2018-03-09 15:10:00

Unyenyekevu wa Kikristo unajenga na kupyaisha maisha na jumuiya!


Unyenyekevu na upendo katika jumuiya viwasaidie waamini wasinie makuu kupita inavyowapasa kunia; bali wawe na nia ya kiasi, kama Mwenyezi Mungu alivyomgawia kila mtu kiasi cha imani. Fadhila ya unyenyekevu inafumbatwa katika kiasi, ili kumwezesha mwamini kutumia vyema akili na utashi wake kutenda mema na kuepuka dhambi. Waamini wawe na mizani sahihi ya kupima maisha na uwezo wao mintarafu fadhila ya unyenyekevu kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria katika utenzi wake wa “Maginificat. Waamini wanakumbushwa kwamba, hakuna unyenyekevu pasi na kunyenyekeshwa!

Haya ni mawazo makuu yaliyotolewa na Padre Raniero Cantalamessa, mhubiri wa nyumba ya kipapa, Ijumaa, tarehe 9 Machi 2018 wakati wa mahubiri, awamu ya tatu, Kipindi cha Kwaresima, yaliyohudhuriwa na Baba Mtakatifu Francisko, wajumbe wa Sekretarieti kuu ya Vatican pamoja na wakuu wa mashirika ya kitawa na kitume yaliyoko mjini Roma. Mahubiri haya yameongozwa na kauli mbiu “…kila mtu aliyeko kwenu asinie makuu kupita ilivyompasa kunia; bali awe na nia ya kiasi” . Rum. 12:3. Haya ni mafundisho yanayotolewa na Mtakatifu Paulo juu ya mwelekeo sahihi wa fadhila ya unyenyekevu inayofumbatwa katika upendo kama chachu muhimu sana ya kupyaisha maisha ya kijumuiya na katika ngazi ya mtu binafsi mintarafu mwanga wa Roho Mtakatifu.

Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha Kristo Yesu, aliyejinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya Msalaba. Mtume Paulo anakaza kusema, Kristo Yesu ndiye mfano halisi wa fadhila ya unyenyekevu, changamoto na mwaliko kwa wakristo kujitahidi kuwa na moyo wa Kristo! Unyenyekevu unafumbatwa katika kiasi, kwa kuratibu akili na utashi kadiri ya uwezo na dhamana ambayo Mwenyezi mungu amemkirimia mja wake. Katika Agano la Kale, Mwenyezi Mungu anaoneshwa kuwabeza watu wenye dharau na kuwapatia neema wanyenyekevu. Ingawa Mwenyezi Mungu yuko juu, lakini anamwona mnyenyekevu, naye anamjua mwenye kujivuna kutokea mbali. Mwenyezi Mungu anawapenda wanyenyekevu kwani ni watu wakweli wasiokuwa na hila nyoyoni mwao. Majivuno katika maisha ya Kikristo ni mzizi wa dhambi. Padre Cantalamessa anakaza kusema, ilikuwa ni vigumu sana kwa wanafalsafa wa Kigiriki kupokea dhana ya unyenyekevu katika maisha yao, kwani waliihusisha na kazi ya uumbaji pamoja na dhambi!

Lakini, Mtakatifu Paulo katika Agano Jipya, anakazia fadhila ya unyenyekevu unaofumbatwa katika ukweli na kiasi kama kielelezo cha hekima inayowawezesha wakristo kuwa na kiasi. Hii inatokana na ukweli kwamba, mtu wenye hekima na busara daima atatenda kwa unyenyekevu na hivyo kumkaribia Mwenyezi Mungu katika maisha yake, kwani Mungu ni mwanga na ukweli wote! Mtakatifu Paulo anawataka Wakristo kuzama zaidi katika maisha yao ili kutambua dhambi na nafasi zake kwa maana mtu akijiona kuwa ni kitu, naye si mali kitu, anajidanganya nafsi yake. Mtu anapaswa kuwa na mizani halisi ya kupima na kupembua maisha yake kwa njia ya unyenyekevu, daima akitoa nafasi ya kwanza kwa uwepo wa Kristo Yesu katika maisha yake.

Tabia ya watu kutaka kujikweza kupita kiasi ni dhambi inayowapekenya watu wengi, kielelezo kwamba, wananyemelewa na dhambi, ili kujikweza kwa kujitafutia umaarufu usiokuwa na mvuto wala mashiko! Unyenyekevu unamwezesha mwamini kuwa na amani na utulivu wa ndani katika maisha na maamuzi yake. Unyenyekevu ni ngome thabiti katika maisha ya Kikristo, ndiyo maana Mtakatifu Paulo anawataka Wakristo kutotenda neno lolote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake. Huu ndio mwelekeo sahihi unaowawezesha waamini kuambata utakatifu wa maisha, vinginevyo watapekenywa na ubinafsi na kumezwa na uchoyo.

Bikira Maria ni mfano na kielelezo makini cha fadhila ya unyenyekevu anayoishuhudia katika utenzi wake wa “Magnificat” kwa kutambua mambo makuu ambayo Mwenyezi Mungu amemtendea katika maisha: kwa kumkingia dhambi ya asili, kwa kumpatia nafasi ya kushiriki katika kazi ya ukombozi, kwa kuwa ni Mama wa Mungu na Kanisa. Kwa hakika, Bikira Maria ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha neema na fadhila ya unyenyekevu kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Padre Cantalamessa anakaza kusema, hakuna unyenyekevu bila kunyenyekeshwa, ili kutambua udhaifu na mapungufu yanayoweza kujitokeza katika maisha ya Kikristo. Hii ni njia makini ya kukumbatia fadhila ya unyenyekevu katika ukweli na uwazi, ili kuondokana na hali ya mtu kutaka kujikweza! Waamini wahamasike kutafuta na kutekeleza utukufu wa Mungu katika maisha yao. Unyenyekevu ni mapambano endelevu katika maisha, vinginevyo, waamini watajenga kiburi na ubinafsi. Lakini kwa njia ya neema na baraka ya Mungu, waamini wanaweza kutoka kifua mbele wakiwa ni washindi katika vita hii baada ya kunyenyekeshwa, ili kuuvua utu wao wa kale na kuanza kutembea katika utu mpya na unyofu wa moyo kama njia ya kumfuasa Kristo Yesu na kulitumikia Kanisa.

Waamini wajifunze kujaribiwa katika imani, ili waonekane kuwa wenye sifa, utukufu na heshima kwa kufunuliwa kwake Kristo Yesu. Unyenyekevu ni hija inayompeleka mwamini katika utakatifu wa maisha kwa kukumbatia mambo msingi katika maisha, tayari kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa jumuiya na Kanisa katika ujumla wake. Unyenyekevu ni mwanga katika maisha na utume wa Kanisa unaomwezesha Mwenyezi Mungu kuwafunda watu wake katika amani na utulivu wa ndani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.