Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Hotuba

Viongozi na walezi seminarini acheni tabia ya kutenda kazi kwa mazoea

Papa Francisko anawataka viongozi na walezi seminarini kuachana na tabia ya kutenda kazi kwa mazoea kwani imepitwa na wakati.

08/03/2018 15:36

Kuna haja ya kushikamana na kutembea kwa pamoja kama ndugu kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko Barani Ulaya. Watu kama vile Mapadre wana imani na matumaini kwa amana na utajiri mkubwa unaofumbatwa katika maisha na utume wa wakuu wa seminari na nyumba za malezi waliopewa dhamana ya kuwafunda majandokasisi kwa ajili ya maisha na utume wa Kipadre. Lakini, kutokana na utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, leo hii, kuna tamaduni mpya zinazoendelea kuibuka nje kabisa ya ufahamu, uelewa na mitindo iliyokuwa inafahamika na wakuu wengi wa Seminari kwa nyakati zao. 

Changamoto kubwa iliyoko mbele ya walezi ni kuondokana na tabia ya kutenda kwa mazoea, ili kuyaelekeza macho yao kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Katika madonda yake matakatifu kama yalivyo pia madonda ya walimwengu, viongozi wa Kanisa waweze kuona na kutambua alama za ufufuko, changamoto na mwaliko wa kuendelea kufanya hija kama mashuhuda na Injili ya matumaini! Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 8 Machi 2018 wakati alipokutana na kuzungumza na wajumbe wanaoshiriki mkutano wa Magombera kutoka katika seminari zinazozungumza lugha ya Kijerumani.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, wito ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kamwe hawawezi kuutengeneza, bali wao wanaweza kuwa ni mashuhuda wa wito wa huruma ya Mungu katika maisha yao, anayewaita kutoka katika ubinafsi wao, ili kukutana na watu katika uhalisia wao; watu wanaohitaji uwepo wa karibu kutoka kwa jirani zao pamoja na ukaribu wa Mungu katika maisha yao, kwani wote wanaitwa kutengeneza familia kubwa ya watu wa Mungu. Hii ndiyo Jumuiya ambayo itaweza kuwategemeza ili kujibu na kutekeleza kwa moyo wote wito kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewadhaminisha Magombera pamoja na majandokasisi wanaojiandaa kwa ajili ya maisha, wito na utume wa Kipadre kutoka katika nchi zinazozungumza Kijerumaini chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

08/03/2018 15:36