Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Hotuba

Mwanaume na mwanamke wanakamilishana kama sura na mfano wa Mungu

Mwanaume na mwanamke wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na wanakamilishana katika maisha na wito wao kwa kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.

12/03/2018 12:15

Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini, CAL, Jumamosi, tarehe 9 Machi 2018, imehitimisha mkutano wake wa mwaka mjini Vatican kwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko aliyewatia shime wanawake, kuendelea kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu Amerika ya Kusini. Mkutano huu umeongozwa na kauli mbiu “Mwanamke, mhimili wa ujenzi wa Kanisa na Jamii Amerika ya Kusini”. Kardinali Marc Ouellet, Rais wa Tume, anasema, Kanisa linahimiza mshikamano na mkamilishano kati ya wanawake na wanaume walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wanawajibika kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia ambazo kwa sasa zinakabiliwa na changamoto kubwa ya utandawazi na utamaduni wa kifo!

Fumbo la Utatu Mtakatifu kama anavyofafanua Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia” umoja, upendo na mshikamano ni mihimili mikuu ya maisha na utume wa ndoa na familia kama anavyofundisha Mtume Paulo anapowaandikia Wakristo wa Efeso kwa kukazia upya wa maisha ya kidugu ndani ya familia. Haya ni maisha yanayofumbatwa katika unyenyekevu, utii, upendo, msamaha, utakaso pamoja na udumifu kwani hii ni siri kubwa inayofumbatwa katika Fumbo la Kristo na Kanisa lake.

Haya ni mahusiano yanayopaswa kuangaliwa kwa mizani ya upendo kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu ili kushiriki katika kazi ya uumbaji. Matokeo ya umoja, ushirikiano na upendo huu ni watoto ambao kimsingi ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Umoja na mshikamano huu umefunuliwa kwa namna ya ajabu katika Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu alipotwaa mwili na kukaa kwake Bikira Maria, akawa ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili. Bikira Maria akawa ni Mama wa Mungu na Kanisa, ndiyo maana hata wanawake ni mihimili mikuu ya maisha na utume wa Kanisa hata katika ulimwengu mamboleo.

Mwanamke anao mchango mkubwa sana kama: mama mzazi na mlezi; daraja na mpatanishi wa watu. Mwanamke anao wajibu mkubwa katika maisha ya kijamii na kikanisa. Ni watu waliobahatika kuwa na karama ya kusikiliza kwa makini; wakweli na watu wazi; wepesi kusamehe na kusahau tayari kuanza mchakato wa maisha mapya. Umefika wakati anasema Kardinali Marc Ouellet, kwa viongozi wa serikali na kijamii kuhakikisha kwamba, wanathamini mchango wa wanawake katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kanisa katika maisha na utume wake, limeendelea kuwa mstari wa mbele katika kupigania haki msingi za wanawake, utu na heshima yao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Wanawake wanawapaswa kupewa ajira na mshahara sawa katika maeneo ya kazi; kwa kuthamini mchango na dhamana yao katika maisha ya ndoa na familia bila kutumbukizwa katika dhana ya ukoloni mamboleo unaotoka kuwafisha wanawake na kuwageuza kuwa kama kichoko cha kuridhisha tamaa za wanaume. Kuna tofauti kubwa kati ya mwanaume na mwanamke, lakini wote wanakanilishana, ili kukuza na kuendeleza ile sura na mfano wa Mungu katika maisha yao! Kukengeuka na kutopea katika ubinafsi, kutasababisha maafa makubwa kwa familia ya binadamu inayoweza kumezwa na utamaduni wa kifo kwa watu kukengeuka na kumsahau Mungu.

Kwa upande wake, Professa Guzman Carriquiri Lecour, Katibu mkuu wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini, CAL, anasema, kwa bahati mbaya kwa miaka mingi wanawake Amerika ya Kusini wamebaguliwa na hatimaye kusahaulika kwa kumezwa na mfumo dume. Lakini, wanawake wamekuwa na mchango mkubwa katika maisha ya ndoa na familia, kwa kushiriki kikamilifu katika utume wa Kanisa na jamii kwa ujumla, kwa kumwiga Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Kumekuwepo na kundi kubwa la wanawake walei ambao wamejipambanua kwa: ari, maisha na utume wao kama wamisionari na wahubiri wakuu wa maisha ya kiroho.

Ni wanawake wa shoka waliojitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kufundisha na kuwahudumia wagonjwa hospitalini; wakawa ni chemchemi ya huruma ya Mungu kwa watu wa Mataifa. Hawa ni wanawake watawa na wamisionari walioenea sehemu mbali mbali za dunia. Kumekuwepo na wanawake walio bahatika kupata nafasi kama wabunge na hivyo kushiriki katika kutunga sheria za nchi mbali mbali Amerika ya Kusini, kati yao ni Mtakatifu Catarina. Ni wanawake waliothubutu kusimama kutetea haki msingi za binadamu kama walivyofanya nchini Cuba, hadi kikaeleweka! Professa Guzman Carriquiri Lecour anakaza kusema, kuna mamilioni ya wanawake wanaofanya kazi kubwa sana huko Amerika ya Kusini, lakini hata siku moja, hawataweza kutajwa kwenye vyombo vya mawasiliano ya jamii, lakini hawa ndio wanawake wa shoka ambao wamekuwa mstari wa mbele kurithisha: imani, maadili na utu wema; wamejenga na kudumisha umoja, mshikamano na maridhiano ya watu ndani ya jamii. Kimsingi wanawake ni wajenzi wa utamaduni wa watu kukutana, ili kuishi kwa amani, furaha na upendo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

12/03/2018 12:15