Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Hotuba

Toba na wongofu wa kiekolojia ili kutunza mazingira nyumba ya wote!

Toba na wongofu wa ndani ni muhimu katika kulinda, kutunza na kudumisha mazingira nyumba ya wote na kwamba, uchafuzi na uharibifu wa mazingira ni dhambi mbele ya Mwenyezi Mungu. - AP

08/03/2018 10:00

Chuo kikuu cha Kipapa cha Gregoriani kilichoko mjini Roma, kwa kushirikiana na ubalozi wa Ujerumani, Georgia na nchi za Scandinavia kwa siku mbili kuanzia tarehe 7 hadi 8 Machi 2018, kinafanya mkutano wa kimataifa unaoongozwa na kauli mbiu “Wongofu wa dhati wa kiekolojia baada ya Waraka wa Kitume, Laudato si” uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko. Mkutano huu pamoja na mambo mengine, unapania kuibua mbinu mkakati utakaosaidia kuleta toba na wongofu wa ndani wa kiekolojia katika maisha ya watu binafsi, kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Mkutano huu umekuwa pia ni mwanzo wa kuzindua shahada ya utunzaji bora wa mazingira itakayokuwa inatolewa na vyuo vikuu vya kipapa vilivyoko mjini Roma katika kipindi cha miaka mitano, ili kuhakikisha kwamba, mafundisho ya Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” yanafahamika na wengi. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa washiriki wa mkutano huu, anawatakia heri na baraka katika kipindi hiki cha Kwaresima, ambamo Mama Kanisa anawaalika watoto wake kutubu na kumwongokea Mungu kama njia muafaka ya kupyaisha maisha ya Kikristo sanjari na uwajibikaji wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Ni matumaini yake kwamba, wajumbe wataweza kupata fursa ya kushirikisha wengine uzuri na utakatifu wa kazi ya uumbaji ambao ni kielelezo madhubuti cha mpango wa upendo, huruma na ukuu wa Mungu.

Kwa upande wake, Patriaki Bartolomeo wa kwanza, wa Kanisa la Kiothodox la Costantinopoli, katika ujumbe wake kwa washiriki wa mkutano huu anakaza kusema, uchafuzi na uharibifu wa mazingira ni dhambi! Kumbe, kuna haja ya kupembua kwa kina na mapana tunu msingi za kazi ya uumbaji ili kuibua mbinu mkakati utakaosaidia kulinda, kutunza, kudumisha na kuadhimisha utimilifu wa mazingira bora kama kielelezo cha kazi ya uumbaji. Anasema, kwa miaka ya hivi karibuni viongozi wa Makanisa wamekuwa mstari wa mbele katika mchakato wa kuragibisha utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, watambue dhamana na wajibu wa kulinda na kutunza mazingira kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Utunzaji bora wa mazingira uwe ni kielezo cha upendo na mshikamano kwa jirani ili kuondokana na dhambi ya kutaka kuwanyonya watu wengine, kama ilivyo pia hata katika mazingira kwa kutaka kupora rasilimali hii adhimu kwa ajili ya mafao binafsi. Hapa kuna haja ya kufanya “metanoia” yaani “kutubu na kumwongokea Mungu” mintarafu ekolojia!

Mahubiri na sala zinapaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha. Ni jambo la kusikitisha kuona kwamba, watu wanasali kwa ajili ya kuombea amani, lakini wengine, mawazo na malengo yao yako katika kutengeneza silaha za maangamizi kwa ajili ya mafao binafsi. Toba na wongofu wa ndani ni sawa na chanda na pete, kwani haiwezekani kuwatumikia mabwana wawili! Kwa upande wake, Padre Nuno da Silva Goncalves, S.J. katika hotuba yake ya ufunguzi , amewashukuru wale wote waliojisadaka ili kuhakikisha kwamba, mkutano huu unafanyika sanjari na kuzindua “Shahada ya Ekolojia Endelevu”, changamoto iliyovaliwa njuga na Padre Prem Xalxo, kama changamoto pevu ya elimu ya ekolojia na maisha ya kiroho ili kukuza na kudumisha agano kati ya mwanadamu na mazingira. Ndoto ya Mwenyezi Mungu kwa kila kiumbe ni: utulivu, haki na uzuri mambo yanayowezekana ikiwa kama mwanadamu atajizatiti katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

08/03/2018 10:00