Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa \ Kanisa Ulimwenguni

Ushuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa watu wa Mataifa!

Watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia wameshuhudi Injili ya huruma, upendo na matumaini ilivyowagusa katika maisha yao kwa njia ya Jumuiya ya Mtakatifu Egidio katika kipindi cha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake!

12/03/2018 09:37

Katika mwendelezo wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili, tarehe 11 Machi 2018 alipata nafasi ya kusikiliza shuhuda za maisha na utume wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Hawa ni watu wanaounda na kujenga Jumuiya ya Mtakatifu Egidio kutokana na huduma makini ili kuwaonjesha watu hawa furaha ya Injili inayobubujika kutoka katika: shule ya amani kwa ajili ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi Afrika na Amerika ya Kusini. Injili ya upendo kwa maskini, wazee na watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Hawa ni wale ambao wameonjeshwa Injili ya matumaini ya kuendelea kuishi na kupambana na hali zao dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi, kwa njia ya Mradi wa “Dream” unaopania kudhibiti maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto. Katika kipindi cha miaka 15 zaidi ya watoto laki moja wamezaliwa kutoka kwa akina mama waliokuwa wameambukizwa virusi vya Ukimwi, lakini watoto hawa wako salama salimini. Mradi wa "Bravo" unaowasaidia watoto kupata fursa tena ya kuandikishwa na hatimaye, kurejea shuleni kuendelea na masomo. Ushuhuda huu umetolewa na wakimbizi na wahamiaji waliofanikiwa kusalimisha maisha yao kwa kutumia “njia za ubinadamu”. Huu ni mradi ambao Jumuiya ya Mtakatifu Egidio inashirikiana kwa dhati na Makanisa ya Kiinjili nchini Italia ili kuwahudumia waathirika wa vita kutoka Siria na huko Mashariki ya Kati. Zaidi ya watu 1, 000 tayari wamepatiwa hifadhi nchini Italia.

Jumuiya pia kwa kushirikiana na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI imeweza kutoa hifadhi kwa wakimbizi na wahamiaji 500 kutoka katika Nchi za Pembe ya Afrika.  Jumuiya ya Mtakatifu Egidio imeendelea kujikita katika mchakato wa kutafuta na kudumisha amani sehemu mbali mbali za dunia kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa huko Senegal, Sudan ya Kusini, Libia, Iraq na Ufilippini. Hawa ni mashuhuda wa Injili ya upendo na mshikamano unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu, kila kukicha. Ni ushuhuda ambao umejikita katika sala inayoendeshwa na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, sehemu mbali mbali za dunia!

Professa Marco Impagliazzo, Rais wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio amemwambia Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Neno la Mungu na Sala ni kiini cha maisha na utume wao kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Anamshukuru Baba Mtakatifu Francisko ambaye ametoa kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wake kwa maskini kama amana na utajiri wa Kanisa na kwamba, hawa ni walengwa wa kwanza wa Habari Njema ya Wokovu wanaofumbatwa na kuambatwa na huruma na upendo wa Mungu.

Padre Marco Gvavi, anasema, katika kipindi cha miaka 50 ya maisha na utume wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, wamejitahidi kuwa ni Wasamaria wema wanaomwilisha Amri kuu ya Upendo kwa Mungu na jirani kama kielelezo na ushuhuda wa imani tendaji. Ni Jumuiya ambayo imejikita katika kusoma, kusikiliza na kulitafakari Neno la Mungu kama ilivyokuwa kwa Maria aliyekuwa amechagua fungu bora zaidi kwa kumsikiliza Kristo Yesu, bila kusahau huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kama alivyofanya Martha alipokuwa anamhudumia Yesu nyumbani mwao. Kumbe, Jumuiya ya Mtakatifu Egidio inamwilisha ile kanuni kuu ya Sala na Kazi; Ora et Labora! Hiki ni kielelezo cha chemchemi ya: huruma, upendo na mshikamano wa dhati unaoleta mabadiliko ya kweli katika maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

12/03/2018 09:37