Yesu kama Kuhani mwenye huruma.

Katika Injili – tunaongozwa na wazo la kujitoa kama mbegu ili kuanza upya. Kama tungesoma sura iliyotangulia twaona ufufuko wa Lazaro – akakwezwa kama mshindi wa mauti. Katika sura hii ya 12 tunaona mwisho wa utume wa hadharani wa Yesu. Ni tendo la mwisho rasmi la Yesu hadharani kabla ya Jumapili ya Matawi. Pia katika sura hii ya 12;12 – tunaona aingiavyo Yerusalemu kama Masiya na katika sehemu hii ya Injili, anatamka utukufu wake kwa njia ya mauti.  Na katika Yoh. 12:19 – hapo mafarisayo walipoona hayo yote, wakasemezana, mwaona, yote ni kazi bure. Tazameni, ulimwengu wote unamfuata yeye. Na hapa ndo somo la leo linaanza – masiya anatangazwa kwa Wagiriki. Wakati Yesu akiishi hapa duniani, Wagiriki walikuwa ni taifa kubwa na lililoenea sana. Kulikuwa na vikundi vingi vya dini na falsafa mbalimbali. Katika watu waliofika katika sherehe ya mikate ni hawa Wagiriki. Wakatambua kuwa kuna kitu cha pekee pale Yerusalemu. Wakataka kumwona Yesu. Kwa  nini? Pengine sababu ziko nyingi. Jibu la Yesu ni tofauti na matarajio yako. Angalia dhamira yetu ya leo – wanataka kumwona Yesu. Ni mtu wa aina gani? Katika Injili ya Yohani – kuona ni kuamini.

Walitaka kumwona Yesu naye anajitambulisha kwao katika dhana ya mateso ila kwa utukufu. Kifo chake kimeleta uzima. Bila mateso, maisha ya Kristo hayana maana. Yesu anaona kifo kama ukamilifu wa uzima na utume wake.  Katika Yoh. 7:30, 8:20 – tunaona mazingira mengi ya kifo yaliyomkabili Yesu, lakini anasema wazi, wakati haujatimia. Katika somo hili la Injili – huo muda umefika na anatumia mfano wa chembe ya ngano kuelezea hilo. Wale wote wanaotaka kumfuata basi hawana budi kufanya hivyo. Yesu yuko wapi? Katika utukufu. Ila kufika hapo alipita katika mlango wa kifo katika uaminifu kwa mapenzi ya Mungu. Hiyo ndiyo habari. Pengine inaonekana kuwa mwanadamu hawezi kupitia njia hiyo. Tutafakarishwe na maisha ya ushuhuda ya Mt. Maxilian Maria Koble – ambaye alitoa maisha yake wakati wa utawala wa wanazi huko Polandi kwa ajili ya kumwokoa mwingine.

Tukumbuke kuwa hamu kubwa ya mwanadamu ni kumwona Mungu. Katika Agano la Kale – Zab. 119:135 – umwangazie mtumishi wako uso wako, unifundishe kanuni zako. Pia tunakumbushwa kumtafuta Mungu – Zab. 27:8 – moyo wangu unasema, njoo utafute uso wake Mungu, nitautafuta uso wako Ee Mungu. Ila inaonekana kuwa si jambo rahisi kumwona Mungu – Zab. 102:2 - usinifiche mimi uso wako siku ya shida yangu. Unitegee sikio lako, unisikilize upesi ninapokuomba. Aidha Musa alipoongea na Mungu aliomba kumwona uso wake. Mungu alimwambia haiwezekani – huwezi kuniona na kuishi – Kut. 33:20 – akazidi kusema, huwezi kuniona uso wangu, kwa maana mwanadamu hawezi kuniona akaishi. Katika zaburi, tunapoomba kuona uso wake Mungu, yamaanisha kuingia katika ukweli wake, katika mapenzi yake. Aidha katika Ufu. 22:4 – tunasoma – watauona uso wake. Sisi leo tunaweza kuuona uso wa Mungu uliofunuliwa kwetu katika Yesu Kristo wa Nazareti. Hii inadhihirisha jibu la Yesu kwa wale Wagiriki – atashinda mauti, atatukuzwa katika ufufuko, ni mwokozi aletaye wokovu kwa watu wote. Mbegu ni lazima ianguke ardhini ili ipate kuoza na hatimaye, kuzaa upya.

Tutafakarishwe na maisha ya mama mmoja aliyelemaa miguu baada ya ajali mbaya ya gari. Tangu hapo akawa mlemavu wa miguu na akitumia magongo kutembea. Siku moja akiwa jikoni akipika, alisikia harufu ya moshi toka chumba cha juu. Akatambua kuwa sehemu hiyo imeshika moto na chumbani mtoto wake mdogo alikuwa amelala naye alikuwa peke yake nyumbani. Alipata nguvu ya ajabu ya kutupa yale magongo, na kupanda chumbani kumwokoa mwanae aliyekuwa katika hatari. Hakuna hata madaktari walioamini kile kilichotokea. Ili kupata uzima ni lazima kuupoteza. Ili wengine waweze pia kuishi. Hapa haja ya kiongozi makini ili kuwaongoza wengine kwa Yesu inaonekana wazi. Ili kutoa uzima ni lazima pia sisi tuwe na huo uzima, tuwe nao tele tena wa kimungu. Angalia mtume Andrea na Filipo walivyofanya – wakawachukua kwa Yesu.  Ili kufika kwa Yesu ni lazima kuongozwa. Wale wanaoishi maisha hayo, wanashuhudia, wanamwonesha Yesu kwetu kwa ulimwengu. Huu ni wajibu wa kila anayemwamini Mungu.

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.

13/03/2018 14:46