Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Hotuba

Walimwengu wanatamani kuwaona mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu

Papa Francisko asema, walimwengu wana kiu kubwa ya kutaka kuonana na mashuhuda na vyombo vya huruma katika maisha yao, ili kuwashirikisha: Injili ya imani, matumaini na mapendo yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

12/03/2018 11:35

Huruma ni kielelezo makini cha upendo wa Mungu unaosamehe, unaopyaisha na kubadili mwelekeo wa maisha, kielelezo cha ufunuo wa Fumbo la Mungu ambao ni huruma ya milele, inayowakumbatia na kuwaambata wote pasi na ubaguzi. Ni huruma inayowakirimia chemchemi ya furaha na matumaini ya maisha mapya, yanayovunjilia mbali ubinafsi ili kutenda wema, kufikiri vyema na kuondoa huzuni moyoni. Huu ni mwaliko kwa waamini kufanya mang’amuzi ya huruma inayowakirimia furaha, hata kama bado maisha yanasheheni matatizo na changamoto mbali mbali, ili kuondokana na utamaduni wa huzuni, utupu na upweke unaopelekea msongo wa mawazo kwa watu wengi!

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Misericordia et misera” yaani “Huruma na amani” anasema, ulimwengu mamboleo unahitaji mashuhuda na vyombo vya matumaini na furaha ya kweli inayobubujika kutoka katika undani wa mtu anayefurahia uwepo wa Kristo Yesu ndani mwake! Hii ni changamoto ambayo Baba Mtakatifu Francisko amependa kuwashirikisha wajumbe wa Chama cha “Fontaine de la Misericorde”  kutoka nchini Uswiss, waliomtembelea mjini Vatican, Jumamosi, tarehe 10 Machi 2018 kama sehemu ya hija ya maisha ya kiroho mjini Roma.

Baba Mtakatifu amewashukuru kwa kuwapokea na kuwasindikiza wale wote wanaowahudumia kwa njia ya “Shule ya Sala” na majiundo ya kidugu, changamoto na mwaliko wa kuendelea kujizatiti katika maisha ya sala yanayowawezesha kukutana mubashara na Kristo Yesu; wanaposoma na kutafakari Neno la Mungu, anawajalia tena nafasi ya kuzama katika chemchemi ya huruma ya Mungu inayobubujika kutoka katika Moyo wake Mtakatifu, uliotobolewa kwa mkuki! Baba Mtakatifu anawataka wajumbe wa chama hiki cha “Chemchemi ya huruma ya Mungu” kwa njia ya maisha yao ya Kisakramenti kuwa vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu, wito kwa watu wote kutambua uzuri na furaha ya kupendwa na kuthaminiwa na Mwenyezi Mungu.

Mwishoni, Baba Mtakatifu anawahimiza kwa msaada wa Roho Mtakatifu, kujenga na kukuza maisha ya kidugu yanayofumbatwa katika utamaduni wa watu kukutana, kwa kuheshimiana na kuthaminiana bila ya mtu kumbeza au kumdharau jirani yake, kiasi cha kumpatia kisogo, anapoona anateseka kwa sababu mbali mbali katika maisha. Amewaweka wanachama wote wa Chama cha “Chemchemi ya huruma ya Mungu” chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria na kwamba, waendelee kumsindikiza kwa sala katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

12/03/2018 11:35