Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Maisha Ya Kanisa Afrika

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania: Maelekezo muhimu!

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania: Kilele cha Jubilei Jumapili tarehe 7 Oktoba, 2018. Kauli mbiu: Miaka 150 ya Uinjilishaji, Furaha ya Injili. - REUTERS

09/03/2018 15:30

Katika kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2018, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujiuliza maswali msingi kuhusu hatima ya maisha yao kwa kuzingatia mambo makuu yafuatayo: Kuhusu sababu ya kwanza, ni lazima tunapoadhimisha miaka 150 ya Ukatoliki Tanzania Bara tujiulize hilo swali kwa namna ifuatayo: “Je, sisi Wakatoliki katika kipindi hicho cha miaka 150 tumekuwa walinzi wa binadamu wenzetu, ambao tumefanywa kuwa ndugu zao kama Familia ya Mungu kupitia Mwanae Yesu Kristo na Mama yetu Bikira Maria?”.

Kuhusu sababu ya pili, tujiulize swali hilo hilo kama ifuatavyo: “Je, katika kipindi hicho cha miaka hamsini, kuanzia 1968 mpaka mwaka huu 2018, sisi Wakatoliki tumekuza roho na moyo wa kuwajali binadamu kama ndugu zetu, kuendana na barua ya kichungaji ya mwaka huo, yenye kichwa cha habari The Church and Developing Society of Tanzania,  iliyotuasa kuwa falsafa na imani ya Azimio la Arusha, Azimio ambalo lilitoa mwelekeo na hatima ya nchi yetu, inakubaliana kwa karibu kabisa na ( kwa kunukuu sehemu ya ujumbe huo) “roho ya kweli ya Kristo na Kanisa, roho ambayo ni ya udugu, ya kumegeana, ya kuhudumiana na ya kufanya kazi kwa bidii?” Kwa kusisitiza ukaribu huo kati ya Azimio la Arusha na roho ya kweli ya Kikristo, barua hiyo ya kichungaji ilizingatia barua ya Yakobo, 2:14-17 inayosema kuwa imani bila matendo ni imani mfu!

Kuhusu sababu ya tatu, baada ya kufanya toba na kusherehekea Ufufuko wa Bwana Wetu Yesu Kristo, tukiwa na ari na mwelekeo mpya wa maisha ya Kikristo yanayodhirishwa na imani hai, swali hilo tulihusishe na dhamira ya kweli ya viongozi wetu watarajiwa wa serikali za mitaa, kwa kujiuliza, “Mwaka huu wa maandalizi ya kuchagua viongozi wa serikali zetu za mitaa, vijiji na vitongoji, tufanye nini ili maandalizi yetu ya uchaguzi yatupe viongozi wetu wa karibu ambao hawatakwepa wajibu wao kwa kujitetea kwa mtazamo wa swali kama hilo?” Hivyo basi, ili kuhakisha kuwa tuna pata majibu ya kweli na yenye kuleta mabadiliko katika nafsi zetu na mahusiano na mashirikiano katika jamii yetu, ujumbe huu wa Kwaresima una lengo la kuwahimiza, kuwahamasisha na hata kuwadai waumini Wakatoliki wote kuuitikia kwa moyo wa toba, mageuzi na kushiriki kwa kujitoa zaidi katika uinjilishaji wa nchi yetu kama mwanga na chumvi ya ulimwengu wa Tanzania.

Maelekezo Muhimu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Kuhusiana na Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Ukatoliki Tanzania Bara linasema, kilele cha maadhimisho haya ni Jumapili tarehe 7 Oktoba 2018 huko Bagamoyo na wala si tena tarehe 2 Oktoba kama ilivyokuwa imetangazwa hapo awali kwenye Ujumbe wa Kwaresima kwa Mwaka 2018. Pili, Mapadre, Watawa na Waamini walei wote wanaalikwa kujiandaa na kushiriki kwa: Ibada na Hija; na kwa hali na mali katika maadhimisho ya Jubilei hii katika ngazi ya Parokia, Jimbo, Kanda na Taifa huko Bagamoyo, mlango wa imani na matumaini kwa watu wa Mungu Afrika ya Mashariki. Aidha, Dominika ya 4 Kwaresima mwaka huu, yaani tarehe 11 Machi 2018, sadaka zote za misa za siku hiyo kwa nchi nzima zitakusanywa na kuwasilishwa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ili kusaidia maandalizi ya maadhimisho ya Jubilei hii. Hakutakuwa na michango mingine yoyote ya kiparokia siku hiyo. Sadaka yote ya kwanza na ya pili ikusanywe na kupelekwa Jimboni ili iweze kuwasilishwa Taifani. 

Tatu, Makundi mbalimbali ya Familia ya Mungu yanatakiwa kufanya maadhimisho ya Jubilei hii katika ngazi ya Jimbo katika tarehe zilizotajwa katika barua iliyoambatanishwa hapo chini. Tarehe hizi za maadhimisho ni kwa nchi nzima. Mwishoni, waamini wanahimizwa kuisali Sala Maalum ya Jubilei katika parokia, jumuiya na katika vyama vyao vya kitume ambayo tayari imekwisha kutumwa Majimboni na Parokiani. Kauli mbiu ya Jubilei: Miaka 150 ya Uinjilishaji, Furaha ya Injili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

09/03/2018 15:30