Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Mahubiri

Papa Francisko: Upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu haina mipaka!

Papa Francisko asema, wema na huruma ya Mungu kwa waja wake hauna mipaka hata kidogo.

12/03/2018 11:22

Mama Kanisa anaendelea kutoa kipaumbele cha pekee katika Sakramenti ya Upatanisho kama mahali muafaka pa kuonja huruma na upendo wa Mungu, tayari kusimama tena na kuendelea na safari ya Imani, matumaini na mapendo kwa Mungu na jirani! Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha Mapadre waungamishaji kwamba, wao ni vyombo vya upatanisho, huruma na upendo wa Mungu na kamwe si wamiliki wa dhamiri za waamini. Wajenge utamaduni na sanaa ya kusikiliza kwa makini, ili wawasaidie waamini wao kufanya mang’amuzi ya kina kuhusu maisha na wito wao ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake!

Baba Mtakatifu, Ijumaa jioni, tarehe 9 Machi 2018 katika Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ameadhimisha Ibada ya Upatanisho wa jumla na baadaye, kufuatiwa na maungamo na maondoleo ya dhambi kwa mwamini mmoja mmoja. Katika mahubiri yake, amewakumbusha waamini waliofurika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro kwamba, ni upendo wa Mungu unaowafanya kuwa ni watoto wapendwa wa Mungu, kiasi hata cha kuvuka udhaifu na mapungufu ya binadamu, yanayoisuta dhamiri nyofu. Huu ni upendo usiokuwa na mipaka wala vizingiti kama vinavyoweza kuwekwa na binadamu kwa hofu kwamba, pengine uhuru wao utamezwa.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, dhambi inamtenganisha mwamini na Mwenyezi Mungu, lakini Mungu mwenyewe anaendelea kuwa mwaminifu na karibu zaidi kwa watoto wake. Uhakika huu, uwe ni dira na mwongozo wa maisha ya waamini kukimbilia na kuambata daima upendo wa Mungu katika maisha yao, kwani anapenda kuwatuliza kwa maana Mungu ni mkuu kuliko mioyo yao na kwamba, anajua yote. Neema yake inaendelea kutenda kazi ili kuwaimarisha waja wake katika fadhila ya matumaini, ili kamwe wasitindikiwe na upendo, licha ya dhambi wanazotenda kwa kukataa kutambua uwepo wake katika maisha yao.

Ni matumaini haya yanayowasukuma waamini kuchunguza dhamiri zao, ili kuangalia ni mahali gani ambapo wameteleza na kuanguka kama alivyofanya Mtakatifu Petro baada ya kumkana Yesu  mara tatu, akasutwa na dhamiri yake kwa kuyakumbuka maneno ya Kristo Yesu kwamba, angemkana mara tatu! Petro mtume, akatoka nje ya baraza na kuanza kulia kwa majonzi! Mwinjili Mathayo anakaza kusema, Petro mtume alimkana Yesu na katika machozi ya uchungu na majonzi, akamwona Mwenyezi Mungu aliyejifunua kwa njia ya Kristo Yesu aliyekuwa anateswa, anatukanwa na kukanwa na wanafunzi wake na kutokana na upendo wake, alikuwa analiendea fumbo la kifo kwa ujasiri mkuu.

Baba Mtakatifu anaendelea kukaza kwa kusema kwamba, Petro mtume, aliyejigamba mbele ya wanafunzi wengine kwamba, angesadaka maisha yake kwa ajili ya Kristo Yesu, akajikuta ananyong’onyea na “kuwa mdogo sana kuliko hata kidonge cha pilitoni!”. Akatambua kwamba, Kristo Yesu, Bwana na Mwalimu alikuwa anasadaka maisha yake kwa ajili ya maondoleo ya dhambi za binadamu! Petro mtume, hakulitambua hili na wala hakutaka hata kidogo liingie akilini mwake. Lakini, mwishoni, Petro mtume akakumbana mubashara na upendo wa Kristo, akajiachilia mwenyewe kuzama katika upendo ili kuokolewa na Kristo Yesu, aliyempenda upeo!

Mwishoni, Baba Mtakatifu anasikitika kusema, ni vigumu sana kwa binadamu kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu ili aweze kuonja huruma na upendo wake usiokuwa na mipaka. Hii inatokana na ukweli kwamba, binadamu mbele ya Mwenyezi Mungu, daima anajiona kuwa anadaiwa mambo mengi, lakini Mungu ndiye anayechukua hatua ya kwanza ili kumwokoa na kumpenda mwanadamu. Waamini wanaalikwa kumwomba Mwenyezi Mungu neema ya kutambua ukuu wa upendo wake unaosamehe na kufuta dhambi zote! Daima wakimbilie huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, ili aweze kuwatakasa na kwa njia hii, wataweza kuonja upendo wa Mungu katika maisha yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

12/03/2018 11:22