2018-03-12 12:33:00

Papa Francisko mwezi Septemba 2018 kutembelea nchi za Baltic!


Baba Mtakatifu Francisko amekubali mwaliko uliotolewa kwake na Baraza la Maaskofu Katoliki kutoka katika Nchi za Lithuania, Latvia na Estonia pamoja na wakuu wao wa nchi ili kutembelea nchi hizi zilizoko kwenye Ukanda wa Baltic kuanzia tarehe 22 hadi tarehe 25 Septemba 2018. Hii ni taarifa iliyotolewa na DR. Greg Burke, Msemaji mkuu wa Vatican. Amefafanua kwamba, Baba Mtakatifu akiwa kwenye Nchi za Baltic, atatembelea miji ya Vilnius na Kaunas huko Lithuania; Riga na Aglona iliyoko Latvia na hatimaye, mji wa Tallin ulioko huko nchini Estonia.

Kauli mbiu inayoongoza hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Lithuania ni “Kristo Yesu, ni tumaini letu”. Kauli mbiu ya Latvia inajikita katika tunza na ulinzi wa Bikira Maria yaani “Jioneshe Mama Yetu” sala kutoka katika Mapokeo ya Kanisa yanayomtaja Bikira Maria kuwa ni “Nyota ya Bahari”. Kauli mbiu ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko huko Estonia ni “Amka Ee Moyo wangu” maneno kutoka katika wimbo wa maisha ya kiroho uliotungwa na Bwana Cyrillus Kreek.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Zbigņevs Stankevičs wa Jimbo kuu la Riga, nchini  Latvia, anapenda kuchukua nafasi hii kumshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko ambaye ameamua kwenda kuwatia shime katika maisha na utume wao, wakati huu Kanisa katika Ukanda huu linaendelea kuboresha maisha na utume wake, licha ya shida na changamoto nyingi zinazoendelea kujitokeza mbele yao! Tangu mwanzo wa utume na maisha yake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, ametoa kipaumbele cha pekee kwa Makanisa yaliyoko pembezoni mwa Jumuiya ya Mataifa, ili kuyainua tena, yatari kutekeleza dhamana na wajibu wake wa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu anatembelea nchi ya Latvia, wakati huu inapoadhimisha Jubilei ya Miaka 100 ya Latvia. Uwepo wa Baba Mtakatifu kati yao itakuwa ni changamoto ya toba na wongofu wa ndani, tayari kujizatiti kikamilifu katika kusimamia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kama anavyokaza kusema Askofu Viktors Stulpins wa Jimbo Katoliki la Liepaja, lililoko nchini Latvia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.